Home Latest News HAMASA YA MKUTANO WA VIONGOZI WA KOREA ITADUMU?

HAMASA YA MKUTANO WA VIONGOZI WA KOREA ITADUMU?

5623
0
SHARE
NA HILAL K SUED    |  

Ilionekana ni rahisi kusahau kwamba kiongozi huyu alitishia dunia nzima kwa kutaka kuanzisha vita ya nyuklia, hakusita kuwanyonga wapinzani wake pamoja na kutuma majasusi nchi za nje kuwamaliza mahasimu wake. Kwa ujumla alisimamia utawala wenye rekodi mbaya zaidi dhidi ya haki za banadamu duniani katika miaka ya karibuni.

Lakini pamoja na hayo yote, Kim Jong Un, kiongozi wa Korea ya Kaskazini alionyesha tabasamu kubwa wakati akitembea kuelekea mstari unaotenganisha sehemu ya kaskazini na ya kusini ya eneo huru (Demilitarized Zone –DMZ), eneo lisilokuwa na askari wala silaha baina ya Korea mbili asubuhi ya Ijumaa iliyopita, Aprili 27.

Kim aliunyoosha mkono wake kati kati ya mstari wa mpaka, akisalimiana na kiongozi mwenzake wa Korea ya Kusini, Moon Jae-in kabla ya kutambuka na kuingia kabisa Korea ya Kusini. Na katika hali isiyo ya kawaida Kim Jong Un alimsihi mwenzake kuvuka mstari huo na kuingia Korea ya Kaskazini, na baadaye wote wawili hao walivuka na kuingia kusini tena tayari kwa kuanza mkutano wao.

Mkutano huu unaonyesha kwamba ni mara ya kwanza kabisa kiongozi wa Korea ya Kaskazini kusafiri hadi kusini tangu mwisho wa vita ya Korea mwaka 1953. Katika kipindi hicho cha miaka 65, mara mbili marais wa Korea ya Kusini walitembelea Pyongyang (mji mkuu wa Korea ya Kaskazini) kwa ajili ya mikutano – mwaka 2000 na 2007.

Kabla ya mkutano wa wiki iliyopita kulikuwapo matukio kadha, mbali na kupeana mkono: ukaguzi wa gwaride uliofanywa na vikosi vya Korea ya Kusini waliovaa sare za karne ya 19 za rangi mbali mbali na upandaji wa “Mti wa Amani” katika eneo hilo la mpakani.

Matukio haya yalikuwa na ishara moja kuu – kwamba viongozi wawili hawa walionyesha kwamba nchi zao zinaweza kuweka pembeni ‘uadui’ wao wa jadi na kufanya mazungumzo ya dhati.

MKUTANO ULIIBUA HAMASA KUBWA K. KUSINI

Kwa upande wa Korea ya Kusini, tukio hilo liliibua hamasa kubwa. Mitandao ya kijamii ilisheheni ujumbe wenye mshangao na hamasa kubwa. Wananchi barabarani walisimama kuangalia runinga kwenye migahawa na vituo vya treni zilizokuwa zinaonyesha tukio hilo la kihistoria. Wanafunzi nao walipewa muda kuangalia tukio hilo katika runinga.

Hata wale wenye misimamo mikali kuhusu jirani wao wa kaskazini walishangilia wakati viongozi hao wawili walipopeana mikono, huku wengine wakibubujika na machozi.

Lakini pamoja na yote hayo, matokeo ya mazungumzo yao hayakubeba kitu kipya, yalikuwa ya kawaida kufuatana na tamko la pamoja lililosainiwa na viongozi hao wawili.

“Viongozi wawili wanatoa taarifa mbele ya wananchi 80 milioni (wa Korea zote mbili) na dunia nzima kwa ujumla kwamba katu hakutatokea tena vita katika Ras ya Korea,” sehemu ya tamko hilo ilisema.

Aidha viongozi hao wawili walitoa azma yao ya ‘kumaliza rasmi ile Vita ya Korea’ hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu. Hilo latarajiwa kufafanyika kwa kuigeuza ile ‘hali ya kuacha mapigano’ (armistice) na kuwa ‘mkataba wa amani’ (peace treaty) ikisaidiwa na Marekani na China.

Baada ya kuendeleza mradi wake wa nyuklia na kufanikiwa kutengeneza bomu la zana hiyo na kufurahia kila anapofyatua kombora sasa Kim Jong Un anautangazia ulimwengu angependa kuona Ras ya Korea haina zana za nyuklia.

