Home Makala Hii ni kwa viongozi wenye hofu na ‘maneno ya pembeni’

Hii ni kwa viongozi wenye hofu na ‘maneno ya pembeni’

1198
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA

WAKATI wa uhai wake, aliyekuwa Mkurugenzi wa uzalishaji wa vipindi wa Clouds Media, marehemu Ruge Mutahaba alipata kunena, “Usihofie maneno ya watu wanaokusema vibaya pembeni.Kumbuka wapo pembeni,”

Aghalabu maneno hayana sababu za kucuambuliwa zaidi, kwani yanajieleza kibanagaubaga. Katika kmaisha yetu wanadamu au viongozi, kwenye mihangaiko yetu tunakutana na changamoto nyingi mno. 

Miongoni mwa changamoto hizo ni kusemwa vibaya na baadhi ya watu tunaofahamiana nao au wanaokerwa na mihangaiko yetu ya kutafuta mlo wa siku. 

Mathalani ukiwa kiongozi hakuna mtu anayeacha kukukosoa. Ukiwa kiongozi haiwezekani kukosekana wakokosoaji. Wakosoaji wengine kila kukicha huwa wanatafuta udhaifu au namna yoyote ili ili wakuseme vibaya. 

Watu wa aina hiyo watakosoa maamuzi yako na hata yale yaliyomo kwenye mamlaka yako. Wakosoaji hao wanarusha vijembe na kejeli,watatoa kila aina ya ‘povu’ kama wasemavyo vijana wa mjini wakiwa na lengo la kuonesha juhudi zako katika kuwatumikia au kujiletea maendeleo binafsi kuwa ni bure. 

Wao wanachoona ni mtazamo hasi kwa kila unachokifanya madarakani ukwia kiongozi au kwenye maisha yako kama wanadamu wengine. 

Si wakosoaji pekee, bali hata wale ambao wanakuunga mkono kuna wakati wanalazimika kukutetea kiongozi kwa imani kuwa hustahili kukosolewa,kusemwa vibaya,kunangwa, kurushiwa vijembe na kadhalika.

Yumkini sifa za kiongozi wa ngazi yoyote ni pamoja na kutambua na kuwafanya watu anaowaongoza kuwa washiriki wa michakato na mipango ya maendeleo katika eneo lake, kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata, tarafa, Wilaya, Mkoa, Kanda na taifa. Ili kukamilisha dhana nzima ya maendeleo.

Msingi wa kwanza wa kukamilisha maendeleo katika nchi yoyote ni pamoja na kuruhusu wakosoaji hao waliopo pembeni na mijadala kutamalaki ili kusherehesha uhuru wa mawaidha yetu kwenye taifa.

Ikumkbukwe mijadala ni sehemu ya kukua kwa jamii yoyote. Mijadala ni sehemu ya kukuza upeo wa mwanafunzi, mfanyakazi (mtumishi),kiongozi kuanzia sekondari, vyuoni,maofisini, mitaani na uongozini. Hata mwendesha Guta, bodaboda, Bajaji, Boti na mtumbwi wanakuwa na mijadala kuhusiana na eneo lao la kazi pamoja na uongozi wa kaya, kijiji, Kata,Tarafa, wilaya, mkoa na taifa lao kw aujumla.  

Kimsingi mijadala uwe unapenda ua hupendi ndio msingi wa jamii yoyote kukua, kuendelea, kupevuka na kupata maarifa. Tunaandikiwa vitabu ili kupata maarifa, kuburudika na kukamilisha mchakato wa maisha duniani. Tunashudia mijadala kwenye runinga,vitabuni,tafiti na mengineyo kwa sababu ndiyo msingi wa kukua kwa jamii. 

Kiongozi, hotuba yako lazima ijaliwe kwa njia hasi na chanya. Kuwa kwenye kundi hasi haina maana kuwa huwezi kuwa chanya wala kuwa chanya haina maana huwezi kuwa hasi. Ni uhuru binafsi. 

Kiongozi, kama hutaki hotuba zako zijadiliwe, acha kuzitoa basi ili uishi kwa amani. Kiongozi thabiti hatishwi na ‘maneno ya pembeni’. Kamwe hakimu au jaji katika Mahakama yoyote hatoi hukumu ya kesi eti kwakuwa wananchi wamejadili mno mitaani, bali misingi ya sheria ndiyo inayoongoza kutamatisha kesi. Haiwezekani ‘maneno ya pembeni’ kufanywa msingi wa kuhukumu kesi au uongozi.

Ukitaka watu wakuunge mkono wafanye watende kwa hiari yao. Kiongozi jenga hoja zako, fanya vitu vyenye mantiki, waachie uhuru wao wa kuamua. Hakuna sheria inayomshurutisha mtu au watu kuunga mkono jitihada fulani bali ni uhuru binafsi.

Aghalabu baadhi yetu tumekuwa waumini wa kushindanisha mawazo. Mawazo ambayo yanakusudia kujenga jamii. Kwa wenye wazo kila mmoja anayo haki ya kutoa kwa jamii, iwe unapenda au hupendi. 

Kumbuka wale ambao unawahutubia ni watu wazima. Wana akili timamu na wanayo haki ya kuamua kukukisiliza au kuacha. Wanayo haki ya kuchambua na kujadili kile unachowaambia. Wanayo haki ya kutoa maoni yao dhidi ya kile ulichowashawishi au kuwaeleza.

Watu wazima wanafikiria, wanachakata mawaidha na kutoa uhuru wa wengine kufikiri. Sio mazumbukuku. Haiwezekani maoni ya wasikilizaji yakamkosesha mpangilio mtangazaji. Maneno ya pembeni yakigeuzwa kuwa nongwa tunaunda uongozi unaotamani shari na kuumiza nyoyo za watu kwa madai ‘kuchapa kazi’.

Wajibu wa ubongo ni kufikiri. Kufikiri ni sehemu ya kuchapa kazi kwa kushirikisha ubongo. Wananchi si watoto ambao unadhani kwamba ukiwadanganya kuwaletea pipi watanyamaza au kuacha kufikiri. 

Wananchi wana haki zote za kujadili hali nzuri au mbaya ya nchi yao. Ni haki yao. Ni wajibu wao. Ni jukumu lao, iwe kiongozi unataka au hutaki. Unatakiwa kufanya kitu cha kuwafanya wakukubali, wakupende, wakuzimikie, wakuhusudu na kukuthamini. 

Kamwe wananchi hawawezi kumpenda kiongozi ambaye anahangaika kuwakomesha au kuwafanya wakose amani. Kwa wenye hasira na dhaifu wanaogopa mijadala. Kwa viongozi dhaifu wanadhani kuwa kutoungwa mkono ni uhaini. Ni jambo la ajabu kwa kiongozi au mwanadamu kuogopeshwa na maneno ya pembeni. 

Uongozi sio kuviziana kutunishia kwapa na misuli ya miili bali misuli ya akili na ushawishi. Pia uongozi kuelekeza,kuendesha na kukumbushana na kujaliana. Waache wananchi wakupende wala usiwalazimishe. 

Hasara ya kuogopa mijadala katika taifa ni kujikusanyia kundi kubwa la watu, wafuasi na wasaidizi wako ambao  wanajipendekeza na kushindwa kuwa huru kimawazo na kihulka. Nawatakieni wakati mwema viongozi wasiogopa ‘maneno ya pembeni.