Home kitaifa ‘Hata Bunge letu ni jipu’

‘Hata Bunge letu ni jipu’

2479
0
SHARE

bungeNA MALIMBILI MWAMLIMA

WAHENGA walisema ‘Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu’ Wakiwa na maana kwamba, watu wanapoamua kuuganisha nguvu na fikra zao ili kuzitumia kwa pamoja na kwa manufaa ya pamoja ni rahisi  kufanikiwa kuliko kila mtu kutumia nguvu na akili zake kwa manufa yake binafsi.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni chombo kilichoundwa kisheria, ambacho kulingana na malengo ya kuundwa kwake kinapaswa kutumika kuwakutanisha watu pamoja,  walioaminiwa na wananchi ili kwa umoja wao  watumie fikra zao kwa manufaa ya nchi na wananchi wake, kwa kujadili kwa hoja, wakiwa na lengo moja na wamoja.

Kwa maana hiyo, tunapozungumzia vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumzia vikao ambavyo wahusika wanapaswa kuweka pembeni tofauti za makabila yao, dini na ufuasi wa vyama vyao vya siasa, na kukaa pamoja kwa umoja, wakisukumwa na uzalendo kutanguliza maslahi ya nchi na wanachi wake.

Vikao hivyo vya Bunge vilishaanza mjini Dodoma, jambo la kusikitisha ni kwamba, licha ya kuwa inatakiwa viwe na sura inayosadifu kuwa ni vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vinavyotambulika kikatiba, vimeendelea kukosa sura hiyo. Pia vimeendelea kukosa kile kinachojulikana kuwa ni malengo ya kuundwa kwa chombo hicho muhimu cha Bunge.

Kinachoonekana kinaweza kuleta tafsiri kuwa Bunge la nchi yetu lilishaporwa. Vikao vyake havina sura inayosadifu kuwa  ni chombo cha wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa kisheria bado linatambulika hivyo.

Halitumiki kwa maslahi ya Watanzania, bali linaonekana kutumika kwa maslahi binafsi ya wanasiasa. Vikao vyake vimetawaliwe na hoja za Uchama-tawala na Upinzani.

Wahusika hawafanyi shughuli zinazowapasa kufanya kama wabunge, badala yake wanafanya mambo yao binafsi kwa kusukumwa na chuki za kiitikadi katika ufuasi wa vyama.

Hawaonyeshi kuwa ni watu waliokaa kwa pamoja, kwa umoja, wakiwa na lengo moja kuhusu nchi yao kama inavyotakiwa. Ni watu  waliojengeana chuki na wivu uliopitiliza na kusababisha fahamu zao kuwehuka, hivyo kushindwa kufanya kazi wanayopaswa kuifanya kama wabunge.

Wameligeuza Bunge kuwa uwanja wa mapambano, dhihaka, kejeli na hoja zinazolenga kufitinishana.

Hatua stahiki  zichukuliwe. Kwa kuwa mambo wanayoyafanya wabunge wetu ikilinganishwa na gharama zinazotumika katika kuwalipa ni majipu yanayolitia hasara taifa letu. Yanapaswa katumbuliwe.

Kama ni kanuni kali ziwekwe. Kama zipo zitumike pasipo kumuogopa mtu. Wakati huo huo wabunge wajitafakari. Waache kusema ‘Bunge ni chombo cha kutunga sheria, kuisimamia na kuikosoa serikali’ wakati wao pia wanapaswa kujikosoa kabla ya kukosoa wengine kwa kuwa nao pia ni sehemu ya serikali.

Watambue hawajaenda bungeni kwa ajili ya kugonga meza na kuunga hoja kwa sababu tu ni hoja ya Serikali inayoongozwa na chama chao, hata kama haina tija.

Hawajaenda kwa ajili ya kupinga kila hoja kwa sababu tu inatoka upizani hata kama ni hoja ya msingi.

Kadhalika watambue kuwa hawajaenda bungeni kwa ajili ya kupinga kila hoja ya Serikali kwa sababu tu serikali iliyopo madarakani si ya chama chao.

Kupitia makala haya sina maana kwamba ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao hawalitumii vyema Bunge letu tukufu, ingawa inasemekana samaki mmoja akioza ndani ya kapu wote Watanuka na kuonekana hawafai.

Natambua wapo wabunge wa Chama cha Mapinduzi wenye hekima na busara zao, pia wapo wabunge wa upande wa upinzani ingawa hekima zinaweza kutofauti.

Ni vema wabunge wenye hekima watumie hekima zao kuwaelimisha wenzao ili nao pia watambue majukumu yao wakiwa kama wabunge.

Wenye uelewa na ufahamu mzuri kuhusu Bunge wasikatishwe tamaa na hali inayoendelea kwenye vikao vya bunge ambayo inasababishwa na wachache walioamua kwa makusudi ama kutojua kuligeuza Bunge kuwa kama sehemu ya kupiga soga.

Ni wajibu wao kuutanguliza utaifa mbele huku wakitambua hali mbaya ya maisha waliyo nayo Watanzania.

Watanzania wenye mapenzi mema na  taifa hili tupo nyuma yenu tukipigana pamoja nanyi kwa kutumia fursa tulizonazo.

Wabunge makini wasiogope kuitwa mamluki, wasaliti na wapinzani katika vyama vyao, Waendelee kupambana kwa umoja wao kama wabunge, pasipo kubaguana kwa itikadi ya vyama vyenu vya siasa, dini wala tofauti za makabila yenu.

Ikihitajika kukosoana kosoaneni kwa namna ambayo haiwezi ikawafanya mtafsiriane vibaya. Busara na hekima zitumike  haipendezi kukosoana kwa kubwekeana kama mbwa. Kila mmoja akubali kukosolewa na kujirekebisha awe waziri, spika, naibu, mwenyekiti au mbuge wa kawaida. Kwa kuwa hakuna mtu aliyekamilika chini ya jua.

Nawatakia kheri katika majukumu yenu mazito ya kulitumika Taifa.

Mungu awabariki na kuwatangulia katika kila hatua.