Home Latest News HELLEN KIJO-BISIMBA: NILITAMANI MCHAKATO WA KATIBA UKAMILIKE KABLA SIJASTAAFU

HELLEN KIJO-BISIMBA: NILITAMANI MCHAKATO WA KATIBA UKAMILIKE KABLA SIJASTAAFU

4668
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA                  |                


BAADA ya kuhudumu kwa miaka 23 katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, hatimaye Julai 30, mwaka huu, amestaafu kama Mkurugenzi wake.

Dk. Bisimba aliyeanza kutumikia kituo hicho kama Mjumbe wa Bodi mwaka 1995, atakumbukwa kutokana na misimamo mbali mbali aliyoiamini kuhusu masuala yanayohusu haki za binadamu na utawala wa sheria, ambapo mara kadhaa alijitojekeza kukemea, kuonya na hata kwenda mahakamani kupinga mambo ambayo aliamini yanakiuka misingi ya haki za binadamu.

Baada ya kustaafu rasmi, RAI limepata nafasi ya kufanya naye mahojiano. Katika mazungumzo hayo, aliwatakwa watetezi wa haki za binadamu nchini, kutafuta mbinu mpya za kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu. Mahojiano yalikuwa hivi.

RAI: Naomba kufahamu ni mambo gani ulitamani kuyatimiza katika utetezi wa haki za binadamu?

HELEN: Nilitamani Watanzania wazijue haki zao na wawe na uthubutu wa kuzidai pale zinapokiukwa. Nilitamani watendaji wa Serikali, hasa wale wanaosimamia haki, wazielewe haki hizo na wawe watende kazi zao kwa kulinda na kuziheshimu haki hizo.

Nilitamani vijana wa nchi yetu, wawe wabadilishaji wa tabia za kutoheshimu haki, na tabia zinazodharau na kubagua watoto na wanawake, na makundi ya watu wenye ulemavu, wazee na hata wakimbizi.

RAI: Kwanini ulitamani mambo hayo yatimie?

HELEN:Nilitamani hivyo kwa kuwa watu wakizifahamu haki zao, wataweza kuzilinda na kulinda haki za watu wengine, na nchi itakuwa na heshima. Haki ikitamalaki, kunakuwa na amani ya kweli nchini.

Watendaji kama polisi, mahakimu na watoa maamuzi, wote wakizifahamu na kuziheshimu haki za binadamu, wananchi watakuwa na imani na vyombo hivyo, na kupeleka shida zao huko, na hivyo kupunguza uwepo wa watu kujichukulia sheria mkononi.

Vijana wakibadilika kimtazamo, taifa litabadilika pia. Taifa likiwa na vijana wapenda haki, litakua taifa la wapenda haki.

RAI: Kati ya mambo hayo, ni mangapi umeyafanikisha?

DK.HELEN: Niliyofanikiwa  ni karibu yote na kwa njia mbali mbali. Kwa sasa tumevuka hali iliyokuwapo tulipoanza kazi. Watu walikuwa hawazijui haki zao na waliokuwa wanazijua, hawakuwa ama na uthubutu, au uwezo wa kuzifuatilia.

Kwa sasa hali imebadilika. Watu wengi zaidi wanazijua haki zao na wako tayari kuzifuatilia. Neno haki limevuma kwa watu wa rika zote—watu wa mijini na vijijini. Na kazi yangu  kupitia LHRC imewezesha hali hii kwa kiasi kikubwa.

Watendaji wa Serikali kama polisi, wana uelewa mkubwa wa haki za watu na wamefikia hatua ya kuanzisha  madawati maalumu ya  jinsia katika vituo vya polisi, lakini pia kwenye vituo vingi vya polisi kuna mabango yanayoelekeza haki za raia.

Tumefanikiwa kuwezesha uanzishwaji wa vilabu vya haki za binadamu katika shule na vyuo—hasa vyuo vikuu. Vijana hao wanaonekana wakifuatilia haki zao na za wenzao pale zinapokiukwa.

RAI: Ni mambo yapi uliyotamani yafanikiwe, lakini hadi unastaafu hukuyafanikisha? 

HELEN: Nilitamani sana mchakato wa Katiba Mpya ufikie hatima yake, maana tulianza nao mbali tangu shirika lilipoanzishwa, lakini kampeni maalumu niliiongoza miaka ya 1998 hadi 2000, LHRC ikijulikana kama Mtandao wa Katiba Mpya.

Nilitamani kuona nchi yetu inaridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Ukatili (CAT).  Nilitamani sana kuona wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapatiwa malipo yao.

