Home Habari NFRA YADAI HAKUNA NJAA NCHINI

NFRA YADAI HAKUNA NJAA NCHINI

1479
0
SHARE

*Yadai chakula kipo cha kutosha


FARAJA MASINDE NA RENATHA KIPAKA,BUKOBA

WAKATI kukiwa na tishio la wazi la njaa nchini, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), imedai kuwa hakuna njaa.

Kauli hiyo ya NFRA inapingana na taarifa mbalimbali zinazotoka kwa baadhi ya wanasiasa, viongozi wa wilaya na mikoa pamoja na wananchi wa kawaida wanaoeleza kuwa hali ya chakula nchini hairidhishi.

Katika mahojiano maalumu na RAI yaliyofanyika  juzi jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu  wa NFRA, Joseph Ogonga, amesema mpaka sasa hakuna baa la njaa linaloikabili nchi kama ambavyo imekuwa ikielezwa na  makundi mbalimbali ya watu.

Ogonga alisema anachokiona yeye si ukosefu wa chakula, badala yake ni wananchi wengi kukosa uwezo wa kumudu kununua chakula.

Alisema ni kweli chakula kimepanda bei, lakini kwa mtu anayefanya kazi hilo haiwezi kumuathiri, badala yake hali inakuwa mbaya kwa watu wenye uwezo mdogo wa kununua chakula.

“Hali kama hiyo imekuwa ikitokea hata kwenye mabasi, mafuta yakikosekana kidogo tu watu wanashindwa kulipa hata nauli, hata kwenye daladala wakipandisha Sh 100-200 watu wanaanza kutembea kwa miguu, kwa sababu uwezo wa watu wengi ni mdogo.

“Bahati mbaya kunapotokea kuyumba kidogo watu wanasema kuna njaa, lakini actual haijafikia hatua ya kwamba chakula hakipo kabisa, na hii hali inaweza ika change ikifika Machi, mvua hizi zinazonyesha sasa zitabadili hali kabisa,”alisema.

Alisema kwa sasa ni mapema mno  kusema  kuwa nchi ina njaa, kwa sababu amepewa taarifa kuwa yupo mfanyabiashara ametoa tani 20,000 kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

“Kuna vyakula ambavyo watu wamekaa navyo, hatujafikia hatua ya kusema kuna njaa, tunapotoa taarifa za namna hii tuwe na uhakika na hata bei haijapanda sana kama ilivyo kwenye nchi za Sudani Kusini na maeneo mengine,”alisema.

Alisema kama hali hiyo ingekuwepo basi kiongozi wa nchi angeshatangaza maana yeye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, alikiri mabadiliko ya hali ya hewa kuwaathiri wakulima wengi, lakini hali hiyo haitoshi kusema kwa sasa nchi imekumbwa na baa la njaa.

“Mpaka sasa hatuwezi kusema nchi imekumbwa na baa la njaa ni mapema mno kulisemea hilo, hali inaweza kuwa hivyo inavyoelezwa sasa Mwezi Machi mwaka huu na tutafikia hapo kama mvua zitaendelea kukosekana katika maeneo mengi ya nchi, lakini pia hata kama kutakuwa na njaa Rais peke yake (Dk. John Magufuli) ndiye mwenye kutoa taarifa kuwa nchi imekumbwa na baa la njaa.

“Unajua ili kufikia hatua ya kutangaza majanga huwa kuna viwango vyake, suala la majanga ya kitaifa huwa yanatangazwa na Rais na inamlolongo wake si jambo rahisi.

“Kwa sasa bado haijafika hatua ya kutangaza kuwa njaa ni janga la kitaifa.”

Alisema kwa sasa chakula kipo cha kutosha kwa sababu hata ukienda sokoni kinapatikana.

Akitolea ufafanuzi kauli zinazotolewa kuwa kuna upungufu wa chakula cha akiba, Ogonga alisema hakuna ukweli wowote juu ya hilo na kwamba chakula kilichopo kinauwezo wa kulisha nchi katika hali ya dharura.

Hata hivyo, alisema jukumu la maghala ya Taifa si kugawa chakula badala yake ni kukihifadhi na uamuzi wa kukigawa uko mikononi mwa Kamati maalumu.

“Mradi huu ulianzishwa ili kusaidia kwa haraka pale panapotokea janga na hali ya chakula ikawa mbaya hapo ndipo kitatumika hiki,

“Mpaka sasa sijawaona wasagishaji wakubwa wanaosambaza unga kama akina Said Bakhresa, Mohamed Dewji na wengine wakija hapa kutaka  mahindi.

“Ninachokiona ni wanasiasa kuwapa nafasi wafanyabiashara wauze bidhaa zao walizozihifadhi kwa bei wanayotaka wao ili watengeneze pesa nyingi,” alisema Ogonga.

