Home Makala HAKUNA POROJO ‘LAINI’ MOJA MITANDAO YOTE

HAKUNA POROJO ‘LAINI’ MOJA MITANDAO YOTE

775
0
SHARE

Na JOHANES RESPICHIUS


NI dhahiri kwamba tangu Tanganyika ipate uhuru mwaka 1961, na baadae kuitwa Tanzania baada ya kuungana na Zanzibar, sekta ya mawasiliano inakua kwa kasi na sasa imehama kutoka mfumo wa analojia na kuingia dijitali.

Mfumo wa dijitali umekuwa chachu kubwa katika ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano ambapo imeshuhudiwa mabadiliko mbalimbali katika mifumo ya kimawasiliano, hususan simu za mikononi.

Kwa sasa unaweza kufanya shughuli ambayo ingekugharimu muda mwingi, hivyo kuifanya kwa muda mfupi. Mfano kupitia simu ya kiganjani unaweza kufanya miamala benki, kufanya manunuzi kwenye maduka ukiwa nyumbani.

Ili kuboresha huduma kwa watumiaji wa mitandao, Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) inakuja na huduma ya kuhamia mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani (MNP).

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Jamesi Kilaba, anasema maendeleo ya sekta ya mawasiliano kuanzia mwaka 2005 watumiaji wa laini za simu za kiganjani walikuwa milioni 2.963, idadi iliyoongezeka hadi kufikia milioni 40.173 Desemba, mwaka jana.

Anasema kutokana na ongezeko hilo la watumiaji wa huduma za mawasiliano, TCRA kwa kushirikiana na wadau hawana budi kusimamia kwa makini, sera, sheria na kanuni ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, hivyo mitandao ambayo haitafanya ubunifu itakosa wateja.
Mhandisi Kilaba anasema huduma hiyo imeanza kutumika rasmi Machi mosi, mwaka huu kwa wateja wote nchini wanaolipia huduma kwanza na baada ya matumizi na simu ya mtumiaji lazima iwe haijafungiwa, kusimamishwa wala kutokulipa malipo ya ankara.
Historia ya MNP
Anasema mradi wa MNP upo kwa mujibu wa kanuni ya ‘Electronic and Postal Communications (Mobile Number Portability) Regulations’ za mwaka 2011.
“Uanzishwaji wa huduma hii ni kwa mujibu ya kanuni za mwaka 2011 yenye lengo la kumpa mtumiaji uhuru wa kuchagua mtandao unaotoa huduma bora zaidi, huduma nzuri kwa wateja na ubunifu.

“Tanzania tunaungana na nchi nyingine Afrika ambazo tayari imeanzishwa kama vile Misri, Kenya, Sudan, Afrika Kusini, Nigeria, Senegal na Morocco pamoja na Rwanda na Namibia ambazo zipo kwenye mchakato wa kuanzisha,” anasema Mhandisi Kilaba.

Jinsi ya kuhama
Anasema mtumiaji wa mtandao husika anapaswa kwenda kwa wakala anayetambuliwa na watoa huduma anakotaka kuhamia na kumweleza kwamba anataka kuhama na namba yake ambapo atatakiwa kuwa na kitambulisho chenye picha yake pamoja na simu yenye namba anayotaka kubaki nayo.

“Iwapo kama utakuwa na salio katika akaunti unashauriwa kulitoa kabla ya kuhama ili kuepuka usumbufu au utatakiwa kutuma meseji yenye neno ‘HAMA’ kwenda 15080 ambayo ni namba maalumu ya kuhama na baadaye utapokea ujumbe wa kukujulisha kwamba maombi yako yamepokelewa,” anasema Mhandisi Kilaba.

Anasema katika hatua zote za kuhama mtandao na namba yako hakuna gharama, isipokuwa kabla ya kuhama itabidi kununua laini mpya ya simu ya kiganjani unakotaka kuhamia.

Anasema vitu ambavyo ni muhimu kuvitoa kwa wakala pindi unapotaka kuhama ni pamoja na kitambulisho chenye picha ambapo kinaweza kuwa cha Taifa, kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva au pasipoti.

Faida za huduma ya MNP
Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Mawasiliano, Mwesigwa Felisian, anasema kuwa mtu aliyehama hataweza kuhamia mtandao mwingine tena kabla ya kutimiza mwezi mmoja, yaani siku 30, kama ni mteja mpya itakuchukua siku 60 ili kuweza kuhama,” alisema Mhandisi Kilaba.

Anasema huduma hiyo itamwezesha mteja kubaki na namba yake bila kujali anatumia mtandao gani na mteja ataweza kupokea simu na ujumbe wa maneno bila kujali ni mtandao upi amehamia na hakuna haja ya kuwataarifu watu wengine kwamba umebadilisha mtandao.

