Home Makala Fukuto CUF: Mwendelezo wa kudhoofisha Ukawa

Fukuto CUF: Mwendelezo wa kudhoofisha Ukawa

893
0
SHARE

DSC_5707NA BALINAGWE MWAMBUNGU

BINADAMU wanasema ni mnyama wa kisiasa—huwezi kumtenganisha na siasa kwa sababu siasa ndio msingi wa maisha yake yote. Wanasiasa wanapenda kutumia nguvu za kisiasa ili kufikia malengo yao ya kukamata dola. Walio wengi wanafurahi kama mahasimu wao wa kisiasa wanapata shida—wanahujumiwa na kuteseka au kuanguka.

Hii inatokana na ukweli kwamba, siasa ni ushindani, na mwenye kumzidi mwenzake ujanja na mbinu katika medani za siasa, ndiye ananyakua ushindi.

Katika siasa za Kiafrika, wanasiasa wanapenda na wanafurahi kama chama pinzani kinapata madhila, wao wakidhani wamesimama imara. Wanasahau kabisa usemi wa Wahenga: Ukiona mwenzako ananyolewa, wewe tia maji.

Naweza kutabiri kwamba fukuto linaloendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), ni mwendelezo wa ajenda iliyosukwa kabla ya Uchaguzi Mkuu (2015), wa kukihujumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)—mpango ambao kwa jumla ulishindwa—ingawaje kwa kiasi fulani ulikiathiri. Lakini kwa yeyote anayekitazama chama hicho kilivyokuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu, ataona kwamba kimejijenga zaidi, kina nguvu zaidi. Chadema hivi sasa kina Wabunge na Madiwani wengi zaidi.

Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), ambavyo vilifanya fungamano pale Jangwani, Dar es Salaam kabla ya Uchaguzi Mkuu, na kukubaliana kwamba vitafanya kazi kwa pamoja, ili kupigana na chama tawala—Chama Cha Mapinduzi (CCM)  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vilichukulia tatizo la sasa la fukuto na mpasuko ndani ya CUF kama fursa ya kuendeleza mageuzi.

Namwona Profesa Ibrahim Lipumba akiudhoofisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa sababu alipojivua uongozi wa CUF, ni moja kwa moja alijivua uwenyekiti wenza wa Ukawa. Halafu amenukuliwa na vyombo vya habari kwamba hataweza kufanya kazi na aliyekuwa mgombea wa urais chini ya mwamvuli wa UKAWA, Edward Lowassa.

Wakati anajiuzulu, Lipumba alisema anasutwa na nafsi, kwa kitendo cha UKAWA kumteua Lowassa kuwa mgombea urais, wakati alishiriki katika majadiliano ya kumkaribisha. Profesa Lipumba akwaachia vita wenzake na kukimbilia Rwanda kusikilizia nini kitatokea. Waliosuka sakata hilo lengo lao lilikuwa kuwapunguza nguvu UKAWA.

Baada ya Dk. John Magufuli kuapishwa, Profesa Lipumba alirudi nchini kimya kimya na akawa mpinzani wa kwanza kwenda Ikulu kumpongeza, ingawaje UKAWA hawakutoa kauli ya pamoja kupinga matokeo ya uchaguzi, hawajawahi kutoa kauli ya kumpongeza Rais Magufuli kwa ushindi.

Kama UKAWA walishindwa kihalali katika uchaguzi uliopita, basi Profesa Lipumba kwa kiasi fulani, alichangia kushindwa kwao. Inajulikana kwamba UKAWA walijiwekea mkakati wa kuunganisha nguvu kutokana na ukweli kwamba hakuna chama ambacho kinaweza kusimama peke yake na kikakishinda CCM. Umoja huu ukiimarika, utaendelea kukimong’onyoa chama tawala kidogo kidogo. Wahenga walituambia: Bandu bandu huisha gogo. Mchwa ni wadudu wadogo sana, lakini kwa umoja wao, wanaweza kuangusha mbuyu—Umoja ni nguvu. Hiki ndicho kinachowatisha watawala.

Tunaelewa kwamba upepo mbaya ulikikumba chama tawala kutokana na figisu figisu au mizengwe iliyofanyika wakati wa uteuzi wa mgombea wa nafasi ya urais. Wanachama 42 wa CCM walichukua fomu za kuomba kuteuliwa, lakini hakuna hata mmoja aliyeitwa kuhojiwa na Kamati Kuu. Badala yake Kamati Kuu ikatoka na majina matano (5) ili yakapigiwe kura na Halmashauri Kuu.

Jina lililokuwa midomoni mwa wajumbe wengi wa NEC na Umoja wa Vijana wa CCM, ni la Edward Lowassa, na wengi walipata mshituko—jina la Lowassa halikuwamo katika majina yale matano.  Jeshi la Polisi ambalo mara zote linaonekana kuibeba CCM tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (1995),  kwa mara ya kwanza, askari walitembeza virungu na kupiga mabomu ya moshi dhidi ya vijana wa CCM ambao walikuwa wametayarishwa kwa shamra shamra za kumpokea Lowassa.

Wajumbe wa NEC walipiga kura za hasira, kumkataa aliyekuwa mpinzani mkuu wa Lowassa na ambaye iliaminika ndiye lilikuwa chaguo la Rais Jakaya Kikwete—Bernard Membe, na badala yake akachomoza Dk. John Magufuli.

Pamoja na UKAWA kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja, lakini kila chama kilikubali kupendekeza mgombea mmoja, na halafu viongozi wangelikaa na kuteua jina moja tu—ambaye ndiye angebeba bendera ya chama kimoja wapo, lakini akiungwa mkono na vyama vingine.

