Home Latest News GENGE LA WAPAMBE HATARI KULIKO KWAPA LA SHETANI

GENGE LA WAPAMBE HATARI KULIKO KWAPA LA SHETANI

5909
0
SHARE
Na Bollen Ngetti    |

Uraibu ni matokeo chanya ya ulevi wa kitu au jambo fulani kiasi cha kuwa mtumwa wake. Ukizoea kunywa pombe kupitiliza tamati unakuwa mraibu wake, kwa kimombo “addicted.” Ukianza kutumia dawa za kulevya mwisho unakuwa mraibu yaani huwezi kukaa au kufanya jambo lolote bila kutumia dawa.

Dhana ya uraibu haikomei kwenye pombe na dawa za kulevya pekee, hapana. Wapo waraibu wa picha za ngono ambao hawawezi kulala na kupata usingizi bila kuangalia picha za ponografia. Hata uvutaji wa sigara nao una uraibu wake ambapo mvutaji hawezi kukaa kwa saa kadhaa bila kuvuta sigara (chain smoker). Kimsingi uraibu ni mazoea ya jambo/kitu yaliyopitiliza.

Mimi ni mraibu wa usomaji wa vitabu hasa vyenye maudhui ya utatuzi wa matatizo na uongozi. Wakati mwingine uraibu huo umeniletea shida katika familia pale ninapojikuta natumia fedha nyingi kununua vitabu na kutumia fedha kidogo kununua mahitaji ya nyumbani! Nina wivu na usongo wa kusoma maandiko ya watu mbalimbali jambo ambalo bila shaka ni jema kwa mwandishi yeyote makini.

Si mpenzi sana wa kuangalia filamu. Lakini ikitokea basi napenda kuangalia filamu inayohusiana na mambo ya uchunguzi, ujasusi na upelelezi. Kwa mantiki hiyo ni kwamba bado sijawa mraibu wa filamu.

Hata hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita niliamua kuangalia filamu ya ki-Nigeria kupitia kituo cha ‘African Movie Channel, AMC’ inayoitwa “Mr. President.” Kila mtu aliyekuwa jirani na mimi alishangaa jinsi akili zangu zilivyokuwa zimetekwa nyara na filamu hii kiasi cha hata kusahau kula au kuongea na watu wengine ambao hawakuona sababu ya kumakinika kuangali filamu hii.

Sijui nisikitike au nifurahi kwamba kilichonitokea baada ya kuangalia filamu hii mwanzo mwisho ni kile kile kinachowatokea waraibu wa pombe, sigara, dawa za kulevya, usomaji vitabu, picha za ngono, nakadhalika. Mraibu yeyote huwa hapendi kuathirika peke yake. Waraibu si wachoyo maana hupenda kugawana uraibu na wengine, ku-“share”.

Kwamba mvuta sigara hupenda mwenzake naye avute, mnywa pombe hajisikii raha ya pombe akiwa peke yake nyumbani hivyo atalazimika kwenda baa kunywa na wengine. Waraibu wa dawa za kulevya vivyo hivyo hupenda kujichanganya na “mateja” wenzao ndipo dawa hukolea! Hata waraibu wa ponografia hupenda kuwajulisha wenzao ujio wa “picha mpya” ili wote waone.

Na mimi baada ya kukolea kuangalia filamu ya “Mr. President” iliyoigizwa mwaka 2013 huko Nigeria nimetamani kila msomaji hapa naye aiangalie kujionea kile nilichokiona ili sote tutafakari.

Katika filamu hii anaonekana Rais Abdul Sherrif (a sitting president) akimalizia muhula wake nchini Seara Leone lakini bado akitamani kuendelea kubakia madarakani kama inavyotokea leo kwa baadhi ya nchi za Afrika ambapo Urais kwao ni fursa adhimu ya kujitajirisha na si kutumikia wananchi waliokuweka madarakani.

Abdul Sherrif anaonekana kulewa chakari vinono vya Ikulu na hili linathibitika pale anapoonekana kuamka vibaya (out of mood) basi wapambe humletea wasichana wawili warembo waliovalia nusu utupu ambao hufanya kazi ya kumliwaza, kumbusu, kujionesha mbele yake, kumnywesha divai na mwisho hufanya nao ngono na ghafla Sherrif anaonekana mchangamfu na hivyo kuendelea na majukumu yake.

Rais Sherrif anaonekana kuogopwa na wananchi wake kiasi kwamba hata kutaja jina lake kama si kwa kumsifia na kumpa utukufu basi ungepotea kimya-kimya. Msafara wa Rais Sherrif ni wa kuogofya ambapo apitapo iwe ni kijijini au mjini basi wananchi hulazimishwa na vyombo vya dola kusimamisha shughuli zao na kujipanga pembezoni mwa barabara kumpungia mikono na kumshangilia.