TAMKO LA PAMOJA HALIKUWA LIPYA

Hata hivyo wadadisi wa mgogoro wa Ras ya Korea wanasema tamko lililotiwa saini katika mkutano wa wakuu wa nchi hizo mbili mwaka 2007 lilikuwa katika lugha hiyo hiyo katika suala la nyuklia, na halikutekelezwa.

Wadadisi wa mambo wanasema Kim Jong Il, baba wa kiongozi wa sasa wa Korea ya Kaskazini alikuwa na tabia ya kudanganya kuhusu makubaliano kuhusu zana za nyuklia hata kabla ya wino kukauka katika hati ya makubaliani hayo.

Lakini wote wawili hao, baba na mwanae waliona kwamba zana za nyuklia pekee ndiyo muhimu katika kudumu kwa itawala wao na wao pia.

Hata hivyo, lugha ya tamko la safari hii halikuweka bayana sharti la Korea ya Kaskazini, ambalo linaweza kuharibu mazungumzo yote yaliyofanyika au yajayo –sharti la kutaka majeshi ya Marekani yaondolewe kutoka Korea ya Kusini.

Rais Moon (wa Korea ya Kusini) amedai kwamba mwenzake wa Kaskazini yuko tayari kuachana na wazo hilo, lakini kama ni hivyo, hakukuwapo na ishara yoyote katika tamko lao. Kwa ujumla hakukuwepo masharti yoyote muhimu wawili hao waliyowekeana.

Pamoja na hayo, wadadisi wa mambo wanasema hakukuwapo na uwezekano wowote wa suluhu kamili kuhusu suala la nyuklia kufikiwa bila ya msaada wa Marekani. Utawala wa Rais Donald Trump umeyapokea matokeo ya mkutano huo na Rais huyo aliandika kwenye akaunti yake ya twitter: “VITA YA KOREA KUMALIZIKA! Marekani na watu wake lazima wajivunie kinachotokea Korea!”

MKUTANO UTASAIDIA MKUTANO WA TRUMP NA KIM

Kwa namna mkutano wa viongozi wa Korea ulivyokuwa na jinsi Trump alivyopokea matokeo yake, ni dhahiri mkutano wake (Trump) na kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu (Mei) au mwanzoni mwa Juni utafanyika.

Lakini nini yatakuwa matokeo ya mkutano huo, au hata nini pande mbili hizo zitajadili bado kujulikana.

Wadadisi wa mambo katika nchi za Magharibi wanasema mwisho wa Vita Baridi mwanzoni mwa miaka ya 90 kungeweza kuleta enzi ya maendeleo makubwa ya watu duniani. Wakati huo wengi waliamini kwamba hakungekuwepo tena mashindano ya kutengeneza silaha, vita za uwakilishi (proxy wars) au uonevu kwa mataifa madogo.

Kila mtu angekuwa anashughulikia kuinua ubora wa hali ya maisha yao. Lakini sasa hivi watu hawazungumzii hayo tena kwani hata sasa ambako kuna uwezekano kwa mgogoro wa Korea, ambao ni kama ukurasa ambao haukumalizwa uliotokana na uhasama baina ya dunia ya mashariki na ya Magharibi sasa unakaribia kupatiwa ufumbuzi. Sasa ni kwanini hali hii isionekane kuwa ni ashirio la amani?

Kuna baadhi ya wadadisi nchini Marekani wanasema sababu huenda ni kwamba mkutano wa viongozi hao wawili wa Korea ni matokeo ya kile walichokiita ‘matamko ya kivita-vita’ yanayotolewa na mtambo wa Trump.

Wanasema hitimisho la hali hii ni la hatari kwa sababu hakuna kitu kilichoelezwa bayana juu ya maelewano kuhusu hali ya mpakani baina ya nchi mbili hizo.

Kwa upande wa Korea ya Kaskazini wadadisi wanasema Kim Jong-un anahitaji ahueni ya haraka kutokana na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa wakati huo huo ikizuia mamlaka za ukaguzi wa mradi wake wa nyuklia, pamoja na haki ya kutaka kuondolewa kwa majeshi ya Marekani kutoka ardhi ya Korea ya Kusini.

Na kwa upande wa Marekani, Trump anahaha kupata hadhi fulani katika sera zake za nje na atakuwa anamtumia vyema Kim Jong-un katika azma yake hiyo.

Tusisahau kwamba Kim Jong-un ni miongoni mwa msururu wa viongozi wengi wa Korea ya Kaskazini ambao wamekuwa wakimudu vitisho vya Marekani na kusalimika.