Majina mawili makubwa yalikuwa yakitajwa—Dk. Slaa ambaye alikuwa Katibu Mkuu (Chadema) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba. Jina la mgombea wa NCCR-Mageuzi halikuwa maarufu. Kwa hiyo watu hawa wawili—Dk. Slaa na Profesa Lipumba—walijua kuwa urais ulikuwa unanukia. Lakini, Chadema wakamwendea Lowassa na kumwomba ahamie kwao. Hii ilitokana na ukweli kwamba wananchi wengi ndani na nje ya CCM, walikuwa wanamkubali na wanamkubali Lowassa.

Ujio wa Lowassa kwenye UKAWA ndio uliowavuruga Profesa Lipumba na Slaa. Pamoja na kwamba walishiriki katika mazungumzo ya kumkaribisha Lowassa, Profesa Lipumba na Dk. Slaa kwa ubinafsi wao na uchu wa madaraka, wakimbilia nje ya nchi na kusema kwamba nafsi zao zilikuwa zinawasuta.

Zilikuwa zinawasuta kwa kuwa walitegemea kuukwaa urais, halafu ghafla anatokea mtu, tena kutoka CCM—anateuliwa kupeperusha bendera ya Chadema kwa niaba ya UKAWA! Kuushinda ubinafsi ni kazi kubwa sana.

Chadema kilipita kwenye wakati mgumu—kuondokewa na Dk. Slaa ambaye alikuwa ndiye roho ya chama, na CUF kuondokewa na Mwenyekiti Profesa Lipumba—lakini kwa kwa upande wa Zanzibar, hapakuwa na shida. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ni kipenzi cha Wazanzibari na alikuwa hana wasi wasi.

Kwa upande wa Tanganyika, kwa kuwa wananchi walikuwa wamekichoka chama tawala—wakasema potelea mbali, tutaenda na Lowassa hata kama alikuwa ni ‘fisadi’ na mgonjwa—kauli zilizokuwa zinaimbwa na CCM.

Lakini hata baada ya uchaguzi kupita, mbinu chafu zimeendelea kupangwa dhidi ya Chadema na hii inatokana na ukweli kwamba Lowassa ana nguvu hata ndani ya CCM. Ushahidi ni jina lake kutajwa mara nyingi katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika Dodoma Julai, 2016.

Hili la ujio wa Profesa Lipumba kwenye CUF, ni mwendelezo wa figisu ambazo hazikuzaa matunda tarajiwa ya mwaka 2015 ya kukisambaratisha Chadema. Mkakati wa sasa ni dhoofisha UKAWA kama sio kuusambaratisha.

Profesa Lipumba hakutafuta ridhaa kwa waliokuwa wamempa kazi. Alijiamulia mwenyewe—hakusema anaomba kujiuzulu. Alisema ameamua kuachia ngazi, tena kwa barua rasmi—maana alijua kuwa angeomba kujiuzulu, CUF wangemkatalia kwa kuwa walikuwa katikati ya vita.

Mwaka mmoja baadaye, Profesa Lipumba anasema anarudi kwenye nafasi yake, ipi? Uchaguzi ndani ya CUF ulikuwa unakaribia, yeye angeomba nafasi ya mwenyekiti, lakini sio kudai nafasi aliyoiacha.

Sakata linaloendelea ndani ya CUF hivi sasa, ni wazi kuna mkono wa tatu wenye njama ovu ya kikivuruga chama hicho na kuivuruga UKAWA. Walifanikiwa kuwavuta pembeni Profesa Lipumba na Dk. Slaa. Chadema hakikufa, ila kimepata nguvu na kujieneza sehemu nyingi zaidi nchini. Kwa mara ya kwanza kilipata ushindi wa jimbo moja Unguja. UKAWA sasa wanaongoza halmshauri 27 za Tanganyika.

Wanasiasa wazoefu kama Edward Lowassa na Seif Sharif Hamad, kwanza wawili hawa ni makomredi—wamefanya kazi pamoja kwenye Sekreteriati za CCM enzi zile za chama kimoja—wanaijua CCM vizuri. Wautumie mgogoro huu kama fursa. Waunganishe nguvu na ikibidi wamwachie Lipumba ‘galasha’la CUF.

Maalim Seif, Mbatia, Mbowe unganisheni nguvu, Profesa Lipumba hana ubavu wa kusimama peke yake. Wako wapi wapinzani ambao kila mara waliwapinga wenzao na kuisifia CCM?

Mwaka 2020 hauko mbali—msikubali kuvurugwa. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikwishatabiri kwamba chama cha upinzani chenye nguvu, kitatokana na CCM. Hakuna aliyejua kwamba mawaziri wakuu wa wawili—Edward Lowassa na Frederick Sumaye, wangekihama CCM. Rais Magufuli amefanya kazi chini yao, anawajua na wanamjua vizuri.

Tanzania itapata chama kimoja cha upinzani chenye nguvu. Wanaofanya figisu figisu hizi—kumfanya Profesa Lipumba na wafuasi wake wa Dar es Salaam, kuwa sehehemu ya dola, watambue kwamba wanampelekea Maalim Seif urais kwenye sahani ya fedha ifikapo 2020. Tusubiri.

Nimesema mtu anayefanya njama ovu ya kutaka kukuangamiza, au anakufungia milango, ili usifanikiwe akifikiri kwamba amekukomoa—hajui kwamba Mungu huwa anafungua mlango mwingine. CUF , NCCR-Mageuzi na Chadema wayaone matatizo ya sasa kama fursa. Fanyeni tathmini kutumia SWOT (strength, weaknesses, opportunities and threats), mtapata pa kutokea.

Wala Maalim Seif asikate tamaa. Abdulaye Wade wa Senegal, aligombea urais kwa vipindi saba vya miaka saba (7), na hatimaye akafanikiwa kuwa rais akiwa na umri wa miaka 72.