Home Makala Hifadhi ya Burigi Chato, itakavyochochea ukuaji wa utalii Kanda ya Ziwa

Hifadhi ya Burigi Chato, itakavyochochea ukuaji wa utalii Kanda ya Ziwa

1767
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU-MAELEZO

JUMANNE ya wiki hii, Rais Dk. John Magufuli, alizindua Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, katika Kijiji cha Mkolani eneo la Katete wilayani Chato, Mkoa Geita.

Akizindua hifadhi hiyo, pamoja na mambo mengine Rais Magufuli alisema kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo na Kimisi si tu kuna manufaa kwa mazingira na utalii bali pia ni mkakati wa kuimarisha ulinzi katika mapori hayo ambayo kwa kipindi kirefu yalikuwa maficho ya majambazi na hata wafugaji haramu kutoka nchi jirani.

Rais Magufuli anasema mkakati wa makusudi wa serikali yake, ni kuona vivutio vingi vya watalii vinaongezwa na vinalindwa ili kuwaletea tija wakazi wa maeneo yanayozunguka vivutio hivyo, lakini pia kuongeza mapato ya serikali kupitia utalii.

Anasema uboreshaji wa miundombinu ikiwemo, barabara na viwanja vya ndege kunaiwezesha sekta ya utalii kukua kwa kasi hivyo kuongeza ajira kwa watanzania.

Aidha aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhamasisha utalii wa ndani, kwa kuwa nao utachangia katika ukuaji wa pato la taifa badala ya kutegemea watalii kutoka nje pekee.

Uzinduzi wa huo ni mwanzo wa kufunguka kwa fursa mbalimbali zitokanazo na utalii katika mikoa ya Geita na Kagera ambayo hifadhi hiyo imo.

Vilevile sekta hiyo inapokua inaamsha pia ukuaji wa sekta nyingine mfano uzalishaji wa mazao ya chakula, matunda, mbogamboga na kadhalika kutokana na mahitaji yake kwenye mahoteli ya kitalii pamoja na wananchi kwa ujumla.

Kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Burigi, Biharamlo na Kimisi kuwa hifadhi ya taifa, kutatanua wigo wa utalii pamoja na kuongeza wawekezaji hapa nchini.

Hifadhi ya Burigi ina ukubwa wa kilometa za mraba 4,702 ikiwa ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa hapa nchini, hifadhi ya Ruaha ni ya kwanza kwa ukubwa ikiwa na eneo la kilometa za mraba 20,300, huku hifadhi ya  Serengeti ikiwa na kilometa za mraba 14,763 ndio inashikilia nafasi ya pili kwa ukubwa hapa nchini.

Rais Magufuli anasema Serikali imepata asilimia 25 ya fedha za kigeni kutokana na utalii, hivyo kuifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17 ya pato la Taifa, pia imetoa ajira za moja kwa moja zipatazo 600,000 na ajira zisizo za moja kwa moja milioni mbili hivyo kuchochea ukuaji wa sekta za biashara, usafirishaji pamoja na sanaa na utamaduni.

Anasema mbali na kuanzishwa hifadhi hiyo, serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii kwa kutengeneza miundombinu, kutangaza vivutio vya utalii, hifadhi za mazingira na uwezeshaji kwa wananchi walio karibu na vivutio hivyo, kadhalika na kuzidisha mapambano dhidi ya ujangili, uwindaji haramu na uvamizi wa mapori ya akiba.

Tanzania inashika nafasi ya pili kwa kuwa na vivutio 19 vya utalii duniani, nchi ya tano barani Afrika kwa kuwa na eneo kubwa lililotengwa kwa ajili ya utalii ambalo ni kilometa za mraba  361,594.

Serikali ilipigana vita dhidi ya ujangili pamona na uwindaji haramu uliopelekea baadhi ya wanyama kupotea, kabla ya kuimarisha vita dhidi ya ujangili na uwindaji haramu, idadi ya tembo ilikua 130,000 ambao walitoweka hadi kufikia tembo 43,330  kwa mwaka 2014, baada ya kuimarishwa kwa kikosi cha kupambana na ujangili idadi ya tembo imeongezeka kutoka 43,300 hadi 60,000 na faru wameongezeka kutoa 16 hadi 163 hadi kufikia mwaka huu.

Aidha, Serikali ilifanya jitihada za kuhamasisha utangazaji wa vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), ambao kwa kutambua mchango wa sekta ya utalii hapa nchini walianzisha chaneli mahususi kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania ijulikanayo kama SAFARI CHANNEL.

Kutokana na ongezeko la watalii hapa nchini kumekua na ongezeko la mapato, mfano mwaka 2015 serikali ilipokea Dola za Kimarekani bilioni 1.9 za kimarekani na  kuongezeka mwaka 2018 kufikia hadi Dola za Kimarekani bilioni 2.5  ambazo ni sawa na  Sh trilioni 5.9.

“Kulikuwa na ujangili ambao ulichangia kwa kiasi kikubwa wanyama kuhama kwenye hifadhi ambapo idadi kubwa ya wanyama kama tembo na faru walipotea lakini Serikali imejitahidi kupiga vita hadi sasa wanyama hawa wameongeza kwa asilimia kubwa pamoja na kutokomeza ujangili.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla anasema kuwa Hifadhi ya Burigi ni ya kipekee ambayo imezungukwa na maziwa takribani matano, yanayosababisha hifadhi hiyo kuvutia Zaidi.

Kigwangallah anasema wizara yake imejipanga kupambana na wanaharakati na wanasiasa wanaotaka kuleta chokochoko kwenye sekta hiyo kwa lengo la kukwamisha maendeleo ya utalii nchini, kwa kuchafua mazingira na kuchoma moto baadhi ya maeneo ya misitu kwa masilahi yao binafsi.

Fursa zitokanazo na kuanzishwa kwa hifadhi hiyo zianze kuchangamkiwa na wazawa wa maeneo hayo ili ziwanufaishe kiuchumi.

Pia wajipange hata kwa vikundi vya maendeleo kuchukua mikopo ili waweze kuwekeza hata kwenye nyumba za kulala wageni kwani mahitaji sasa yatakuwa makubwa.

Ni vyema pia kwa hifadhi za Taifa kuendelea kuitangaza hifadhi hiyo mpya, ili watalii hasa wale kutoka nje ya nchi wasiishie tu kutalii katika mikoa ya Kaskazini na Kusini kama ilivyozoeleka bali waende kwenye Hifadhi ya Burigi Chato.

Fursa hii sasa igeuke kuwa mkombozi wa kiuchumi katika Wilaya na Mikoa ambayo hifadhi hiyo inapatikana.