“Pia itaongeza ushindani kwenye sekta ya mawasiliano na kuwa kichocheo cha utoaji huduma bora, maana kama huduma haziridhishi, basi wateja watahama na namba zao.

Anasema mteja ataendelea kutumia namba yake ya awali anapohama kutoka mtoa huduma mmoja kwenda mwingine, hivyo kufurahia uhuru wa mtandao mpya uliohamia.

“Atapokea simu na ujumbe mfupi bila kujali ni mtandao upi aliohamia na bila kuwa na haja ya kuwaarifu ndugu na jamaa kwamba amebadilisha mtandao.

“Pia itapunguza gharama za kununua laini mpya kwa kila mtoa huduma au simu ya kiganjani zaidi ya moja na ataweza kuchagua mtoa huduma ambaye anaona anatoa huduma bora zaidi, anakidhi matarajio yake ikiwa ni pamoja na ubunifu,” anasema Mhandisi Felisian.

Alisema katika utekelezaji wa huduma hiyo, TCRA iliwashirikisha watoa huduma za kibenki ili wafunge mifumo itakayotambua namba zilizohama, hivyo kuwawezesha kutuma fedha mitandaoni bila shida yoyote, kwamba mteja aliyehama mtandao atatakiwa kufika katika tawi lake la benki ili kuhakiki mtandao aliohamia umeunganishwa na benki anayoitumia.

Mambo muhimu baada ya kuhama
Anasema meseji ambazo zitakuwa zimetumwa na hazijaingia kwenye simu yako zinaweza kupotea kwa kipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa kuhamishwa kwenda mtandao mwingine.

“Meseji za sauti ‘voicemails’ za zamani ulizokuwa umepata na kuzihifadhi kwenye laini ya simu na namba za simu za watu itabidi zihamishiwe kwenye ‘memory card’ ili zisipotee utakapoweka laini mpya ya mtandao unaohamia.

Aidha, itabidi ufanye utaratibu na mtoa huduma wako kuhusu huduma nyingine ulizokuwa unazipata moja kwa moja kutoka kwa mtoa huduma wa awali kama ni za kubenki (mobile banking),” anasema.

Anasema mtu hataruhusiwa kuhamia kwa mtoa huduma wa tatu au kurejea kwa mtoa huduma wa awali ndani ya siku 30 baada ya uhamaji wa kwanza.

“Iwapo unampigia simu mtu ambaye unadhania yuko mtandao mmoja na wewe wakati tayari kashahama, utasikia mlio unapoanza kupiga simu hiyo kukutahadharisha kwamba gharama za simu unayoipigia zinaweza kuwa juu zaidi.

“Mfano, kama uko kwenye mtandao wa Vodacom na unapiga namba ya Voda ambayo imehamia Tigo au Airtel au mwingine utasikia mlio unapoanza kupiga simu hiyo,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Kampuni ya Airtel, Jackson Mbando, anasema wameipokea vizuri huduma hiyo, hivyo kazi yao ni kuboresha na kutoa huduma nzuri ili kukabiliana na ushindani sokoni.

“Hii ni huduma ambayo inampa nafasi mteja kutumia kile anachokihitaji na siyo kitu ambacho mtoa huduma anayetoa huduma nzuri na zenye ubunifu anaweza kuchukia.

“Mpango wa Airtel ni kuendelea kutoa huduma nzuri zenye ufanisi kwa wateja wetu wapya na wa zamani pia, ili mtu kuhama kuna hatua anazozifuata, hicho ndicho kitatufanya tuendelee kuhudumia wateja wetu,” anasema Mbando.
Watumiaji wanasemaje

RAI limezungumza na watumiaji mbalimbali wa simu za kiganjani ambapo wanasema huduma hiyo itawaondolea usumbufu uliokuwapo kwa mtu anayetaka kuhama kulazimika kuachana na namba ya awali na kutumia namba mpya ya mtandao anaohamia.

Emmanuel Mosha ni mteja wa mtandao wa Tigo, anasema huduma hiyo ameisikia, licha ya kwamba alikuwa hajapewa elimu ya kutosha ili kuielewa vizuri, lakini kwa kadiri alivyosikia inaongelewa itakuwa nzuri.

“Kuhama bila kubadili namba kutatusaidia sisi watumiaji wa simu za mkononi kuhama kwa mtoa huduma ambaye huduma zake si nzuri kwa urahisi zaidi, pia itaongeza chachu kwa mtoa huduma wake kuboresha huduma zake ili watu wahamie kwake,” anasema Mosha.