Home Uncategorized HALMASHAURI NYINGI NCHINI ZIMEJAA UFISADI

HALMASHAURI NYINGI NCHINI ZIMEJAA UFISADI

878
0
SHARE

soko la mwanjelwa

NA HILAL K SUED

AKIWA ziarani Mkoa wa Mbeya wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwatia mbaroni watendaji na maofisa 12 wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kutokana na ufisadi katika ujenzi wa soko jipya la Mwanjelwa, jijini humo.

Watu hao ni pamoja na aliyekuwa Meya wa jiji hilo, Atanas Kapunga, wakurugenzi watatu, kaimu mkurugenzi, wahasibu wawili na wanabodi wanne. Hawa wanatuhumiwa kusababisha hasara ya Sh bilioni 63.

Wakati nikimpongeza Waziri Mkuu kwa hatua hizo na ambazo hata hivyo zilichelewa sana, ningemwomba afanye hivyo kwa halmashauri nyingine nchini ambazo nyingi kwa muda mrefu zimekuwa zikituhumiwa kwa ufisadi na ufujaji mkubwa wa fedha.

 

Kwa ujumla hatutakosea tukisema kwamba taasisi hizi ni mashimo yasiyokuwa na kina (bottomless pits). Fedha zinazokusanywa au zile zinazopewa na Serikali kuu huenda chini, bila kuonekana. Bila kuonekana kwa namna ya maendeleo ya wananchi – kuboresha hali zao za maisha na miundombinu katika sehemu zao.

 

Aidha, hatutakosea tukisema kwamba uchafu wote uliyomo ndani ya halmashauri zetu unatokana na upigaji kura. Kwa bahati mbaya katika nchi yetu kura inaliangamiza taifa kwa sababu huingiza watu katika uongozi ambao sifa zao kubwa ni fedha walizonazo kuwanunua wapiga kura.

 

Kabla sijaendelea zaidi tukubaliane kitu kimoja, kwamba habari kubwa zinazokataa kutoweka hapa nchini ni za ufisadi ndani ya utawala na taasisi za umma na hasa hasa ndani ya halmashauri zetu za wilaya na miji. Ripoti chanya za kila mwaka za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni ushahidi tosha wa yanayotendeka. Aidha, habari hizi kamwe hazijapata kukosa walalamikaji kutoka pande zote mbili za medani ya siasa, utawala na upinzani.

 

Ajabu ya yote ni kwamba, viongozi wa juu wa nchi akiwamo Rais John Magufuli na wasaidizi wake wakuu, nao wamekuwa wakililalamikia tatizo hili hili badala ya wao kuchukua hatua madhubuti za angalau kulipunguza tatizo. Hatua kama hizi alizozitangaza Waziri Mkuu kule Mbeya.

 

Ufisadi ndani ya taasisi hizo ambazo ndiyo wadau na wasimamizi wakubwa katika kuleta maendeleo katika sehemu za vijijini, kwa kiasi kikubwa umesababisha sehemu hizo kuachwa nyuma kimaendeleo na athari zake sasa ni dhahiri.

 

Mfano mmoja wa athari hizi ni kilio kilichofuatiwa ghasia za wananchi wa Mtwara miaka kadhaa iliyopita, kutokana na kubakia nyuma kimaendeleo kwa miongo kadhaa,  hasa baada ya kuhisi kwamba rasilimali kubwa ya gesi asilia iliyotangazwa kupatikana katika maeneo yao nayo imeamuliwa ichukuliwe na kupelekwa mikoa mingine.

 

Hakuna haja kutaja hapa jinsi vyama vya ushirika vikishirikiana na bodi za mazao na halmashauri zilivyokuwa zinawakamua wakulima wa korosho mapato yao ya halali miaka nenda rudi.

 

Halmashauri zetu zimekuwa kama shamba la bibi kwa jinsi watendaji wanavyojichotea fedha za umma, kwa kubuni miradi mbali mbali mingi ikiwa feki. Zile halmashauri za mikoani ndizo hasa ambazo hakuna kitu cha maana kinachofanyika, kwani ziko mbali, hivyo hazitupiwi macho vizuri na Serikali kuu ambayo yenyewe pia imezama katika uovu huo huo. Uchafu katika halmashauri umeigwa kutoka kwa ‘baba’ yao yaani Serikali kuu. Suala ni nani hapa mwenye ushawishi wa kimaadili kuweza kukemea wengine.

 

Miezi michache baada ya kuingia madarakani mwaka 2006, wakati bado anao ule moto wa ‘Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya’, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alizishukia halmashauri nchini kwa matumizi mabaya wa fedha za walipa kodi.

 

Katika mkutano wake na madiwani na watendaji wakuu wa halmashauri uiliofanyika Iringa, alitishia kuzisimamisha halmashauri zozote zitakazoshindwa kudhibiti hesabu yao na aliwapa muda wa miezi sita kujirekebisha.

 

Kikwete pia aliagiza ikome ile tabia ya baadhi ya vikao vya madiwani kugeuzwa mahakama za kuwajadili na kuwahukumu watafunaji wa fedha za umma, kwani kazi hiyo ni ya mahakama.

Lakini hadi anaondoka madarakani hakuisimamisha halmashauri yoyote ile na ufisadi uliendelea, tena kwa kiwango cha kutisha kama tulivyokuwa tukisoma katika vyombo vya habari kila siku. Ukimya huu ulipelekea wananchi wa wilaya zilizozama katika ufisadi kuiomba serikali iivunje halmashauri zao – potelea mbali.

 

Hili lilitokea mwishoni mwa mwaka 2014 katika Halmashauri ya Misungwi, mkoani Mwanza, ambapo katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wananchi walimwomba aivunje halmashauri hiyo kwa ufisadi.

 

Hali kama hiyo pia ilijitokeza katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, ambapo madiwani takribani wa vyama vyote (pamoja na wa CCM), walimtaka Meya ang’olewe kutokana na kukumbatia kwake miradi ya kifisadi. Wito huu waliutoa kwa Rais Kikwete katika ziara yake, lakini alionekana kushindwa hata kutimiza kusudio lake la mwaka 2006 la kuisimamisha halmashauri fisadi, angalau kwa lengo la kuisuka upya.

 

Na kama ufisadi na uongozi mbovu katika halmashauri ndiyo kipimo cha kuzisimamisha, basi angepaswa kuanza na zile karibu yake – halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Ni wachache wanaoweza kusema kwamba halmshauri tatu (sasa nne) za mkoa huu pamoja na mwamvuli wao Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,  zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, bila ya ufisadi na mazingira ya makazi pamoja na miundombinu iko katika kiwango stahiki.

 

Sasa hivi kwa mfano kuna malalamiko kwamba, utawala wa Rais Magufuli umepora vyanzo vya mapato vya halmashauri hasa kodi ya majengo. Kwani Jiji la Dar es Salaam ndilo lenye majengo mengi na hivyo ilikuwa inapata mapato mengi kutokana na kodi hiyo.

 

Aidha, upinzani ambao ndio unaongoza halmashauri ya jiji pamoja na ile ya Ilala na Ubungo, imekuwa inalalamika kwamba Serikali inaibania mipango yake ya maendeleo ili ionekane kwa wananchi kwamba upinzani umeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi.