Home Habari Hatua ya Kenya kufunga mipaka na diplomasia ya Tanzania

Hatua ya Kenya kufunga mipaka na diplomasia ya Tanzania

178
0
SHARE
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu

NA ABBAS MWALIMU

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta hivi karibuni alitangaza kufunga mipaka ya Kenya kwa watu kutoingia nchini humo ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona huku akiruhusu malori ya shehena za chakula tu kuingia nchini humo.

Hatua hiyo ilizua sintofahamu kwa raia wa nchi hizo mbili ambao wana mwingiliano wa karibu kimaisha, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Kwa upande wake Rais Dk. John Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa hatofunga mipaka kwa kuwa Tanzania inategemewa na nchi takribani nane katika ukanda wa Mashariki na Kusini hivyo kufunga mipaka ni kuumiza uchumi wa nchi hizo.

Siku ya Jumatatu ya Mei 18 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella alitangaza kuzuia malori yote yanayoingia Tanga kupitia mpaka wa Horohoro hadi pale serikali ya mkoa itakapojiridhisha na afya za madereva hao kutoka nchi jirani.

Ni wazi kuwa kuzuiwa kwa magari kutoka nchi ya Kenya na nchi nyingine kuingia katika mkoa wa Tanga kupitia Horohoro mpaka pale mkoa utakapojiridhisha na afya za madereva wa malori kutoka nchi za jirani, kutaiathiri sana nchi hiyo kwani inaitegemea Tanzania kwa mazao ya nafaka, mbogamboga na matunda.

Kauli hii ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga imezua maswali kutoka kwa baadhi ya watu.

Je Mkuu wa Mkoa amefunga mpaka?

Si kweli kuwa mkuu wa mkoa wa Tanga amefunga mpaka, bali amezuia gari kuingia mpaka pale mkoa utakapojiridhisha kuwa madereva hao wa nchi jirani ni salama.

Tufahamu kuwa Mkuu wa Mkoa ana wajibu wa kikatiba wa kusimamia mambo yote yanayohusu mkoa wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Ibara ya 34.- (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaelekeza kwamba:

‘Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.’

Kwa msingi huo wa Katiba, Mkuu wa mkoa wa Tanga ametekeleza jukumu lake la kikatiba ikiwa ni pamoja na kulinda afya za wakazi wa mkoa wa Tanga.

Hivyo suala la eneo la Horohoro ni la kimkoa ambalo Mkuu wa Mkoa ana mamlaka nalo na si suala la kufungwa kwa mpaka.

Mwenye mamlaka ya kufunga mipaka ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Rejea ibara ya 34. -(3) ambayo inaeleza wazi kwamba:

‘Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.’

Suala la mipaka ni suala ambalo lipo moja kwa moja mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Hivyo ingekuwa ni suala ambalo lingehitaji uingiliaji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ibara ya 32 ingemuongoza Rais kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba.

Rejea ibara ya 32 ibara ndogo ya pili ambayo ingemruhusu Rais kutangaza hali ya hatari endapo janga la Covid-19, kule Tanga lingemtaka aingilie kati kama ilivyoelezwa kwenye vifungu (d), (e) na (f) pamoja na kuchukua hatua stahiki ikiwemo hiyo ya kufunga mipaka:

(d) kuna hatari dhahiri na kubwa, kiasi kwamba amani ya jamii itavurugika na usalama wa raia kutoweka katika Jamhuri ya Muungano au sehemu yake yoyote ambayo haiwezi kuepukika isipokuwa kwa kutumia mamlaka ya pekee; au

(e) karibu kutatokea tukio la hatari au tukio la balaa au la baa ya kimazingira ambalo linatishia jamii au sehemu ya jamii katika Jamhuri ya Muungano; au

(f) kuna aina nyingineyo ya hatari ambayo kwa dhahiri ni tishio kwa nchi.

Kwa kuona hatari iliyopo mbele yao Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu imebidi aitishe mkutano na waandishi wa habari na kueleza hatua ilizochukua Kenya na uhusiano wake na Tanzania akitaja kuwa si majirani tu bali ni ndugu.

Je Kenya iliteleza wapi katika hili?

Suala hili lilihitaji majadiliano ya kina ya nchi hizi mbili. Hivyo kabla ya kuchukua hatua ya kufunga mipaka kulikuwa na umuhimu kwa Kenya kujadiliana na Tanzania kama ambavyo Rwanda ilifanya na nchi hizo mbili kufikia makubaliano kupitia Bilateral Consultations.

Majanga kama Covid-19 ambayo huvuka mipaka ya nchi (cross/ transborder) huwa na athari kwa nchi husika pale inapochukua maamuzi kama huu wa Kenya kwa sababu huweza kuwa na athari hasi katika utekelezaji wa sera za nchi nyingine katika eneo la kikanda na hivyo kuiathiri nchi husika endapo nchi nyingine zitachukua hatua mbadala. Changamoto ya Kenya ilikuwa hapa.

Barry Buzan amefafanua hili kwa kina katika Regional Security Complex Theory (1991, 1998, 2003).

Kwa mtazamo wangu, nadhani Kenya walipofanya vile (kufunga mipaka) walitarajia Rais Magufuli azungumzie hatua yao au Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi azungumzie au labda Balozi wa Tanzania kule Nairobi azungumzie.

Ajabu iliyowashangaza ni kwamba aliyezuia magari ni Mkuu wa Mkoa jambo ambalo amelifanya kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kimsingi Serikali ya Kenya haina uwezo wa kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa sababu sheria zinazohusu Uhusiano wa Kimataifa (Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961) na hasa mawasiliano baina ya nchi na nchi (diplomatic correspondence) haziruhusu kufanya hivyo, hivyo basi imemlazimu Balozi Dan Kazungu ambaye ni mwakilishi wa Rais Uhuru Kenyatta Tanzania azungumze na waandishi wa niaba ya Rais wa Kenya.

Kama angezungumza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu mpaka wa Horohoro au Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo ingekuwa ni kauli ya Wizara ya Kisekta hivyo ingechukuliwa moja kwa moja kuwa ni kauli ya serikali ya Jamhuri ya Muungano au kauli ya Rais.

Pia angezungumza Msemaji Mkuu wa Serikali hiyo ingekuwa ni kauli ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuzungumza kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kikanuni inachukuliwa kuwa si kauli ya Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali ni Serikali ya Mkoa husika katika kujilinda na janga la Covid-19.

Winston Churchill alipata kusema: “Diplomacy is the art of telling people to go to hell in such a way that they ask for directions.”

Wenu: Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter)+255 719 258 484