Nilitaka kabla sijastaafu, wananchi wa Serengeti wa kilichokua Kijiji cha Nyamuma, wawe wamerejeshewa ardhi yao na kulipwa fidia, na yule aliyewatendea uovu huo wa kukiukia haki zao, amewajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Nilitamani kuona watoto wadogo wanalindwa dhidi ya ndoa za utotoni, na pia sheria zinabadilishwa ili kutoa ulinzi huo. Wale waliopatwa na dhahama ya kupata uja uzito, wasaidiwe kukabiliana na hali hiyo, na ikibidi waweze kuendelea na elimu kama walikuwa shuleni.

Kuhusu Katiba Mpya, tulifurahi mchakato ulipoanza 2011 hadi ulipokoma mwaka 2014. Iwapo ungeendelea, basi ningekuwa nimeridhika kuwa tumepata Katiba ya Wananchi. Lakini bahati mbaya mchakato ulitekwa na wanasiasa, ukakosa mwafaka na hata Katiba inayopendekezwa, haiwezi kutufikisha pale tulipokuwa tunapachuchumilia.

Wastaafu wa Jumuia ya Afrika Mahariki nao bado hawajaweza kulipwa haki yao na wengine wamekwisha kufa. Mkataba wa CAT kila wakati Serikalii husema iko katika mchakato na hadi leo mchakato haujakamilika. Hawa ndugu zetu wa Nyamuma, kila haki iko mikononi mwao, ila watekelezaji ndio wanaendelea kuishikilia haki hiyo.

RAI: Wakati fulani ulituambia kuwa unajutia kustaafu wakati huu, kwa sababu unaona kuna mambo ambayo yanakutamanisha kuendelea kupigania haki za Watanzania ila umri unakulazimisha upumzike. Ni jambo gani linakusababisha utamani kuendelea na kazi hii?

HELEN: Ni kweli, kwani tulifikia mahali pazuri kwenye haki za binadamu kufikia Mwaka 2015. Katiba iliokuwa na hati za haki za binadamu na kwa kiasi kikubwa zilikua zinafuatwa. Tulikuwa tayari na mfumo wa siasa wa vyama vingi na uliweza kufanya kazi vizuri kiasi chake, na kuwapo kwa chaguzi za mara kwa mara katika mfumo huo, pamoja na shida za hapa na pale.

Katika kipindi hicho, Wabunge wa vyama vya upinzani, walipata fursa kubwa ya kuibua madudu ndani ya Serikali na kwa kiasi Serikali iliweza kuyashughulikia kwa kiasi, hata Waziri Mkuu mmojawapo alijiuzulu baada ya kufumuliwa kwa kashfa ya  Richmond. Kashfa kama ile ya ESCROW—waliondoka mawaziri kama watatu.

Wananchi waliweza kufuatilia Bunge mubashara na kutoa mawazo yao pale ilipobidi. Lakini ghafla Bunge mubashara likasimamishwa, sheria zikaanza kutumika zinazozuia haki zilizopo kikatiba. Sheria kali kama ile ya Makosa ya Mtandao, inaminya haki za kujieleza na kupata habari, Sheria ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa, licha ya kuwa ilikuwapo, kipindi hiki imeanza kutumika kuminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kisiasa.

Matamko yakawa na nguvu kuliko Katiba na sheria. Mfano kauli za kuwa siasa zikome hadi uchaguzi ujao, wasichana wapatao mimba wakiwa shuleni, wasiwe na haki ya kurejea shuleni iwapo wana uwezo huo.

Pia tumeshuhudia matukio yakutisha nchini, kuvamiwa kwa ofisi za wanasheria kwa njia kadhaa, mfano LHRC baada ya uchaguzi kompyuta zilichukuliwa na baadhi ya watendaji wakakamatwa,  kupigwa mabomu ofisi za mawakili za IIMA, kupigwa risasi kweupe kwa Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, kupotea kwa watu kama Ben Saanane na mwandishi Azory Gwanda, mauaji  ya Kibiti—na hasa wimbi la askari polisi kuuwawa. Yote haya hayaonekani kujulikana na kupatiwa ufumbuzi.

Kwa hiyo, kutokana na hali hii, huu usingekuwa wakati wa kupumzika kazi, bali kutafuta mbinu mpya za kukabiliana na ukiukwaji huu mkuu wa haki za binadamu.

Hii kazi inapokuwa ngumu, ndiyo inapoleta ari ya kuifanya. Ilishaanza kuwa rahisi, ndio maana hata hamu ya kustaafu ilianza, lakini mabadiliko haya yaliinua ari ya kuifanya kazi hii, lakini wakati ukuta. Wapo watakaoiendeleza—tena kwa ari mpya, kwani kuna upya katika hali ya haki za binadamu nchini.