Home Burudani Hashim Kambi: Sikutaka baba yangu anipigie saluti

Hashim Kambi: Sikutaka baba yangu anipigie saluti

2416
0
SHARE

NA GEORGE KAYALA

WAKONGWE wa sanaa ya igizo nchini umri wao unazidi kuwatupa mkono kila kukicha huku wengine wakitangulia mbele ya haki wakiwa na hazina vichwani mwao.

Miaka ya nyuma kulikuwa na vipindi vya maigizo vilivyokuwa vinarushwa na Radio Tanzania (RTD) sasa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) enzi ambazo Radio ndio ilikuwa kila kitu katika suala zima la kupata habari.

Kipindi hicho kulikuwa na ushindani mkubwa sana wa michezo ya kuigiza ya redio (radio drama) na ilikuwa na mvuto mkubwa kwa watu wengi kutokana na kwamba mbali na burudani lakini michezo hiyo ilikuwa ni sehemu maalum ya mkakati wa kutoa elimu ya masuala mbalimbali, ikiwemo kujikinga na magonjwa, ulipaji kodi, kilimo cha kisasa, ushirika na mambo mengine.

Watu hawakupenda kukosa michezo hiyo na kulikuwa na wasanii maarufu sana kama vile Mzee Jangala, (Bakari Mbelemba) marehemu Bi Nyakomba (Catherine Mapunda), Mzee Kipara (Fundi Said), Pwagu (Rajab Hatia), (Pwaguzi) Ali Keto, King Majuto, (Amri Athumani) na Mzee Small (Said Ngamba)  na wengine wengi ambao kwa hakika walifanya kazi kubwa sana ya kuelimisha na kuburudisha.

Unapowazungumzia waigizaji wakongwe waliokula chumvi nyingi hivi sasa kwenye fani ya Bongo Movie bila shaka jina la Hashim Kambi alimaarufu Mzee Kambi halitakosekana.

Mkongwe huyo ambaye ameshiriki katika filamu nyingi sana hapa nchini ni mmoja wa wasanii waliopitia kiopindi cha mabadiliko kutoka kwenye tamthiliya za televisheni hadi kwenye filamu hivyo ameona mengi kwenye tasnia hiyo.

Mzee Kambi alianza sanaa ya maigizo mwaka 1998 akiwa na kundi la Kamanda Art Family. Alianza kuonekana kwenye mchezo wa Uhondo uliokuwa unarushwa na kituo cha luninga cha ITV akiwa anatumia jina la Benjamin.

Pamoja na kwamba ameona mengi, jambo moja ambalo linampa tabu sana Mzee Kambi ni jinsi ya kuwapata warithi wa sanaa ya maigizo kutokana na mfumo unaotumika sasa kutoonyesxha matunda ya kupata wasanii mahiri.

Mzee Kambi anasema kuwa njia ambayo inafanywa hivi sasa kwa ajili ya kuwapata wasanii haifai kwani wanaofanya utaratibu huo wapo kimasilahi zaidi zaidi. “Nakerwa na utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na wasanii wa filamu kwa kuwasaka waigizaji kutoka mikoani kwa kuwatoza fedha kisha kuwashindanisha na wakishapata mapato hayo wanawaacha,” anasema.

“Mbali na hiyo, tumekuwa hatuna utaratibu mzuri, waongozaji na watayarishaji wanaangalia mtu fulani mwenye umaarufu na kumuingiza kwenye filamu si kwa wasichana tu bali hata kwa wavulana, wasiwasi wangu ni kwamba hao akina Kambi wengine watatoka wapi kama tunajikitaka kuingiza warembo na wavulana wenye sura nzuri?” anahoji.

Msanii huyo anaeleza njia sahihi ya kuwapata waigizaji wazuri ni kuunda kundi la waigizaji wenye vipaji kisha kuwatengenezea mchezo ili kila mmoja aoneshe uwezo wake wa kucheza na si kuwalia fedha kisha wanawatelekeza hali inayosababidha tasnia hiyo ionekane imejaa matapeli.

