Home Habari Hii ndiyo Jamafest iliyotikisa tasnia ya burudani

Hii ndiyo Jamafest iliyotikisa tasnia ya burudani

663
0
SHARE

JEREMIAH ERNEST

TAMASHA la Jamafest lilianzishwa mwaka 2013 kwa lengo lilikuwa ni kukuza utamaduni, biashara na ujasiriamali wa nchi za zilizopo katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ni tamasha linalofanyika kila baada ya miaka mbili mfululizo, likienda kwa zamu katika mataifa ya Uganda, Burundi, Rwanda, Kenya, sfari hii likitua kwenye anga za burudani nchini.

Kwa mara ya kwanza, Jamafest lilifanyika Rwanda mwaka 2013, kabla ya kupelekwa Kenya (2015) na Uganda (2017).

Msimu huu wa nne wa tamasha hili ulianza kurindima katika Viwanja vya Uhuru kuanzia Septemba 22, mwaka huu, kwa matembezi ya utamaduni yaliyoanzia Tandika, Temeke, Dar es Salaam, yakihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi rasmi, akiambatana na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Siku hiyo, vikundi vya ngoma za asili takribani vitano vilionesha utamaduni wao kulingana na mila na desturi za kila nchi.

Wasanii wa muziki Tanzania kwa kushirikiana na kamati ya maandalizi ya tamasha hilo walijitolea kutunga wimbo wa Jamafest kuhamasisha utamaduni na umoja wa nchi za Afrika Mashariki, pia wakizindua video ambayo inapatika katika mitandao ya kijamii.

Wimbo huo uliotungwa na Peter Msechu ulitumbwizwa na wasanii wakongwe- Khadija Kopa, Barnaba Elias, Linna Sanga, Mimi Mars na Msami, ambaye ndiye aliyefundisha miondoko ya kucheza.

Katika tamasha hilo, kuna mabanda maalumu ya maonesho ya mavazi, filamu na vitu mbalimbali kutoka katika nchi za Afrika Mashariki, ambapo mgeni rasmi alipata nafasi ya kutembelea.

Tamasha hilo la siku saba katika viwanja vya Uhuru, licha ya burudani, pia kumekuwapo na fursa ya kuuza na kununua bidhaa kutoka katika nchi wanachama.

Katika hotuba yake, Mh. Samia Suluhu alisema tamasha hilo ni chachu ya ushirikiano wa kuendeleza utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki. Kutokana na hilo, aliongeza kuwa walioasisi Jamafest wanapaswa kupongezwa.

Alisema ni fahari kwa Tanzania kupewa jukumu la kufanya tamasha kubwa kwa sababu imeonekana kuwa ni nchi ya amani na upendo, tena inayopenda wageni, hivyo si mbaya endapo itaendelea kupokea matamasha ya aina hiyo.

“Kila mtu anatakiwa kupenda na kuenzi utamaduni wake na kuacha kuiga utamaduni wa wengine. Kuiga kunasababisha kusahau utamaduni wa nchi, hasa katika mambo muhimu, ikiwamo michezo ya jadi,” alisema.

Alisema kila Mtanzania kupitia tamasha hilo anatakiwa kutumia fursa ya kujifunza maarifa na mbinu mbalimbali kutoka kwa wageni, ambazo zitamsaidia kuimarisha utamaduni.

Wakati huo huo, alisisitiza kuwa watoto wanacheza michezo mingi kwenye simu na wanashindwa kucheza michezo ya jadi. “Watoto wengi wamezama kwenye simu na kusahau michezo ya jadi. Hivyo, viongozi na wataalamu wanatakiwa hukakikisha katika shule zetu watoto wanacheza michezo ya jadi, bila kufanya hivyo itapotea na sisi tutakuwa tumebaki na tamaduni za kuiga,” alisema.


Lakini pia, aliona umuhimu wa matamasha ya aina hii kuwa fursa kwa viongozi wa Afrika Mashariki kujadiliana namna ya kuuendeleza na kudumusha utamaduni wa nchi za Afrika.

“Kwa miaka 10 sasa, sanaa za mikono zimeendelea kufanya vizuri katika nchi za nje, hivyo ni fursa kwa vijana kupata ajira katika nchi mbalimbali duniani,” alisema mama Samia.

Tamasha hilo la Jamafest linatarajiwa kufikia ukomo wake Jumamosi ya wiki hii katika Viwanja vya Uhuru jijini Dar es Salaam.