Home Latest News HAPPINESS MAGESE: MTU MMOJA ALIYEBEBA WANAWAKE MILIONI 176

HAPPINESS MAGESE: MTU MMOJA ALIYEBEBA WANAWAKE MILIONI 176

1681
0
SHARE

NA GRACE SHITUNDU

KUWA  mama ni jambo la asili kwa mwanamke  na huwa ni furaha na  faraja anapopata mtoto lakini huwa ni huzuni na masikitiko kwa mwanamke kukosa mtoto hasa wakati wa kupata mtoto unapokuwa umefika.

Tatizo la kukosa watoto kwa sababu mbalimbali linawasumbua wanawake wengi ambao wamekata tamaa ya kuitwa mama.

Miongoni mwa wanawake hao alikuwepo mrembo Happiness Millen Magese ambaye alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa endometriosis ambao huhusisha seli zinazofaa kuwa ndani ya mji wa uzazi kuwa nje ya mji huo.

Kwa zaidi ya miaka 23 amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Endometriosis ambao hauna tiba ambapo hupata maumivu makali kipindi unapokuwa katika siku za hedhi na kusababisha tatizo la kutoshika ujauzito.

Anaonekana kuwa shujaa wa kipekee kwa kuingia katika mapambano  dhidi ya ugonjwa huo kwa  kuhamasisha mamilioni ya wanawake ambao wameathirika  matatizo hayo.

Magese aliweka wazi juu ya tatizo lililokuwa likimsumbua na kuanzisha Taasisi Millen Magese Foundation kuhamasisha a uwepo na athari ya ugonjwa huu, ambao unaathiri wasichana wapatao milioni 176 kote duniani.

Alianzisha kampeni ya Let’s Face it – Period ambayo inatoa elimu kwa jamii kuhusiana na hedhi na usafi.

Hatimaye wiki iliyopita alitangaza ushindi kwa kupata mtoto wa kiume aliyempa jina la Kairo.

Pamoja na mateso ya miaka isiyopungua 20 na kuambiwa hawezi kupata mtoto hatimaye Julai 13 mwaka huu maisha ya Magese yamebadilika kwa kuitwa mama.

Mrembo huyu mshindi wa Miss Tanzania mwaka 2001 alijifungua mtoto katika hospitali ya Colombia iliyopo jiji la New York nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Millen alianza kupata maumivu makali anapokuwa katika siku za hedhi tangu akiwa na umri wa miaka 13 na baada ya miaka 13 aligundulika kuwa na ugonjwa wa Endometriosis na kufanyiwa upasuaji zaidi ya mara 13.

 

Wiki iliyopita Magese alirudisha tumaini kwa wanawake wengine ambao hawajabahatika kupata mtoto kwa sababu  yoyote.

 

Katika akaunti yake ya  mtandao wa kijamii wa Instagram aliandika maneno yenye kuonyesha hisia na jambo lenye miujiza na ameweka picha yake aliyobeba mtoto akiwa kitandani katika mazingira ya hospitali.

 

“Lete tumaini, imani na miujiza kwa mamilioni ya wanawake ambao wanaohitaji kubeba watoto wao kama jinsi nilivyotamani kukubeba wewe, Wewe mshindi wangu”anaandika Magese.

 

Anaongeza kuandika, “Ukue ili ubadilishe ulimwengu na uwepo kwa ajili ya wengine. Uamini Mungu na miujiza yake. Na bila kujali kitakachotokea katika maisha yako, kumbuka una Mungu wetu Mwenye nguvu na nitakuwa hapa daima,”

 

Mrembo huyu kwa kuonyesha kuwa imetokea miujiza katika kupata mtoto wake kwanza ameendelea kuandika maneno ya kumshukuru Mungu kwa hisia zake mwenyewe.

 

“Naamini tiba ya Endometriosis iko karibu. Tutusaidieni, kwa kila mtu  asisahau kamwe, ikiwa ulijua nani aliyekuwa karibu na wewe, wakati wote kwenye njia uliyochagua, huwezi kamwe kupata hofu au shaka tena, kuwa na imani, simama  na imani yako, badilisha hadithi yako na unaweza,” alimalizia kuandika

Millen amewekeza katika  kampeni ya kutoa elimu ya ugonjwa endometriosis ambao  wanawake zaidi milioni 176 kusumbuliwa nao  duniani kote.

Millen kupitia taasisi yake ya Millen Magese Foundation, amekuwa akihamasisha wanawake hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuhusiana na Endometriosis ambapo amekuwa mstari wa mbele kushirikiana serikali na wadau katika kutafuta ufumbuzi wa ugonjwa huu.

Mwanamtindo huyu anajulikana katika ulimwengu wa mitindo na amewahi fanya kazi za uanamitindo nchini Afrika Kusini chini ya Kampuni ya Ice Model Management kabla hajahamia katika Jiji la New York, nchini Marekani ambapo anaendelea na shughuli zake za mitindo.

Katika mahojiano na BBC mwaka 2015 Magese anasema alipatikana na ugonjwa huo baada ya kupata hedhi yake ya kwanza miaka 13 iliyopita wakati huo.

“Sikuwahi kufikiria kuwa siku yangu ya kwanza kuanza kupata hedhi ningeweza kuanza kupata maumivu makali ambayo yamekuwa ni vita vikali katika maisha yangu,” anasema Magese katika mahojiano hayo.

Anasema  amefanya jitihada kadhaa kuhakikisha anakabiliana na ugonjwa huo, na tayari amefanyiwa upasuaji mara 13 .

Maumivu yanapozidi sana, yeye hulazimika kunywa dawa za kupunguza maumivu na wakati mwingine hata kujidunga sindano.

“Huwa najiuliza, niliwahi kutumia kitu gani kibaya au kwa nini ninapitia mateso haya kutokana na endometriosis?

Mwaka huo alianzisha kampeni inayosema Many Faces for Endo, Speak out!” (Sura nyingi za Endo, Usinyamaze).”

Katika kampeni hiyo, wanawake walijipiga picha na kuwahamasisha wengine kuweka picha wakiwa kwenye pozi mbalimbali katika mtandao wa kijamii wa Instagram, kampeni hiyo ilifana sana na ilinishindia tuzo.

Millen Magese Foundation inahudumia nchini Marekani, Afrika Kusini na pia Tanzania.

“Ninataka kuhamasisha watu kuhusu endometriosis na matatizo mengine yanayowakabili wanawake. Sitaki kuona msichana mwingine wa umri wa miaka 13 akiteseka kutokana na endometriosis.”

Dk. Esther Eisenberg kutoka kituo cha kitaifa cha afya nchini Marekani anasema ugonjwa huo ambao husababisha ugumba kiini chake hakijulikani vyema.

“Inawezekana kuwa wakati mwanamke akiwa katika siku zake, ndipo madhara hujitokeza katika mishipa ya ukuta wa mji wa uzazi na damu hiyo ya hedhi kumwagika nje ya mishipa hiyo,” anasema.

Hivyo madhara yake huathiri maeneo yote ya mishipa ya uzazi yaani fallopian tubes, uteras na mji wote wa uzazi.

“Lakini ninachokiona hapa ni kwamba tunapaswa kufanya uchunguzi zaidi ili kuwa na uelewa mpana wa ugonjwa huu,” daktari huyo anatahadharisha