Home Habari Hatima ya Fastjet Desemba 11

Hatima ya Fastjet Desemba 11

1441
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA

HATIMA ya kampuni ya ndege ya Fastjet inatarajiwa kujulikana Desemba 11 mwaka huu, baada ya kufanyika kikao kupitia maombi ya kampuni mbalimbali zilioomba kutoa huduma ya usafiri wa anga nchini.

Kampuni hiyo ilisitisha huduma zake baada ya kukabiliwa na hali mbaya ikiwamo kukosa ndege za kutolea huduma, pamoja na kukabiliwa na madeni iliyokuwa ikidaiwa na watoa huduma mbalimbali.

Akizungumza na RAI, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa Desemba 11 mwaka huu wanakutana kujadili maombi hayo, baada ya kikao kilichopangwa kufanyika Novemba 26 kushindwa kufanyika kutokana na baadhi ya maombi yaliyowasilishwa kutokamilika.

“Kikao cha kupitia hayo maombi kitafanyika tarehe 11, kikao cha jana (juzi) hakikufanyika, kwa sababu kuna baadhi ya application (maombi) hazikukaa sawa, wakaomba tuwaongezee muda, kwa hiyo Desemba 11 ndio tutazipitia,” alisema Johari.

Hivi karibunu Johari alisema mamlaka hiyo ingekutana Novemba 26 kupitia na kufanya tathmini ya maombi ya kampuni mbalimbali ikiwamo Fastjet, na kwamba endapo kampuni hiyo itakidhi vigezo vya kisheria, itaruhusiwa kuendelea kutoa huduma.

Kabla ya kusitisha kutoa huduma nchini, Fastjet iliandamwa na matatizo ya mara kwa mara ikiwamo kuahirisha safari.

Kutokana na hali hiyo, Desemba 17 mwaka jana, TCAA iliiandikia kampuni hiyo notisi ya siku 28 ikiitaka kujieleza kwa nini isifutiwe leseni ya kutoa huduma hiyo nchini baada ya kukosa sifa, ikiwamo kutokuwa na ndege baada ya moja kati ya mbili zilizosajiliwa nchini kuharibika na kupelekwa nje ya nchi kwa matengenezo, huku moja ikizuiwa na mamlaka hiyo, ili kulinda madeni waliyokuwa wakidaiwa na watoa huduma mbalimbali.

Ndege hiyo ilizuiwa baada ya kampuni iliyowakodishia Fastjet kuitaka irudishwe kwa kile walichodai kuwa inafanya kazi bila wao kupata chochote, jambo ambalo liliilazimu TCAA kuizuia ndege hiyo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya sheria iliyoianzisha mamlaka hiyo pale inapotokea kampuni au shirika la ndege linakabiliwa na madeni, hadi hapo madeni yote yatakapolipwa.

Sababu nyingine ya ndege hiyo kusitisha huduma ni kukabiliwa na madeni makubwa iliyokuwa ikidaiwa na watoa huduma mbalimbali ikiwamo TCAA yenyewe, ambayo ilikuwa inadai zaidi ya Sh bilioni 1.413 pamoja na kutokuwa na meneja uwajibikaji ambaye ni lazima awe mtaalamu wa masuala ya kiufundi ya ndege.

Kutokana na kampuni hiyo kukosa ndege, ililazimika kuazima ndege nyingine moja kutoka Afrika Kusini, ili kuiwezesha kuendelee kutoa huduma, ndege ambayo pia ilizuiwa baada ya kubainika kuwa ni mbovu.

Sababu nyingine ni kushindwa kuwasilisha andiko linaloonesha kubadilishwa umiliki kutoka kwa mmiliki wa awali ambayo ni kampuni kutoka nchini Uingereza kwenda kwa wafanyabiashara wazawa, andiko ambalo pia lilitakiwa kuelezea mikakati waliyojiwekea ili kuhakikisha shirika linajiendesha bila kutetereka.

Fastjet ilijikuta katika wakati mgumu siku chache baada ya kufanya mabadiliko ya umiliki, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kupitia kwa Ofisa Uhusiano na Masoko wa Fastjet, Lucy Mbogoro, kutangaza kununua asilimia 64 ya hisa za kampuni hiyo, hivyo kuongeza hisa zake kufikia asilimia 68 kutoka nne alizokuwa akimiliki awali.

Katika ununuzi wa hisa hizo uliotajwa kama mpango wa kuboresha kampuni hiyo, Masha alinunua asilimia 17 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni mama ya Fastjet PLC ya Afrika Kusini na asilimia 47 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na wawekezaji wazawa na kuifanya kampuni hiyo imilikiwe na Watanzania kwa asilimia 100.

Mwisho.