Home Habari Hamad Rashid Mohamed alia kutengwa na wapinzani

Hamad Rashid Mohamed alia kutengwa na wapinzani

1399
0
SHARE

GABRIEL MUSHI

Mwenyekiti wa Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC), Hamadi Rashid Mohammed amesema anashangaa kwanini vile vyma sita vya upinzani vilivyokuja Zanzibar wiki mbili zilizopita kujadili, pamoja na mambo mengine, muswada mpya wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa havikukishirikisha chama chake kwa kutokipa mauliko.

Katika mahojiano maalum na RAI, mwanasiasa huyo mkongwe wa Zanzibar alisema hii ni tofauti na vikao vingine vya mijadala ya kisiasa vilivyoandaliwa na wanasheria ambavyo walialikwa na kushiriki.

Kauli hiyo ilitokana na swali aliloulizwa kwanini ADC inaonekana kujitenga na wengine katika upinzani, hata katika baadhi ya mambo kuonesha msimamo, kwa kutaja mfano muswada huo wa marekeboisho ya sheria ya vyama vya siasa.

Katika maamuzi mengine Hamad Rashid alisema uamuzi wa Rais John Magufuli kupiga marufuku mikutano na harakati za kisiasa nchini umefanana na ule alioutoa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume.

Hamadi Rashid ambaye pia ni Waziri wa Afya katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alisema baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Mzee Karume alipiga marufuku uwapo wa vyama vya siasa Visiwani humo na kuagiza uchaguzi utafanyika baada ya miaka 60.

“Kwa mfano Mzee Karume wakati anaingia kwenye serikali baada ya mapinduzi alipiga marukufu vyama vya siasa akasema uchaguzi utakuwa baada ya miaka 60, kikabakia chama cha Afro Shiraz peke yake. Ukitazama kipindi chake kuanzia mwaka 1964 mpaka 1972  maendeleo aliyofanya ni makubwa huwezi kulinganisha na sasa,” alisema Hamadi katika mahojiano yake na RAI wiki hii.

Katika mahojiano hayo Hamadi Rashidi pia alitolea mfano wa nchi ya Singapore ambapo kiongozi wake Lee Kuan Yew pia alipiga marufuku harakati za kisiasa ambazo sasa zimeifanya nchi hiyo kuwa na maendeleo yasiyo kifani.

Hata hivyo, Hamadi ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Wawi (CUF) alisema ili Rais Magufuli afanikiwe lazima akae meza moja na wanasiasa wote na kufanya mazungumzo yenye tija kuhusu namna sahihi ya kufanya siasa katika kipindi hiki.

“Tatizo ni kwamba uelewa wa watu wetu ni mdogo sana. Asikudanganye mtu, wakati unataka kufanya jambo lazima uondoshe mambo ya vurugu.

“Lakini ili ufanye hivyo vizuri lazima uelewane na wenzako nafikiri ni jambo la msingi sasa Rais Magufuli apate muda wa kukaa na viongozi wa kisiasa. Ili kuhakikisha nchi inabaki katika amani na utulivu,” alisema.

Kauli hiyo ya Hamadi pia inaendana na baadhi ya kauli za wasomi na wanasiasa mbalimbali ambao pia wamekuwa wakimfananisha Rais Magufuli na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kutokana na kuiga falsafa ya ujamaa na kujitegemea katika uongozi wake.

Pamoja na mambo mengine Hamadi alisema Serikali yoyote lazima iheshimu Katiba, sheria na kanuni.

“Jambo la msingi lazima nchi ibaki kwenye amani, mnaweza mkatumia katiba na sheria hizohizo lakini nchi isibaki kwenye amani, ndio maana kukawa na mtu anaitwa ‘Commander in Chief’(Amirijeshi Mkuu). Kwa mfano kama tunafanya maandamano kuunga mkono serikali ifanye kazi zake vizuri.. hilo sawa, ila kama kutwa kuchwa ni kugombana hilo sikubaliani nalo.

“Ni kweli hali tuliyokuwa nayo kwa Rais Kikwete na sasa ni tofauti maana Magufuli kwa mtazamo wake anataka rais apate muda wa kutosha kufanya mambo ya maendeleo, tusimrudishe nyuma katika hilo,” alisema. 

Endelea kusoma mahojiano hayo zaidi…

RAI: Licha ya kuwa na sifa za mwanasiasa machachari, tangu uongozi wa serikali mbili uingie madarakani 2015, umekuwa kimya sana, nini kimekusibu?

HAMADI: Kila kiongozi inategemea yupo katika nafasi ipi ya kisiasa, kwa mfano kipindi cha nyuma nilikuwa bungeni… ni tofauti unapokuwa waziri serikalini. Kwa hiyo mazingira ya kufanya kazi kipindi cha nyuma ni tofauti na sasa. Lakini pia mwanasiasa makini huangalia mazingira ya kisiasa ya wakati huo. Kila kiongozi husoma upepo ukoje na lengo lake ni nini. Kila mtu ana njia zake. Cha msingi ni kuzingatia sheria na taratibu hivyo kiongozi mzuri ni yule aliyetulia na kusoma alama za nyakati.

