Home kitaifa Hata wasiohusika wanaisoma namba

Hata wasiohusika wanaisoma namba

1365
0
SHARE

Baadhi ya watuhumiwa wa kesi ya makontena wakiingia mahakamaniNa Franklin Victor

UAMUZI sahihi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli (JPM) kuwapa siku saba wafanyabiashara waliokwepa (au kukwepeshwa) kulipa kodi ya makontena yao, kuhakikisha wanalipa kodi stahiki serikalini unaonyesha namna Rais anavyojipanga kwa kutazama na kupima faida ya maamuzi yanayopaswa kufanywa na serikali yake.

Pia, uamuzi wa serikali kuwafungulia mashtaka maofisa wake waliohusika kwa namna moja ama nyingine na upotevu au kutolipwa itakiwavyo na kutakiwako kodi ya serikali kwa maendeleo ya nchi una mantiki zaidi kwa kuwa endapo watendaji wa serikali, wafanyakazi wa umma wanaamua kutenda kwa weledi, uaminifu na uhakika, haiwezekani kwa wafanyabiashara kuamua tu na kufanikiwa kukwepa kodi, kutolipa maduhuli ya nchi kutakiwako.

Watu wa kulaumiwa pale kodi ya nchi inapochepushwa kwenda kusikojulikana au kupotea kirahisi tu mbele ya macho ya serikali si wafanyabiashara bali watendaji wanaozembea majukumu yao au wanaofanya mipango yao ya makusudi yenye nia ya kuipora mapato serikali.

Vitu kama urasimu, rushwa, ubinafsi, tamaa za kilafi na utendaji wa chini ya viwango usiojali wananchi vinavyoendekezwa na baadhi ya watendaji wa umma ndilo jipu kuu lihitajilo kutumbuliwa mapema kabla halijakithiri na kufanya iwe shughuli pevu wakati wa utumbuzi/ utumbuaji. Tanzania inawahitaji zaidi wafanyabiashara walipa kodi kuliko wafanyakazi wanaoendekeza mazoea yenye hasara kwa nchi na watu wake.

Kuna watu siasani walidhani, na wengine bado wanadhani Dk. Magufuli anao wajibu mahsusi wa kuwasikiliza wao kuliko anavyotakiwa kuwasikiliza kwa utuo washauri wake na wananchi wake.

Baadhi ya wanasiasa wanahisi Dk. Magufuli huyu rais wa serikali ya awamu ya tano ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ni yule aliyekuwa waziri katika serikali zilizopita, kwa namna ile ile ya zamani.

Wanadhani rais anayeongoza serikali ya Magufuli kwa kuwa ametokea chama kile kile tawala basi itakuwa ngumu kwake kukidhi kiu ya mabadiliko kwa wananchi bila kuweka ukada mbele.
Rais Magufuli anajinasibu kuweka maslahi ya nchi kwanza, akimtanguliza Mungu mbele, si chama wala ukada.

Hili hadi sasa anaonekana kulimudu, serikali yake inawatia matumaini wananchi wengi kwa jinsi inavyotenda na kuamua kwa wakati.

Uyakini wa kuiweka nchi kwanza ukiendelea kuthibitika, huku ukihanikizwa kwa kauli mbiu ‘Hapa Kazi Tu’ na utendaji wa kiwango cha juu uliozoeleka wa Dk. Magufuli, heshima ya Tanzania kikanda, Afrika na kimataifa inarejea muda si mrefu.
Matukio ya hivi karibuni yanaonesha serikali ya Magufuli ina dhamira ya dhati kujitofautisha na serikali zilizotangulia.

Ingawa bado mapema lakini utendaji wa rais na wasaidizi wake unawavutia wananchi wanaosubiri kwa hamu kuona namna atakavyounda baraza la mawaziri lenye watendaji wachache lakini mahiri watakaoisaidia serikali kusimama upande wa umma pengine dhidi ya mifumo, sheria, kanuni na taratibu kandamizi.

Wengi wako macho kuona namna rais Magufuli atakavyokuwa kiini cha mabadiliko ya kweli kama alivyojinadi wakati wa kampeni na sasa akiwa mamlakani ikulu pamoja na viongozi wenzake; Makamu wa Rais Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Mwanasheria Mkuu, George Masaju, na makatibu wakuu bila kuingiliwa au kuathiriwa na mifumo mazoea.

