Home Michezo Hii ndiyo Yanga inayosubiriwa baada ya Uchaguzi

Hii ndiyo Yanga inayosubiriwa baada ya Uchaguzi

2440
0
SHARE

ZAINAB IDDY

MWISHONI mwa wiki hii, klabu ya Yanga itafanya Uchaguzi Mkuu baada ya kumalizika kwa mvutano wa muda mrefu kati ya wanachama, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali.

Pande tatu hizo zilikuwa na mvutano uliokwamisha uchaguzi kufanyika kwa zaidi ya mara tatu kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji.

Mvutano huo ulihitimishwa baada ya makubaliano ya kusitishwa kwa zoezi la chaguzi zote za awali zilizokuwa zikipingwa na mchakato kuanza upya na sasa Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumapili ya wiki hii.

Mchakato wa uchaguzi ulipokubaliwa na pande zote tatu kwa sasa umefikia hatua ya wagombea kuzinadi sera zao, zoezi lilioanza Aprili 30, huku likitarajiwa kufikia tamati Mei 4.

Aidha, ukweli usio na shaka ni kwamba Uchaguzi huu ni muhimu kwa mustakabali wa klabu ya Yanga kwani ndio utakaoijenga upya baada ya kupitia misukosuko mingi katika wiki za hivi karibuni.

Tangu kutangaza kujiuzulu kwa Manji Mei 23 , mwaja juzi, Yanga imekuwa ikipita katika kipindi kigumu, kiasi cha kupoteza ushindani na hamasa ya mashabiki wake.

Lakini je, ipi taswira mpya ya Yanga baada ya Uchaguzi Mkuu? Nini mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanakiratajia mbele ya uongozi utakaoingia madarakani?

Kwa zaidi ya miaka 80, ni aibu kuiona Yanga ikishindwa kumiliki uwanja wake wa mechi au walau wa mazoezi, licha ya kuwa na jina kubwa katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Hivyo basi, ni wakati sasa na jukumu la viongozi wapya kuiwezesha Yanga kumiliki uwanja wake. Kama zilivyo klabu zingine, nikiitolea mfano Azam FC, uwanja unahitaji kuwa na hosteli za kisasa kwa ajili ya wachezaji na benchi la ufundi. Lakini pia, unapaswa kuwa na sehemu ya mazoezi ‘gym’, bwawa kubwa la kuogelea na sehemu ya kupumzika.

Pili, uongozi mpya una jukumu zito katika kusimamia soka la vijana. Moja ya sifa za kujiita timu kubwa ni kuwa na kikosi imara cha vijana, ambacho muda wowote kitakuwa tayari kuvaa viatu  vya kaka zao, hasa pale ratiba inapokuwa ngumu.

Ni kwamba umefika wakati kwa viongozi watakaoingia madarakani kuwa na mchakato wa kukuza soka la vijana kuanzia umri wa chini ya miaka nane kwani si tu kukipa nguvu kikosi cha kwanza, pia hiyo itaifanya klabu iachane na utamaduni wa kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji.

Aidha, kwa kuwa na mpango wa kuwaandalia mazingira mazuri wachezaji chipukizi, huo utakuwa mradi kwa klabu, ambapo itakuwa ikiingiza fedha endapo itaamua kuwauza kwingineko.

Tatu, lipo la utumizi sahihi ya nembo kwa masilahi ya klabu. Ukweli ni kwamba kwa miaka mingi, si Yanga tu, timu nyingi za Tanzania zimeshindwa kulidhibiti kundi la wajanja wachache ambao wamekuwa wanufaikaji wakubwa wa rasimali zenye nembo zake.

Mfano, wamekuwa wakitumia nembo kutengeneza jezi au kofia ambazo haziziingizii kiasi chochote cha fedha timu hizo. Ni kwa mantiki hiyo basi, viongozi watakaoingia madarakani watatakiwa kusimama kidete kulizuia hilio.

Yaani, kuweka mikakati ya kisasa, ambayo itaifanya nembo ya Yanga, kama ilivyo duniani kote, kuwa chanzo cha mapato kwa klabu. Tofauti na sasa inavyofanywa na ‘wapigaji’, klabu inatakiwa kuwa msimamizi mkuu wa biashara ya kutengeneza vifaa mbalimbali kama fulana, kofia, vishika ufunguo n.k.

Nne, uongozi wa Yanga utawajibika na hili la timu hiyo kushindwa kutamba kimataifa kwa miaka sasa. Katika hilo, Wanajangwani wanatakiwa kujifunza kwa wenzao wa Msimbazi, Simba SC, ambao baada ya ujio wa uongozi wa sasa, waliweza kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara kwanza tangu mwaka 1993.

Simba ikiwa mfano mzuri kwa bajeti yao ya kikosi hiki inayotajwa kuzidi Sh bilioni m0ja, lazima uongozi mpya uwe na uhakika wa uwekezaji mkubwa, ambao utaihakikishia Yanga nafasi ya kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, mashindano ambayo ni muda mrefu sasa, yamebaki kuwa ‘pasua kichwa’ kwa Wanajangwani hao.

Bila shaka mashabiki na wanachama wa Yanga watakumbuka kuwa wakati Manji akiwa Mwenyekiti, timu yao iliweza kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kipindi hicho ikiwa chini ya kocha wao raia wa Uholanzi, Hans van der Pluijm.

Si tu ni kutokana na ubora wa kikosi cha Yanga kipindi hicho, ikiwa na safu kali ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na Amis Tambwe na Obrey Chirwa, bali pia hali ya kiuchumi klabuni hapo ilikuwa poa kutokana na mkwanja wa Manji.

Kwa mantiki hiyo basi, uchaguzi wa mwishoni mwa wiki hii unatakiwa kuipa Yanga viongozi wenye mikakati thabiti ya kuifanya timu hiyo isiyumbe linapokuja suala la fedha.