Kipindi cha Kikwete ni tofauti kabisa na sasa, hata wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na aina yake ya kuifanya kazi za kisiasa.

Katika kufanya siasa kwenye zama hizi, chama chetu ADC tumejifunza mengi, ila kubwa kwanza tunaamini uwepo wa  Mwenyezi Mungu, pili tunaamini katika haki, tunaamini kudai haki kwa njia za amani na salama.

RAI: ADC mnaonekana kujitenga na wenzenu wapinzani, hata katika baadhi ya mambo hamshiriki kuonesha msimamo, tatizo ni nini?

HAMADI: Kwa mfano muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa. Vyama vyote vinakorofishana bila kuangalia mapungufu yaliyopo kuwa je, lengo kubwa ni kuimarisha demokrasia au ni kuibomoa.

Wapo wanaoona kuna upungufu wa uhuru wa kuamiani anachotaka, tunachotaka sisi ADC sio kupiga kelele tu, ndio maana tumeshauri serikali ikae na vyama vya siasa tujenge misingi imara ya majadiliano. Hili ni jambo ambalo tunaamini ndio ushawishi mzuri.

Msingi wa pili wa ADC ni kuhakikisha nchi inabaki salama na amani, hatukubali kuingia kwenye vurugu za aina yoyote, tunaamini kutumia njia ya mazungumzo, kwa mfano wakati muswada huu unaanza mchakato wake tulishirikishwa na maoni yangu nilitoa lakini labda hayakuingizwa ila bado ninayo haki yangu kichama na nitakwenda kutumia… ndio maana hata Shibuda amesema tutumie busara katika mazingira ya siasa za sasa.

Ukiangalia vile vyama sita vilivyokuja Zanzibar kwa majadiliano, havikutushirikisha chochote, hatukualikwa. Ukiangalia vikao vingine vya mijadala ya kisiasa hata vilivyoandaliwa na wanasheria tumekwenda hata Dodoma tumekwenda. Tatizo ni namna ya kulizungumzia hilo suala husika. Mtoto nyumbani unaweza kumuonya ‘wewe usinywe maji hayo’ ila mwingine akamwambia ‘babaa usinywe hayo maji yaache’. Jambo lilelile lakini lugha unayotumia ni tofauti.

RAI: Kwa mantiki hiyo ADC ipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani?

HAMADI: ADC tupo tayari kushirikiana kwa mambo ya msingi. Vitu ambavyo si vya msingi hatushiriki kwa mfano maandamano hatutokwenda. Huwezi kwenda kushawishi watu kupoteza maisha.

RAI: Ushirikiano ulioanza kuoneshwa na vyama vingine vya upinzani umeelezwa kuenenda hadi katika Uchaguzi Mkuu 2020 kwa kuunda umoja utakaosimamisha mgombea mmoja, Je, unazungumziaje mpango huo?

HAMADI: Wakati Ukawa inaanzishwa nilisema unapoingia kwenye taasisi yoyote hakikisha ni taasisi ambayo imesimama kisheria, ndio maana miungano yote iliyoanzishwa imeishia kuvurugika. Wenzetu Kenya wamefanikiwa kwa sababu wameunda kisheria. Mimi siwezi kushirikiana kinadharia. Lazima tukubaliane kisheria. Tulikuta majungu chungu nzima 2015, ambapo CUF walisimamisha wagombea wao na Chadema wakasimamisha.

RAI: Waswahili husema, ‘vita vya panzi furaha kwa kunguru’ kwa kuwa CUF imepatwa na mpasuko upande wa Maalim Seif na ProF. Lipumba, unafikiri ADC ambacho ndicho chama kilichokuwa kinafuatia kwa upinzani Zanzibar kimefaidika na hali hiyo?

HAMADI: Hapana, kwanza sikukubaliana kabisa na uamuzi wa Maalim Seif kuwazuia wawakilishi kushiriki uchaguzi au hata kuchukua hatua za kwenda mahakamani, ni jambo la ajabu sana, walikuwa tayari wana asilimia zaidi ya 45 kwenye baraza la wawamkilishi.

ADC hatuangalia CUF wameanguka sisi tufurahie, hapana lengo letu kuhakikisha demokrasia inakua, haijalishi amefaidika ADC au CUF. Niseme kwa kweli haukuwa uamuazi wa busara kuzuia washiriki uchaguzi. Alikuwa nafasi nzuri sana ya kufanya mazungumzo kwa sababu alikuwa makamu wa rais.

Walipokataa wao kuingia, ADC tukasema nafasi hatuwezi kuiacha, tumepata nafasi moja, watu wameona uwajibikaji wetu kwenye wizara ya kilimo na sasa wizara ya afya. Tunatumia lugha ya kutumia vitendo zaidi kuliko maneno. Popote tulipo tunatekeleza majukumu yetu hatuoni haya.