Wananchi wake wanaonekana kukata tamaa kwa ushahidi wa maisha yao dhalili ya kifukara ambapo hawana maji safi na salama, hawana umeme, hawana barabara, hawana huduma za afya, hawana shule za maana, hawana nguo, vitendo vya uhalifu vimeshamiri kila kona ambapo wanawake na watoto hubakwa hata mchana kweupe, vibaka wametamalaki kila mahali, rushwa na ufisadi vinaonekana ni utamaduni wa kawaida chini ya utawala dhalimu wa Rais Sherrif.

Katika hali hiyo ya kukata tamaa lakini Rais Sherrif anaonekana kila mara katika dhifa mbalimbali Ikulu akiwa amezungukwa na watu mashuhuri waliovalia suti za bei ya kupaa, wenye miili iliyoshiba na kuonesha afya njema usoni, warembo na walinzi waliovalia suti za kiusalama. Magari yaliyoegeshwa Ikulu ni za kifahari huku watu wakiranda-randa katika viwanja vya Ikulu na maglasi mikononi yaliyojaa mivinyo ya kila aina kutoka nchi za Italia, Ufaransa, Ubelgiji, Afrika Kusini na kwingineko.

Ni kikundi kidogo sana cha watu lakini wenye fedha za kutisha maana zaidi ya nusu yao ni wateule wa Rais Sherrif katika nyadhifa mbalimbali wakiongozwa na mpambe namba moja anayejulikana kwa jina la Felix. Kazi kubwa ya Felix anayeonekana mpendwa wa Rais kuliko wengine ni kutafuta, kusaka mtu yeyote anayemsema vibaya Rais Sherrif au kwenda kinyume na utawala wake. Hawa adhabu yao imekuwa ni “kupotea”.

Kama ilivyo kwa Wakristo kwamba huwezi kufika kwa Baba bila kupitia kwa Yesu mwanaye mpendwa ndivyo ilivyo kwa wananchi wa Seara Leon hawakuweza kumfikia Rais Sherrif bila kupitia kwa Felix na kumueleza shida zako ambapo alikuwa na uwezo wa kukubali au kukataa. Kwa maneno mengine Felix alikuwa ni mkono wa kuume wa Sherrif. Nani kama Felix?

Felix anaonekana kijana makini, msomi, mwenye kuvutia hasa na hubadilisha magari ya kila aina ya kifahari. Felix ndie anajua Bwana Mkubwa anataka kusikia nini, anataka kugusa nini, anataka kusoma nini, anatakiwa kufanya nini na kwa wakati gani. Felix anamhakikishia Rais Sherrif jinsi asivyotakiwa kuwaza au kufikiria ni kwa namna gani ataendelea kuwa Rais maana nchi yote iko mikononi mwake.

Felix anajuana na wafanyabiashara wote wakubwa, anajuana na wanasiasa wote hata wale “wakorofi” walioonekana kumpinga Bwana Mkubwa. Katika filamu ile Felix anaonekana kutumia fedha nyingi sana kuwarubuni baadhi ya wanasiasa “wakorofi” walioonekana kuonesha nia ya kutaka kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi uliokuwa unazidi kukaribia. Felix anatembea na gari aina ya Hummer iliyojaa dola za Kimarekani akikutana na “wakorofi” wote ambao baadhi yao huchukua hela na kutokomea na wengine pia hupokea lakini wakiendeleza harakati zao za kutaka kwenda Ikulu. Hawa hukumu yao mara zote huwa mikononi mwa Felix ambao ni kifo tu.

Hata hivyo anajitokeza kijana masikini Hemed Kabiya akitaka kupambana na Rais Sherrif katika kinyang’anyiro cha Urais ambapo zimesalia siku chache kampeni zianze. Mke wa Hemed Kabiya, Zara anamuonya mumewe kuachana kabisa na mpango huo akiamini ataishia kufa tu.

Wakiwa chumbani, Zara anamuuliza Hemed Kabiya ambaye ni kutoka chama cha upinzani, “hivi wewe mume wangu niambie uko kwenye lipi kati ya haya: wewe ni masikini hatuna fedha za kampeni kuweza kumshinda Rais Sherrif je, umeiba fedha mahali unataka kufanyia kampeni? Je, una watu wanataka kukufadhili uwe rais na ukishinda utawalipa nini?” Lakini mwisho Zara anaongea kwa uchungu na kuamua kuvaa nguo nyeusi za eda kuonesha kuwa tayari mumewe atakufa tu!

