Home Latest News HEKIMA ZA VIONGOZI WA DINI ZINAHITAJIKA

HEKIMA ZA VIONGOZI WA DINI ZINAHITAJIKA

2611
0
SHARE

NA GOODHOPE AMANI

TANGU aingie madarakani kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano, Rais John Magufuli, amekuwa akijinasibu kuwa anataka kuwaletea maendeleo wananchi wa kada ya chini na kukomesha rushwa na umasikini unaosababishwa na unyonyaji. Jambo hili ameendelea kulisisitiza kila mara na kuongeza kuwa yeye ni Rais wa wote.

Itakumbukwa kasi kubwa aliyoanza nayo ikiwamo kutengua uteuzi wa wateule wake walioenda kinyume na matarajio yake maarufu kama “Tumbua jipu”. Ziara za kushtukiza katika ofisi mbalimbali ambazo kwa namna moja ziliongeza nidhamu ya kazi ingawa wapo wanaoona imezidisha nidhamu ya woga na kuweka kando utaaluma.

Moto huo ndio ulioonyesha dhamira yake ya kuleta mabadiliko katika uendeshaji wa chama chake (CCM) kama Mwenyekiti na Rais.

ara kadhaa Rais Magufuli katika ziara zake pindi azungumzapo na wananchi na kutatua kero mbalimbali, amesikika akiwasihi wananchi wamuombee kwa Mungu katika vita anayopambana nayo ili aweze kuwaletea maendeleo.

“Ukiwa Roma, kuwa Mroma.” Msemo huu unajidhihirisha waziwazi, kwanini Rais Magufuli amejitahidi kuwa wa hali zote ili kufanya jamii imuelewe nini hasa anatamani Watanzania wakipate.

Nasema hivi kwakuwa wananchi walio wengi wanaamini uwepo wa Mungu hivyo kuwafanya wawe na dini zao ambazo wanazithamini na kuziheshimu. Kwa kutumia mantiki hiyo, Magufuli amefanikiwa kuhudhuria na kufanya  ibada au kujumuika pamoja na waumini wa dini zote kubwa hapa nchini kwa nyakati mbalimbali suala ambalo kwa namna moja au nyingine, linachangia kuungwa mkono kwani wananchi huguswa zaidi pale wanapomuona Rais akiwatembelea katika madhehebu yao bila kujali tofauti zao.

Itakumbukwa Magufuli ameshiriki huduma kadhaa ikiwa ni pamoja na ibada ya majivu Ushirika wa Mtakatifu Petro Osterby, Ibada ya Jumapili KKKT Ushirika wa Moshi Mjini, Kuadhimisha  mwaka mpya wa Kiislamu katika Msikiti wa Bohora na hivi karibuni kuhudhuria katika ibada ya Sabato Kanisa la Magomeni Mwembe Chai, ambapo pia alichangia ujenzi wa kanisa hilo kwa kutoa mifuko 400 ya sementi.

Aidha, kwa nyakati tofauti Rais amekutana na viongozi mbalimbali wa kidini Ikulu pindi anapokuwa na shughuli muhimu zinazogusa masilahi ya Taifa kama kukabidhiwa ripoti za masuala ya madini.

Uhusishwaji wa viongozi wa dini katika shughuli za kiserikali ni jambo muhimu ingawa siasa haipaswi kuchangamana na masuala ya kidini. Viongozi wa kidini wanapaswa kuwepo kama washauri huku wakiliombea Taifa liendelee kuwa na amani pamoja na maendeleo.

Pamoja na ushirikishwaji huu wa viongozi wa dini, juhudi za Rais Magufuli kuleta maendeleo ni kama kuna mvutano unajitokeza unokwamisha gurudumu kusonga mbele.

aon sasa ni wakati wa Serikali kuhitaji hekima za viongozi wa kidini ili kusaidia gurudumu la maendeleo kusonga mbele. Nasema viongozi wa dini kwani natambua viongozi hawa ndio wenye nguvu na husikilizwa sana na waumini wao kuliko hata tunavyoweza kudhania.

Yapo mambo kadhaa ambayo yanafikirisha kichwa hasa ukiyatafakari kwa undani, wapo baadhi ya viongozi waliozoea kupiga madili ila sasa mambo yamebadilika na hivyo kuanza kupandikiza chuki kwa viongozi mbalimbali wa Serikali.

Wapo watu na vikundi vya watu vilioamua kuendesha oparesheni za matukio maovu, kama vile mauaji na wizi ambavyo vimepewa majina ya “watu wasiojulikana” vinavyochafua sura ya nchi na kudumaza jitihada za maendeleo.

Aidha, wapo viongozi wanaojitia kuunga jitihada za maendeleo ilihali ni wanafiki wakifunika kombe mwanaharamu apite.

Hata hivyo, upo upande wa vyama vya upinzani unaona baadhi ya maamuzi yanayochukuliwa na serikali hayafuati taratibu, na kuwafanya wahoji ijapokuwa kuhoji kwao kumezidi kuamsha maswali chungu nzima na wengine hata kuhojiwa uzalendo wao.

Ukiachana na hayo, yapo masuala kama bomoa bomoa ya nyumba zilizopo kando ya barabara. Licha ya kwamba hatua hizo zinachukuliwa kwa maendeleo ya nchi, wengine wanadai mashauri yao bado yapo mahakamani, bado bomoabomoa iliendelea kushika kasi hadi Rais alipoamua kusimamisha bomoabomoa ya nyumba zaidi ya 17,000 jijini Dar es Salaam.

Fikiria wakati wengine wakipiga sala kumuombea Rais apate nguvu ya kusimamia masilahi ya nchi, wengine kama wakazi wa Kimara waliobomolewa nyumba zao wana lalama watalala wapi, sina uhakika kama watakuwa wanamuombea Rais aendelee kutetea masilahi ya umma.

Katika hali kama hii na mazingira kama haya, viongozi wa dini pekee ndio wanaoweza kuweka mambo haya sawa. Tukubali tusikubali, viongozi wa dini wanayo sauti kubwa kwa waumini wao na kwa vile wanachokisema wao ndio waumini hufuata, lazima wawahubirie umuhimu wa kusimama kama taifa kutetea masilahi yetu ndipo sasa mambo mengine yafuate.

Lazima viongozi wa dini wasimame madhabahuni, vimbwetani wapige kelele kukemea uonevu usio wa msingi unaoendelea katika jamii, lazima wasimame kuwataka wananchi kuweka masilahi ya nchi mbele kwa maendeleo ya jamii. Lazima wasimame kuishauri Serikali bila upendeleo na bila woga juu ya njia bora za ustawi wa jamii.

Kama viongozi wa dini hawatatumia busara zao walizopewa na Mungu kukemea maovu, kuhamasisha haki na kushauri kwa busara, maendeleo ya Taifa yakizidi kudorora machozi ya wananchi yatawaangukia mikononi mwao.