“Mimi ni msanii ninayejiheshimu kwenye tasnia ya filamu. Ni mtu mzima. Napenda sana sanaa yetu maana inatusaidia lakini napenda iendelee kuwasaidia vijana wetu , sisi umri wetu umeshakwenda kwa hiyo hatuwezi kukaa kwenye uigizaji kwa muda mrefu.

“Itafikia mahali tutakaa pembeni na kuwaacha vijana waendelee, hivyo kuna kila sababu za kuanzisha makundi ya maigizo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na sisi tukajulikana badala ya kuendesha mashindano ya kula fedha za wanyonge na kisha kuwaacha wakiwa hawana cha kufanya,” alieleza Mzee Kambi.

Msanii huyo alieleza kuwa si jambo baya kufanya hivyo lakini namna wanavyoendesha ndipo kwenye tatizo lilipo. “Nimeshaona mara nyingi, baadhi ya wasanii tena wenye majina makubwa wanakwenda mikoani na kutangaza kuwasaidia chipukizi lakini cha ajabu  wanawatoza fedha kati ya shilingi 5,000 na 10,000 kwa ajili ya fomu, na baada ya hapo hawawapi hata mrejesho wa shindano lenyewe.

“Swali la kujiuliza, chipukizi huyo ndiyo kwanza anatafuta kutoka, bado unachukua na pesa yake, hapo umemsaidia kweli au unamkandamiza? Cha kuchekesha wakishakusanya hizo fedha, wanaishia kutangaza majina ya wasanii wachache kuwa wameshinda halafu wanahamia mikoa mingine,” anaeleza Mzee Kambi.

Mzee Kambi alieleza kuwa yeye uwezo wake wa kuigiza aliuonesha akiwa na kundi la Kamanda Art Family ambapo alicheza kwa muda wa miaka mitatu na kisha kuhamia Kundi la Shirikisho Msanii Afrika lenye lililokuwa na maskani yake Sinza jijini  Dar es Salaam ambalo michezo yake ilikuwa ikirushwa na Runinga ya ITV.

Kwenye Shirikisho Msanii Afrika alifanikiwa kucheza michezo kama Hatia, Darubini, Wimbi na mingine mingi. Mbali na michezo ya kwenye luninga, Mzee Kambi anaeleza filamu yake ya kwanza kuigiza ilikuwa ni Penzi la Baba kati ya mwaka 2002 na 2005 akiwa ndani ya Shirikisho Msanii Afrika.

Msanii huyo ni miongoni mwa wasanii wa muda mrefu ambaye amekuwa akishirikishwa kwenye filamu za waigizaji mbalimbali lakini hana mafanikio makubwa kutokana na sanaa hiyo licha ya ukongwe wake huo.

Anaeleza enzi za kuanza kwao kuigiza ilikuwa ni kama kujiburudisha na kutoa elimu tofauti na sasa ambapo imekuwa ajira. Mzee Kambi anajivunia kufahamika katika jamii japo mafanikio kisanaa siyo makubwa. Tangu aanze kuigiza mwaka 1998 hadi sasa, amefanikiwa kununua kiwanja nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mbali na sanaa Mzee Kambi ni mwanasoka mzuri. Mkongwe huyo aliwahi kuwa mcheza wa timu ya Yanga. Alisajiliwa kuitumikia timu hiyo mwaka 1978, na timu hiyo ilienda kuweka kambi ya mazoezi ya mwezi mmoja nchini Romania.  Wakati huo alikuwa  mwajiriwa wa Shirika la Bima Tanzania.

Kabla ya kujiunga na timu ya Yanga alikuwa anacheza Tumbaku na baadaye alitakiw akuchezea timu ya Magereza ya mkoa wa Morogoro, lakini aligoma kwa kuheshimu nafasi ya baba yake mzazi.

Baba yake alikuwa anafanya kazi katika Jeshi la Magereza mkoani Morogoro akiwa na cheo ya usajenti hivyo kama angekubali kujiunga na timu hiyo, angepelekwa kozi na baada ya hapo angekuwa bosi wa baba yake.

“Kila mchezaji wa timu hiyo alikuwa anapelekwa chuo cha Magereza hivyo nami ningepelekwa kutokana na elimu yangu, baba angelazimika kunipigia saluti kitu ambacho sikutaka kitokee,” alieleza Mzee Kambi.