ADC tunasema tuna nafasi nzuri kwanza wametufahamu, na wameona ni kiongozi wa namna gani, ukiwa kiongozi unatakiwa kuweka alama, ila kuwaambia watu wasizikane, wasioane ni jambo la hovyo.

RAI: Mwaka jana kulidaiwa kuwapo kwa migogoro ya kikatiba ndani ya ADC, je, bado ipo?

HAMADI: ADC tunaamini katika kusameheana, tunaweza kukoseana ila lazima tusameheane. Hakuna utaratibu wa kusema tunamtenga mtu. Ndio maana kukitokea jambo tunaweza kulimaliza sisi wenyewe ndani yetu. Na tunaendelea vizuri hakuna mpasuko wa aina yoyote.

RAI: Kwa kuwa inatafsirika kuwa nguvu kubwa zimeelekezwa Zanzibar, je kuna mikakati yoyote ya kuimairisha chama Tanzania Bara?

HAMADI: Sio kweli upande wa bara, tumeweka matawi mengi Mbeya na Ruvuma kote huko tumefanya kazi kubwa, tumerudi Unguja, Kigoma na sasa Mtwara, tunaendelea tatizo hatufanyi kazi kwa kelele, sisi ni amani tu.

RAI: Katika siku za karibuni Tundu Lissu ametajwa kushika hatamu vyama vya upinzani katika nafasi ya urais 2020, unadhani atakuwa ni mtu sahihi wa kuungwa mkono na wapinzani?

HAMADI: Urais ni taasisi na taasisi ina miiko na taratibu zake za kuiendesha. Ni mapema sana kusema anaweza kuongoza wapinzani katika nafasi hiyo, taasisi ya urais ni pana sana. Kwa mfano Magufuli kuna vitu vingi ameviibua huko nyuma havikuonekana lakini pia kuna vitu vingi alifanya Mwalimu Nyerere alijenga urais kama taasisi na sasa vinabomolewa.

Sisemi kuwa Lissu hawezi kuwa rais au hafai, ila lazima tujue tunahitaji mtu wa aina gani kuongoza. Ni mapema mno kusema Lissu anatufaa kutuongoza, huwezi kukadiria kuwa anaweza kuwa na umaarufu au alivyo sasa akawepo mwaka huo 2020. Kikubwa wananchi ndio watakaoamua.

Chadema wana Mbowe vilevile anaweza kusema na mimi nagombea. Sisemi Lissu ni mbaya, ila kikubwa taasisi yenyewe iamue. Kwa mfano 2020 ninataka kugombea urais Zanzibar, ila wananchi ndio watakaoamua.

RAI: Ipo dhana iliyojengeka kuwa mpinzani akishateuliwa na kiongozi wa chama kilichopo madarakani kushika nafasi za kiserikali, ni sawa na kumalizwa kisiasa kama ilivyotokea kwa Morgan Tsvangira – Zimbabwe au Raila Odinga – Kenya, sasa upo ndani ya Serikali ya CCM- Zanzibar, unafikiri nafasi unazoshikilia zimekudumaza kisiasa?

HAMADI: Ni kweli au si kweli, kwamba unaposhiriki katika serikali yapo mambo ya msingi unakubali kushiriki bila kupenda. Unapoapa unakamata katiba na kitabu cha imani yako. Kwamba utaitii serikali yako, wakati ni hilo lilikuwa ni jambo ambalo ulikuwa unalipinga kabla hujala kiapo.

Kwa sababu kuna mambo ambayo hayapo katika sera za chama chako. Kwa mfano ADC tulikuwa tunaamini asilimia 70 kufanya kazi, 30 kupiga maneno. Nilipokuja kwa Dk. Shein anasema tusifanye kazi kwa mazoea, huku Magufuli anasema hapa kazi tu. Kwa hiyo nilichofanya ni kuoanisha tu sera ya ADC na CCM.

Inategemea uwezo wa kisiasa wa kiongozi aliyepo madarakani. Tukiweza kufanya kazi kwa pamoja mambo yanaenda vizuri kabisa, kwa mfano nimefanya kazi wizara ya kilimo kwa siku kadhaa lakini nilipoondoka nimeacha heshima ya hali ya juu na sasa nimekuja kwenye afya vilevile watu wanakubali kazi ninayofanya.

Ndio maana wenzetu hawachagui chama, wanachagua mtu. Hatutizami Chadema tunatazama kiongozi aliyepo anatufaa?

Nitastaafu siasa 2025

RAI: Ni yapi matarajio yako kisiasa?

HAMADI: Nimejipanga kuwa ikifika 2025 nitastaafu siasa, sifanyi kama Maalim Seif kufia kwenye siasa hapana, nitagombea urais 2020 kwa mara ya mwisho. Nikipata sawa, nisipopata basi nakaa pembeni namalizia kutumikia uenyekiti wangu wa chama kwa sababu katiba ya chama chetu uongozi wa juu ukomo wake ni miaka 10.

Kwa hiyo nitakapostaafu nitakaa nitawashauri vijana namna ya kufanya siasa. Huo ndio mpango wangu na nawaomba wanachama wa ADC wanipitishe kugomnbea urais 2020.