Home Michezo HATIMA YA TFF MIKONONI MWA WAPIGA KURA

HATIMA YA TFF MIKONONI MWA WAPIGA KURA

965
0
SHARE

download (4)

NA MWANDISHI WETU

MIAKA, miezi, wiki hatimaye siku tatu tu zimebaki kabla ya           kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaoingiza madarakani safu mpya ya uongozi utakaokuwa na mtihani mkubwa wa kulisogeza mbele soka.

Licha ya mchakato wa uchaguzi huo kugubikwa na matukio kadhaa bado hatima yake inaachwa kwa wajumbe wa mkutano Mkuu wa TFF ambao ndiyo wenye dhamana ya kuwaweka madarakani viongozi kwa mujibu wa katiba.

Wajumbe ndio hasa watu wa kutazamwa kwa sasa kwani kupata au kukosekana kwa viongozi bora kutatokana na maamuzi yao siku hiyo ya uchaguzi hivyo hawatakwepa lawama iwapo watawachagulia watanzania viongozi legelege na vilevile hawatakosa pongezi iwapo wataweka madarakani viongozi sahihi kwa maendeleo ya mchezo huo.

Macho na masikio ya wadau wote wa soka nchini na hata nje ya nchi yataelekezwa mjini Dodoma kunakofanyika uchaguzi huo ambao pengine unaweza kuweka historia kutokana na jinsi mchakato wake ulivyokwenda.

Kuenguliwa ‘kiana’ kwa baadhi ya wagombe kama vile Rais wa sasa anayemaliza muda wake Jamal Malinzi ambaye alijitosa katika hatua za awali za kuwania tena kiti hicho lakini ameshindwa kuingia katika hatua za mwisho kupigiwa kura kutokana na kesi inayomkabili ya tuhuma za utakatishaji fedha akiwa pamoja na watendaji wengine wa TFF, ni moja ya mikasa iliyoikumba uchaguzi huo.

Sakata la uraia wa mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti, Wallace Karia nalo lilichukua nafasi yake ingawa baadaye utata huo ulimalizwa na Idara ya Uhamiaji kumthibitisha kuwa ni raia halali.

Lakini pia tukio la kukamatwa kwa baadhi ya wagombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kwa madai ya rushwa huko jijini Mwanza, Elius Mwanjala, Shafii Dauda, Benista Rugora nalo lilichukua nafasi yake. Hata hivyo baadaye Dauda alijitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa ujumla uchaguzi wa mwaka huu umegubikwa na hofu kubwa kwa wapiga kura kuhofia kutiwa hatiani kwa madai ya kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wagombea.

Taasisi ya Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) angalao katika uchaguzi huu imeonesha meno yake kwani uchunguzi uliofanywa na RAI umebaini tofauti kubwa ya kati ya uchaguzi wa mwaka huu na ile iliyopita hasa katika suala la rushwa.

Miaka iliyopita kuna nyakati wagombea walikuwa wakifanya ushawishi kwa wapiga kura kwa njia ya fedha wakiwa katika mazingira ya wazi lakini kipindi hiki hali imekuwa tofauti sana hata ile tu kukuta mikusanyiko ya wazi baina ya wagombea na wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndiyo wapiga kura.

Mkono mrefu wa Takukuru umesababisha wajumbe wa mkutano huo kuwa na hofu hata ya kukutana na wagombea katika mazingira waliyozoea katika miaka ya nyuma.

Mpaka sasa wagombea wa nafasi ya uenyekiti na makamu ndiyo wanaoonekana kuwa katika upinzani mkubwa kutokana na ukongwe wao katika fani hiyo. Wagombea hao Wallace Karia, Fredrick Mwakalebela, Emmanuel Kimbe, Ally Mayayi, Imani Madega na Shija Richard wote wanawania nafasi ya Uenyekiti.

Wanaogombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Michael Wambura,Mlamu Ng’ambi, Stephen Mwakibolwa, Robert Selasela, Mtemi Ramadhani.

Pamoja na kuwa sura zilizojitokeza ni zilevile zilizozoeleka miongoni mwa wadau wa soka nchini kwani wengi ni wale waliokuwa madarakani hivyo wanataka kutetea nafasi zao au wale waliokuwa katika klabu au vyama vya mikoa lakini sasa wakitaka kupanda ngazi na kuingia ‘Ikulu’ hiyo ya soka.

Awali Malinzi ambaye alikua anatetea nafasi yake alikuwa anatarajiwa kupata upinzani mkubwa kutoka kwa msadizi wake Karia japokuwa rais huyo anayemaliza muda wake anatajwa kuwa na wafuasi wengi kutokana na kusaidia viongozi wengi wa soka kushinda chaguzi za vyama vya mikoa.

Lakini kuchomoka kwake katika kinyang’anyiro hicho bado hakumpi nafasi kubwa karia kutokana na ukweli kwamba ‘team Malinzi’ wamepanga kummaliza kwa kupeleka kura zao kwa mgombea mwingine ili tu kumkoa mgombea huyo.

Wachambuzi wa masuala ya soka hapa nchini wanampa nafasi kubwa Karia, Mwakalebela na Shija wakiamini kama atakayeshinda atakuwa si makamu wa rais wa sasa wa TFF basi atakaeshinda atanufaika na kura za Malinzi.

Kampeni zimeanza kwa wagombea kujinadi licha ya ukweli kuwa walio wengi walishapita na kutafuta ushawishi wa kuungwa mkono hivyo kinachoendelea hivi sasa ni kama kuhitimisha tu.

Wagombea wengi walitumia mikusanyiko ya matukio ya kisoka kama vile mechi za timu ya soka ya taifa hasa ile iliyofanyika kule jijini Mwanza Julai  mwaka huu ambapo ilikutanisha wagombea wengi halikadhalika na wapiga kura pia.

Vyovyote itakavyokuwa uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa mgumu kulingana na mazingira halisi yaliyopo. Lakini pia mgombea atakayeweza kuwashawishi wapiga kura kutokana na sera zake zenye mlengo wa kuleta mabadiliko katika mchezo huo bila shaka ndiye atakayeibuka mshindi.

Kwa mantiki hiyo kuna kila dalili ya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na heshima kubwa kama siyo kuwa huru na haki kutokana na jinsi vyombo vya dola vilivyo makini kuhakikisha amani inatawala wakati wote.