Home Latest News GEORGE WEAH: KUTOKA DIMBANI HADI IKULU

GEORGE WEAH: KUTOKA DIMBANI HADI IKULU

1459
0
SHARE

NA HILAL K SUED

BAADA ya matokeo ya uchaguzi wa Liberia wiki iliyopita kutangazwa na kuonyesha mchezaji nyota wa soka wa zamani George Weah kuwa anaongoza katika kura za urais, kuna uwezekano mkubwa wa nyota huyo kutinga Ikulu ya nchi hiyo baada ya uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba.

Ikitokea hivyo George Weah akaukwaa urais atakuwa mchezaji nyota wa soka wa kwanza duniani kuchaguliwa kuwa rais wa nchi kutokana na umaarufu wake katika fani hiyo.

Ni nadra sana duniani kwa watu maarufu kuwa wakuu wa nchi kupitia umaarufu wao unaotokana na fani zao mbalimbali kama vile michezo, muziki, uchezaji sinema, riadha na kadhalika.

Mcheza sinema wa Marekani katika miaka ya 40, Ronald Reagan alichaguliwa kuwa rais wa Marekani miaka 40 baadaye. Na mwaka 2003 mcheza sinema nyota mwingine wa huko huko Marekani, Arnold Schwarzenegger aliukwaa Ugavana wa jimbo maarufu la California.

Pamoja na umaarufu wao katika fani ya ucheza sinema, hakuna mcheza sinema yoyote wa India aliyewahi kufanikiwa katika siasa zaidi ya kuwa mbunge tu.

George Manneh Oppong Weah mwenye umri wa miaka 51 ni miongoni mwa wacheza soka mashuhuri zaidi barani Afrika na duniani, wakati wa enzi zake, katika safu ya ushambuliaji. Mwaka 1995 alipata Tuzo na kuwa Mchezaji Bora wa Fifa (Ballon d’Or), ambaye hadi sasa ni pekee kutoka Bara la Afrika kuikwaa Tuzo hiyo.

Aidha alichaguliwa mara tatu kuwa mcheza soka bora Barani Afrika – mwaka 1989, 1994 na 1995. Mwaka 1996 alitajwa kuwa mcheza soka bora wa karne kutoka Bara la Afrika. Mwaka 2004 Pele, mchezaji soka maarufu wa zamani wa Brazil alimtaja Weah kuwa miongoni mwa wacheza soka 100 maarufu zaidi duniani.

Weah amezichezea klabu maarufu za Ulaya kama vile Monaco, PSG, AC Milan, Chelsea,  Manchester City na Marseilles.

Baada ya kustaafu soka mwaka 2003, George Weah aliingia katika siasa, wakati huo nchi yake ndiyo inaanza kutulia baada ya duru la pili la vita ya wenyewe kwa wenyewe. Katika uchaguzi wa 2005 aligombea urais na alishindwa kwa kiduchu na Ellen Johnson Sirleaf katika uchaguzi wa marudio.

ELIMU YAKE

Katika uchaguzi huo, pamoja na jina lake kuwa maarufu sana nchini humo, katika kampeni wapinzani wake kisiasa walitaja suala la kutokuwa na elimu na kusena hakuwa na uwezo kuendesha masuala ya nchi ikilinganishwa na mshindani wake, Bi Ellen Johnson Sirleaf ambaye alikuwa na shahada kutoa chuo maarufu cha Harvard, Marekani.

Aidha, walitaja kutokuwa kwake na uzoefu katika masuala ya utumishi wa umma huku mshindani wake aliwahi kuwa waziri wa fedha katika utawala wa Rais William Tolbert katika miaka ya 70, na pia kushika nyadhifa kubwa kubwa katika Benki ya Citibank, Benki Kuu ya Dunia na Umoja wa Mataifa.

Kingine kilichotajwa ni kwamba hakuwa raia wa Liberia, kwani alidaiwa kuchukuwa uraia wa Ufaransa wakati akichezea klabu ya PSG ya Paris. Hata hivyo Weah alipinga madai hayo na hatimaye mahakama ilimsafisha kugombea.

Suala la Weah kutokuwa na elimu lilikuwa mithili ya mwiba kwani lilimchoma sana, hivyo akaamua kujipanga upya na kurudi darasani.

Hatimaye alisomea na kupata shahda ya Utawala wa Biashara (Degree in Business Administration) katika Chuo Kikuu cha DeVry, Miami, nchini Marekani.

Baada ya kupata shahda hiyo Weah alisema “nimetimiza ndoto yangu nami kwa sasa ni miongoni mwa wasomi wa kweli.”

Hata hivyo, Weah alsisitiza kwamba hakurudi kusoma kwa ajili ya kuusaka urais, bali kuonyesha kuwa, hakushindwa kusoma kwa sababu ya kutokuwa na ‘kitu’ kichwani.

Alisema: “Wote tunakuwa na ndoto za kusoma mpaka Chuo Kikuu. Baadhi wanaweza, wengine waliikosa kabisa hiyo nafasi na wengine walisubiri hadi wakati mwafaka.”

Katika uchaguzi wa 2011 aligombea kama mgombea mwenza wa Winston Tubman aliyechuana na Bi Sirleaf ambaye alishinda kipindi chake cha pili. Mwaka 2014 Weah aligombea na kuukwaa Useneta kupitia chama cha Coalition for Democratic Change (CDC).

UTAJIRI WAKE

Baada ya kutangazwa kwamba Weah atagombea urais kupitia chama CDC kuliibuka madai kwamba mchezaji soka huyo wa zamani alikuwa amefilisika, hali ambayo ingemuondolea sifa ya kugombea.

Hata hivyo baada ya utafiti wa kina, jarida moja la “Investigation” nchini humo lilisema huo ulikuwa uzushi tu kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa.

Likinukuu majarida mbali mbali kuhusu utajiri wa watu mashuhuri duniani, jarida la “Investighation” lilitaja kwamba Weah alikuwa ni wapili miongoni mwa watu mashuhuri (celebrities) Barani Afrika baada ya mchezaji wa soka wa zamani wa Cameroon Samuel Eto.

Jarida hilo lilitaja kwamba Weah alikuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani 85 milioni wakati Samuel Eto Dola 90 milioni. Orodha hii ya watu wa mashuhuri Barani Afrika inajumuisha wacheza soka na wanamuziki.

Aidha mtandao wa Thecelebritynetworth.com pia umetaja kwamba utajiri wa George Weah unafikia Dola za Kimarekani 85 milioni.

Inasadikiwa kwamba uwekezaji wa George Weah umejikita zaidi katika makampuni ya utalii, hususan hoteli za kitalii Barani Afrika nchini mwake Liberia, Afrika ya Kusini na Mauritius.

Aidha miaka 15 iliyopita baada ya ujio wake hapa Tanzania, Weah aliwekeza katika kiwanda kimoja cha maji ya chupa kule Zanzibar – “Drop of Zanzibar”.