Home Habari Hifadhi za Taifa zaongeza ajira

Hifadhi za Taifa zaongeza ajira

790
0
SHARE

MIAKA 4 YA JPM

Na MWANDISHI WETU

KUONGEZEKA kwa hifadhi sita za Taifa katika kipindi cha mwaka 2015/19, kumeongeza ajira kwenye shughuli za utalii na kufikia watu 200,000.

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi, alitaja idadi hiyo wakati akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo katika kuadhimisha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, jijini Dar es Salaam.

Mbali na ajira hizo kwenye sekta zinazohudumia watalii, lakini pia kuongezeka kwa hizo kumetoa jumla ya ajira 850 ndani ya shirika hilo.

“Kuongezeka kwa idadi ya hifadhi kunaongeza uwiano wa fursa za utalii nchini pamoja na ajira. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwapo na ongezeko la ajira 850 katika Shirika.

“Pia kumekuepo na ongezeko la ajira kupitia taasisi binafsi na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani (value chain) wa biashara ya utalii katika hifadhi za Taifa.

“Kwa mfano, kumekuwapo na ongezeko la wastani wa ajira 100,000 hadi 200,000 katika maeneo yanayotoa huduma za malazi ya watalii (hoteli, nyumba za wageni na kambi za watalii), alisema.”

Kijazi alisema katika kipindi cha miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli ilipoingia madarakani, Shirika limepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali.

Miongoni mwa maeneo hayo ni kuongezeka kwa idadi ya hifadhi na ukubwa wa eneo la hifadhi za Taifa.

“Wakati tukipata Uhuru mnamo mwaka 1961, Taifa la Tanzania lilikua na hifadhi tatu tu za Serengeti, Ziwa Manyara na Arusha, zikiwa na jumla ya eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 17,000.

“Hadi kufikia mwaka 2015 kipindi ambacho Serikali ya sasa ya Awamu ya Tano ilikua ikiingia madarakani, Tanzania ilikua na jumla ya hifadhi za Taifa 16 zenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 57,000. Hivyo kwa kipindi cha miaka 54 tangu tumepata Uhuru kulikua na ongezeko la eneo la hifadhi za Taifa lenye ukubwa wa kilomita za mraba 40,000.

“Kwa kipindi cha miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, kumekua na ongezeko la hifadhi sita zaidi. Hifadhi hizo ni Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe; pamoja na hifadhi nyingine tarajiwa tatu za Nyerere, Kigosi na Mto Ugalla, ambazo kwa ujumla zina ukubwa wa kilomita za mraba 47,000.

“Hivyo miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuongeza eneo kubwa zaidi la uhifadhi (kilomita za Mraba 47,000) ikilinganishwa na lile lililoongezeka ndani ya miaka 54 ya Uhuru (kilomita za mraba 40,000).

“Hali hii italifanya shirika kuwa na jumla ya hifadhi za Taifa 22 zenye eneo la kilomita za mraba 104,000, ikiwa ni ongezeko la hifadhi 6 katika kipindi cha miaka minne,” alisema.

Kiuhifadhi, Kijazi alisema nchi yetu ni tajiri kwa mifumo ya ikolojia ya asili, lakini mifumo hiyo imekuwa ikiathirika kutokana na shughuli za kibinadamu.

Kutokana na umuhimu wa shughuli za maendeleo, Kamishna huyo alisema lazima shughuli hizo ziendelee, lakini kuna umuhimu wa kuwa na maeneo ya kutosha kuwezesha mifumo ya asilia ya kiikolojia ambayo itaendelea kuyafanya mazingira ya binadamu kiuzalishaji kuwa endelevu.

Alisema kutoweka au kupungua kwa maeneo hayo kwa kiasi kikubwa kutakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi, kwani shughuli kama za kilimo ambacho ndio tegemeo la zaidi ya 80% ya Watanzania, hutegemea uasili wa mazingira, hivyo kuongezeka kwa maeneo haya ni kuweka misingi imara ya uzalishaji, ambayo itachangia kuiondoa nchi kutoka uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati.

Kuhusu ulinzi na usalama wa hifadhi, alisema umeimarika na matukio ya ujangili kupungua kwa zaidi ya asilimia 80, na idadi ya wanyama wahanga wa ujangili, hususani tembo na faru imeongezeka, ambapo faru pekee wameongezeka kwa asilimia 10. Hali hii imechangiwa na kuimarika kwa mifumo ya ulinzi na intelijensia.

Pia katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, shirika limefanikiwa kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia kwenda mfumo wa jeshi usu. Mabadiliko hayo yamelenga katika kuimarisha uzalendo, ukakamavu, utii na mbinu za utendaji kazi ili kukabiliana na vitendo vya ujangili.

Alisema uwepo wa maeneo ya hifadhi pia ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa nchi, ambapo Sekta ya Utali imekuwa mojawapo ya sekta tatu kuu za kiuchumi ikichangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa na 25% ya fedha za kigeni.

Zaidi ya nusu ya wageni wanaotembelea nchini hutembelea hifadhi za Taifa, ambapo jitihahada ambazo zimefanyika kwenye awamu ya nne zimesaidia kuongeza kwa kasi mapato ya shirika, na hivyo kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea.

Akitoa mfano alisema, katika mwaka wa fedha 2015/2016, shirika lilikusanya Sh bilioni 175.1 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka wa fedha 2017/18, ambapo shirika lilikusanya Sh bilioni 279.4, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh bilioni 100. Ongezeko hilo limetokana na juhudi mbalimbali.

Juhudi hizo ni pamoja kujitangaza kwenye masoko mapya na ya zamani, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, kupunguza tatizo la uhaba wa malazi ya watalii kwa kuwavutia wawekezaji wa ndani kuwekeza katika eneo hilo.

Juhudi hizo zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya vitanda kutoka 2,400 hadi 5,829 kwa wageni wa nje, na kutoka vitanda 3,601 hadi 4,970 kwa wageni wa ndani.

Katika kuvutia watalii wengi zaidi, shirika linaelekea kuboresha zaidi huduma kwa kutumia mfumo wa mfumo wa uendeshaji wa viwango vya kimataifa (ISO 9001:2015 Quality Management System).

Pia kuongezeka kwa mapato ya moja kwa moja kumechangia kulifanya Shirika lisimamie kikamilifu majukumu yake, hivyo kupunguza utegemezi wa wafadhili.

Lakini pia kuongeza gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kutoka Sh bilioni 3.5 mwaka 2015/2016 hadi Sh bilioni 42 mwaka 2018/2019.

Kamishna Kijazi alisema katika kuimarisha uhusiano na jamii kupitia programu za Ujirani Mwema, shirika limetumia zaidi ya Sh bilioni 20 kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuimarisha huduma za afya, elimu na vikundi maalum.

Katika maeneo yanayozunguka hifadhi shirika limetumia zaidi ya Sh bilioni 5 kusaidia vikundi mbalimbali vya uzalishaji na ujasiriamali katika maeneo hayo.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, asilimia 90 ya migogoro baina ya shirika na jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi za Taifa imepatiwa ufumbuzi.

Aidha, shirika kwa kushirikiana na mamlaka husika linaendelea na utekelezaji wa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi (Land Use Plans) katika vijiji hivyo kwa lengo la kuongeza tija katika maeneo hayo, kwa lengo la kudhibiti migogoro isijitokeze tena.

Pia mwamko wa utalii wa ndani umeongezeka sana kutokana na juhudi mbalimbali za kutangaza vivutio, hususani baada ya uanzishwaji wa Safari Channel ambayo shirika limeshirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na asasi nyingine chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuianzisha.

Mwisho.