“Huenda wafanyabiashara wakubwa kuna kitu  wanafanya kama ilivyofanyika kwenye sukari,  kwa sababu huwezi kuwalazimisha wauze mazao yao, kama chakula kisingekuwapo hali ingekuwa mbaya zaidi ya sasa, maana wafanyabiashara wakubwa wangelalamika kupita kiasi, kikubwa ni kuwapo kwa chombo maalumu kitakachosimamia bei za mazao, kwa sasa imekuwa ni kama yatima hivyo serikali ianzishe haraka,” alisema Ogongo.

Alisisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hayo mwaka 2008 hawajawahi kugawa chakula kwa mtu mmoja mmoja,”

“Hatugawi chakula kiholela, ndio maana unaweza kukuta kuna njaa Songea na sisi tuna mahindi pale, lakini tunashindwa kuwasaidia, kuna utaratibu wa kufikia hatua hiyo,”alisema.

Alisema ili kuondoa uwezekano wa baadhi ya wanasiasa kutumika kisiasa katika masuala haya ya chakula, ipo haja ya eneo hili kuanzishiwa mamlaka ya udhibiti.

“Mwarobaini wa kulikwepa hili ni kuhakikisha  kunaundwa chombo maalumu cha kudhibiti bei za mazao kama inavyofanywa EWURA na SUMATRA jambo ambalo litasaidia kuwapo kwa bei za uhakika, lakini pia itawasaidia wakulima kujua taarifa za soko la bidhaa mazao yao,” alisema.

Alisema suala la kuwapo kwa njaa limekuwa likichanganywa na siasa hali inayowaaminisha wananchi kuwa ni kweli kuna njaa.

Hata hivyo, Ogonga alikiri kuwapo kwa tani 90,000 tu za chakula kwenye maghala yao, ambazo haijawahi kutokea zikategemewa na Watanzania wote.

“Tutoke huko kwenye kufikiria kila Mtanzania kutegemea hizo tani 90,000, haiwezekani na sijui ni kwanini wanasema hivyo, mahindi yetu sidhani kama yalishawahi kutoka Dar es Salaam, yakafika Kigoma tangu dunia iumbwe, hayajawai kufika.

“Kigoma imekuwa ikijitosheleza miaka yote, wala haijawahi kupewa msaada na hata yakipungua hawawezi kupelekewa mahindi huko kwa sababu wao wanayatoa ng’ambo ya pili, haijawahi kutoa mahindi Dar es Salaam, yakarudi kule.”

“Tuache siasa kwenye mambo ya msingi kama haya, nchi haijawahi kuwa na chakula cha kugawa kila mahali bure,”alisema.

Akitoa ufafanuzi wa kwanini NFRA inazo tano 90,000 tu za chakula, Ogonga alisema kimekuwa kikipungua kutokana na kukigawa kwa Magereza, lakini pia wamekuwa hawana uwezo wa kununua chakula mara kwa mara kutokana na kukosa fedha za uhakika.

Alisema kuchelewa kununua mazao kumekuwa kilio chao tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2008  na kwamba mara nyingi kwenye kipindi cha mavuno ambacho bei ya mazao inakuwa chini, serikali inakuwa haijatoa pesa kwa ajili ya kununua chakula jambo ambalo halijafanyika na mpaka sasa.

Akieleza namna ya chakula kinavyoweza kugaiwa, alisema ni lazima kamati maalumu ikae kwa ajili ya kuangalia namna ya kutoa chakula kilichopo na kwamba wao kama NFRA mamlaka yao yanaishia kwenye kukitunza.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa kama nchi itaendelea kukumbwa na changamoto ya kukosekana kwa mvua hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu upo uwezekano mkubwa kwa mikoa  ya Tanga, Kagera, Mwanza, Geita, Pwani, Shinyanga, Kilimanjaro, Kigoma na Arusha kukumbwa na njaa.

Ogonga alitoa ushauri kwa serikali kuiangalia upya sekta ya kilimo kwa kuwa na utayari wa kutoa nafasi kwa watu kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa mazao kwa mwaka mzima.

“Kuna haja ya serikali kuhakikisha kuwa inaboresha eneo hili la kilimo, tunapaswa kuwa na kilimo cha uhakika, kwa mazingira ya sasa itakuwa ngumu kufikia mkakati wa uchumi wa kati,” alisema.

Vijana walazimishwa kulima

Wakati NRFA ikieleza kuwa hakuna njaa, mambo mkoani Kagera ni tofauti, tayari Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Luteni Kanali Denis Mwila amejipanga kutekeleza mkakati wa kuwabana vijana wanaoshinda vijiweni ili waende  mashambani ili wakajishughulishe na kilimo ambacho kitasaidia kuiepusha wilaya yake na njaa.

Katika mazungumzo yake na RAI, Luteni Kanali Mwila alisema anajipanga kwa ajili ya kufanya kikao cha pamoja na wanasiasa ili kuzungumzia uamuzi wake huo.

“Tutakaa kikao ambacho kitawajumisha wanasiasa na viongozi wa serikali kwa lengo la kuwadhibiti vijana ambao ndio nguvu kazi ya wilaya, wote wakalime hata mazao ya muda mfupi, ingawa mvua zimenyesha chini ya kiwango kinachotakiwa”alisema.

Alisema mvua ilitakiwa kunyesha kwa kiwango cha milimita 400.8 badala yake ilinyesha kwa kiwango cha chini sana ambayo ilikuwa ni milimita 93.8 hivyo kutokana na upungufu huo wakulima waliokuwa wamelima mazao hayakustawi kama ilivyotakiwa.

Alisema kutokana na hali hiyo zipo kata 13 zimeathirika huku kata nne za Kakunyu, Mtukula, Mabale, Kilimilile, zikiwa zimeathiriwa zaidi, na kwamba  vijiji 27 na kaya 4614 nazo zimeathiriwa na ukame.

“Kuna upungufu wa chakula kwa asilimia 49, tumefanya  jitihada a kuomba chakula kwenye ofisi ya Waziri Mkuu na kufanikiwa kupewa tani 100 ambazo kati ya hizo tani 10 tuligawa bure na tani 90 wananchi waliuziwa kilo moja kwa sh 50.

“Nimepiga marufuku uchomaji wa mahidi mabichi na usafirishaji wa mahindi kutoka nje ya wilaya ya Missenyi, kila mtu anatakiwa kupanda mazao yanayoweza kuhimili ukame,kama vile Mihogo, viazi vitamu, pamoja na magimbi” alisema Mwila

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyerwa, Shedrack Muhagama, alisema  hali ya chakula katika mwezi wa nane na wa tisa ilikuwa mbaya tofauti na sasa ambapo mvua zinanyesha japo ni katika kiwango cha chini.

“Japo hali ya mvua si nzuri lakini wananchi wamepanda mahindi na kuondoa dhana ya kutengemea migomba kama chakula chao kikuu na sasa nimeagiza viongozi kuanzia ngazi ya kata na wenyeviti wa vitongoji kuwahimiza wananchi kutunza chakula kwa wingi ili kuepukana na njaa ambayo inaweza kujitokeza” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karagwe, Godwin Kitonka, alisema uwa Kata ambazo zimepata mvua yakutosha na ukuaji wa mazao shambani ni mazuri ni kata za Ihembe, Nyakasimbi, Rugu,Kituntu, Bwela nyange.

Kitonka alieleza kuwa Kata mbazo zina mvua ya wastani na ukuaji wa mazao ni wa wastani ni Bugene, Kayanga, Chonyonyo, Rugera, Igurwa, Kanoni, Kamagambo, Nyakahanga, Ndama, Ihanda, Kiruruma.

Aliendelea kufafanua kuwa katika Halmashauri hiyo kuna Kata ambazo hazikuwahi kupata mvua kabisa ambazo uwezekano wa kuvuna mazao ni mdogo au haupo kabisa, Omurutoma kijiji pamoja na Kata za Chanika, Nyaishozi, Nyabiyonza.

“Serikali ilileta chakula tani 100 za mahindi ambapo tulizigawa tani 90 bure na tani 10 tuliziuza kilo moja kwa sh 50, kwa awamu ya pili zililetwa tani 100 ambazo tulizigawa bule kwa Kata zote 23” alisema Kitonka

Pia waziri wa kilimo na umwagiliaji Charles Tizeba, alitoa tani 10 za chakula ambazo ziligawa bule katika Kata tatu ambayo ni kihanga, na Nyakakika ambazo ni jitihada za serikali kuwasaidia wananchi.

Biharamulo imetajwa kuwa na chakula cha kutosha kutokana na Halmashauri hiyo kupata mvua za kati ambazo zimesababisha wakulima kulima na kuvuna tofauti na sehemu zingine za mkoa huo.

Akizungumza na RAI Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Wende Ng’ahala, hata hivyo amewahimiza wananchi kulima zalo la mtama kwa kuwa linakomaa mapema na kuhimili ukame.

Hali ya chakula katika Halmashauri ya Ngara ni ya wastani kutokana na kutegemea kilimo cha mabondeni ambako maji hudumu kwa muda mrefu tofauti na maeneo ya kawaida.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Ngara, Aidan Bahama,  alizitaja kata zilizopata mvua kuwa ni Kasulo, Bukililo wakati Kata za Nyakisasa, Mulusagamba mvua hazikunyesha kabisa hivyo hata upatikanaji wa mazao ya chakula sio mzuri.

Kauli ya NRFA inapingana na idadi kubwa ya watu wa kada mbalimbali waliozungumza na RAI kwenye kijarida cha Hoja ya wiki kilichomo ndani ya gazeti hili.

RAI lilimtafuta Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, ili kuzungumzia suala hili la kuwapo ama kutokuwapo kwa chakula nchini, ambapo alisema hawezi kulizungumzia kwa sababu yuko kwenye kikao.