Zara anasema; “unaweza ukawa na fedha, unaweza ukawa na wafadhili lakini huwezi kuwa na wa kukuokoa utakapotua mikononi mwa Felix,” kuonesha jinsi kijana huyu wa Rais Sherrif alivyoogopwa na watu wa nchi hii kuliko hata mkuu wa nchi mwenyewe. Kwa maneno mengine ni kheri kukutana na kwapa la shetani kuliko ukutane na mpambe wa Sherrif, Felix.

Hata hivyo Hameed Kabiya anajipa moyo, anaanza kampeni kwa kugawa vipeperushi vyenye jina lake katika migahawa midogo midogo, anakutana na makundi ya watu dhalili na masikini kama yeye, anakutana na vijana waliokata tamaa vijijini na mijini, anakutana na wazee na kina mama wenye watoto migongoni wakisaka maji na kuni lakini kampeni zake zikiwa za kichovu sana ukilinganisha na kampeni za Rais Sherrif.

Asubuhi moja Rais Sherrif anapitia magazeti na kisha kushikwa na ghadhabu kubwa na kumuita Felix kumuuliza hayo anayoyaona magazetini ambapo kila gazeti, televisheni na redio zimejaa jina la Hameed Kabiya. “Hivi unafanya kazi gani na timu yako kama vyombo vya habari vimejaa jina la mpinzani wangu Kabiya? Una faida gani na mimi? Kwa nini nisimteue Kamara (miongoni mwa wapambe) kuchukua nafasi yako?” anafoka Rais Sherrif huku akigida “whisky” yake.

Kwa kuwa Felix anamjua bosi wake, kwanza anaamua kuwaleta vidosho wawili nusu uchi ambao wanaingia “kumtuliza” Bwana Mkubwa kwa mahaba. Yeye Felix anaita vijana wake na kumsaka Hameed Kabiya ambaye wanakutana naye barabarani, wanamsimamisha na kumwambia, “Kabiya, jiondoe kwenye kinyang’anyiro hiki, mheshimu mkuu wa nchi, fedha hizi hapa kafanye shughuli nyingine.” Hameed Kabiya anakataa kuacha kampeni na kuhamasisha umma dhidi ya udhalimu wa Serikali ya Sherrif lakini pia anakataa kupokea fedha za Felix.”

Felix na timu yake wanaondoka na kumwambia, “lakini usije ukasema sikukuonya, endelea.”

Siku ya siku Felix na timu yake wanamteka Kabiya na kwenda naye “kusikojulikana” na huko wanampiga risasi miguuni na kuondoka. Kabiya akiwa hospitali kupitia televisheni anamuona mkewe Zara na marafiki zake wakiendelea na kampeni na kumuombea mumewe kura huku wakimtaja kama “kiongozi mwenye maono” (visionary leader) na hii ni baada ya mke kupata taarifa kuwa mumewe hakufa. Hali hii inamtia moyo kiasi cha kunyanyuka kitandani huku akibubujikwa machozi ya furaha.

Hatimaye vyombo vya usalama wa vya nchi vikamkamata Rais Sherrif akihusishwa na matukio ya kupotea kwa watu, kuuliwa ovyo kwa wapinzani wake na umasikini uliotopea. Filamu haioneshi alipelekwa wapi lakini Felix naye alipojaribu kuwatoroka askari polisi wale wale waliokuwa watiifu kwake walimfyatulia risasi mgongoni na kumuua. Mwisho wa kampeni na uchaguzi kijana Hameed Kabiya alitangazwa mshindi wa Urais kwa kupata asilimia 74 lakini yeye akiwa bado yuko kitandani akiendelea na matibabu. Hivi filamu kama hii usingependa ku-“share” na wengine?

Viongozi wengi wa Kiafrika wamelaumiwa na kulaaniwa kwa matendo maovu ya uonevu kwa watu wao. Wamewatesa wapinzani wao, wamewafunga jela wapinzani wao. Wengine wameuliwa hadharani wengine sirini. Wengine wamedhoofishwa kiuchumi, wananchi wametiwa hofu na dhana nzima ya demokrasia kutoweka na yumkini haipo tena na mifano iko tele kuanzia Kenya, Uganda, Burundi, Zimbabwe, Msumbiji nakadhalika. Hata hivyo yote haya hutendwa na genge la wapambe wachache wenye kuneemeka na vinono vya Ikulu. Tujiulize, Tanzania tuko salama? Je, hatuna genge hili la wapambe wanaonuka kwapa la shetani? Tafakari!

Mwandishi ni mchanganuzi na mtafiti masuala ya siasa na maendeleo ya jamii. Anapatikana kwa simu namba 0786 791 229