Maamuzi magumu yameanza kufanywa na serikali ya Magufuli, sakata la awali likizihusu mamlaka mbili; Mamlaka ya Mapato – TRA na Mamlaka ya Bandari – TPA.

Mpaka sasa kuna maofisa wa serikali wanaoisoma namba kutokana na ushiriki wao katika sakata lililoikosesha serikali kodi shilingi bilioni 80 kutokana na makontena 349 ya makampuni zaidi ya 43 kutolipiwa kodi husika serikalini.
Waziri Mkuu Majaliwa amegundua uwepo wa makontena mengine zaidi ya 2,431 yanayoonekana kutoroshwa bandarini bila ushuru!
Namba kwa maana ya tarakimu ziundazo Sh. bilioni 12.7, ambazo ni kodi ya makontena 329, inasomwa na bandari kavu Azam ya jijini Dar es Salaam.

Fedha hizi zimeanza kulipwa serikalini kufuatia rais Magufuli kutoa huruma ya siku saba na kuwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi tajwa. Magufuli anawaambia wafanyabiashara watakaoshindwa kulipa kodi ndani ya siku hizo wataisoma namba kweli.

Tayari maofisa waandamizi nane wa serikali wameshitakiwa kwa uhujumu uchumi, kula njama na kuisababishia hasara ya mabilioni serikali huku wengine, wakiwemo wafanyakazi 25 wa TRA wakiisoma namba kwa kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi na hatua zaidi.

Wale vigogo waliokuwa wakifurahia kuendeshwa na magari ya kifahari kwa kodi za wananchi, waliokuwa wakipulizwa upepo safi, baridi wa vipozeo vya magari, ofisi au kumbi za kimataifa zinazopatikana ughaibuni au kwenye hoteli za hadhi ya nyota tano wakifanya mikutano ya bodi huku wakijenga mazoea ya kukejeli wapinzani kisiasa kwamba wataisoma namba kwa kupinga ulaji ukiwaona wanavyohaha sasa kwenda sambamba na utendaji wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa unaweza kuwahurumia.

Jasho linawatoka vigogo waliozoea kutenda kwa mazoea, wengine presha zinapanda kila kukicha wakihofia ziara za kushtukiza, maswali ya ghafla na mustakabali wao kwa ujumla.

Watendaji wengi wanaoziona dalili mbaya kuwaelekea, wanaozisikia sauti za bundi kila walalapo kutokana na kuamini sana nguvu za ushirikina badala ya umahiri kiutendaji wanajua ni muda tu ndiyo uliobakia kabla hawajajikuta wakiisoma namba kwa sauti au kimoyo moyo, kimya kimya.

Wengi wanaisoma namba kwa namna wajuazo, wakiwemo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari waliokuwa wanufaika wakubwa wa fedha za umma kupitia sherehe kama maadhimisho, matamasha, dhifa, tafrija zilizokuwa zikigharamiwa na serikali.

Kwa serikali hii ya Magufuli, matumizi yasiyo ya lazima, matumizi yenye tija hafifu yameota mbawa. Walioyazoea na kunufaishwa nayo wanaugulia, wametulia tuli kokote walipo, wanaisoma namba.

Watendaji wengine wa serikali wanaosubiri muda kushuhudia ziara za kushtukiza kisha waisome namba ni pamoja na wa mashirika yanayokera umma kwa kutoa huduma kwa mtindo wa ‘pasua kichwa’.

Nani asiyekerwa na ukatikati ovyo wa umeme? Nani hakasirishwi na kuahirishwa kwa safari bila taarifa kunakofanywa kuwa kawaida na mashirika ya reli? Nani asiyeumia kusikia viwanda vilivyokuwa vikizalisha kwa tija kabla ya kubinafsishwa vikigeuka maghala ya wawekezaji binafsi? Namba itasomwa sana endapo serikali ya Magufuli itaendelea kutenda kwa namna hii bila kubadilika mbeleni.

Rais Magufuli amekuwa gumzo kitaifa na kimataifa, jambo lililo jema kwa ustawi wa nchi; na changamoto kwake kuhakikisha haiharibu kazi yake nzuri inayompa sifa hizo. Serikali hii ya awamu ya tano ina kila uwezo wa kuwa kipenzi cha Watanzania pale itakapomudu kuendelea na moto huu ilioanza nao ili wananchi hawa wajivunie Utanzania popote walipo.
Binafsi najua, kivunwacho kilipandwa.
0772 066 667.