Home KIMATAIFA Hiki ndicho kilichomkuta Mutharika bungeni

Hiki ndicho kilichomkuta Mutharika bungeni

1181
0
SHARE

*Upinzani walazimika kugomea hotuba yake, kwa kutotambua ushindi wake

ANDREW MSECHU na MASHIRIKA

WABUNGE wa upinzani nchini Malawi wametoka nje ya Bunge Ijumaa iliyopita, baada ya Rais Peter Mutharika kuanza kutoa hotuba yake kwa taifa.

Wapinzani walikuwa wakionesha kutokubaliana na Rais na matokeo ya uchaguzi wa Mei 21, ambao walisema Mutharika alishinda kwa udanganyifu.

Katika matokeo hayo ya uchaguzi, Mutharika alitangazwa mshindi kwa asilimia 39 ya kura wakati aliyekuwa mgombea wa upinzani, Lazarus Chakwera alitangazwa kuwa mshundu wa pili kwa asilimia 35 ya kura, hivyo kupishana kwa asilimia nne tu ya kura.

Wabunge wa upinzani, hasa kutoka Chama cha Congress cha Malawi au MCP, waliendelea kupiga kelele kila wakati Mutharika alipokuwa akijaribu kutoa hotuba yake, hivyo kuzuia mtiririko wa shughuli za Bunge kwa takribani dakika 30.

Hatua hiyo ilimlazimisha msemaji wa Bunge, Catherine Gotani Hara, kuwaagiza wabunge wote waliokuwa wakiongoza kelele hizo kutoka nje ya Bunge, lakini wabunge hao kutoka MCP waliamua kutoka kwa pamoja bungeni ili kuonesha ushirikiano na wabunge wenzao.

“Tulichofanya katika bunge leo ni tu kukubaliana na kile kiongozi wa MCP, Dk Lazarus Chakwera alichosema kwamba hatambui utrais wa Mutharika nchini. Sisi hatukubali matokeo ambayo yalitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Malawi,” alisema Eisenhower Mkaka, Katibu Mkuu wa MCP

Wapinzani hao walidai kuwa chama tawala cha Democratic Progressive (DPP) kilivuruga natokeo ya kura kwa kusaidiana na Tume ya Uchaguzi iliyochaguliwa na Rais. Wote; DPP na tume zinakataa mashtaka.

Alipopata fursa ya kutroa hotuba yake baada ya kutoka kwa wabunge wa upinzani, Mutharika alisema Serikali yake itapambana kuzuia na kudhibiti rushwa, ambayo alisema imeenea kwenye maeneo yote ya nchi.

Aliahidi hukumu kali kwa wale watakaotiwa hatiani kwa makosa ya rushwa au uhalifu wa kiuchumi, pamoja na kuanzishwa kwa “mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za rushwa.”

Mnadhimi Mkuu wa Serikali bungeni,  Kondwani Nankhumwa, alisema kuwa mwenendo wa wawakilishi wa upinzani haukuwa tu bahati mbaya, lakini pia ni aibu kwa taifa hilo.

Alisema Bunge liliweka utaratibu wa kuchukua hatua kwa ajili ya kudhibiti wabunge wanaotekeleza vurugu bungeni.

Lakini Katibu wa MCP, Mkaka Mkaka alisema watunga sheria hao katika Bunge la Malawi wataendelea kususia Bunge kila Mutharika atakapoingia kwenye ukumbi wa Bunge hilo.

“Bila shaka tutarudi bungeni, tunachotaka ni kupitisha bajeti maalumu kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii. Hatutaki kuharibiwa kwa huduma za jamii,” alisema Mkaka.

AAHIDI KUINUA UCHUMI

Kwa mujibu wa Rais Mutharika, anatarajia uchumi utaongezeka kwa asilimia tano mwaka 2019, jambo ambalo aliahidi Ijumaa wiki iliyopita, katika hotuba yake kwa taifa iliyopingwa vikali na MCP.

Mutharika alitoa ahadi hiyo huku wabunge wa upinzani wakimzomea na kutoka nje ya Bunge kupinga hotuba yake, wafuasi wa upinzani pia walichoma matairi mitaani na kurushia mawe magari ya askari polisi, waliokuwa wamezingira Mahakama ya Katiba, ambayo ilitoa uamuzi kuwa mgogoro wa uchaguzi utaweza tu kuamuliwa iwapo utafikishwa kupitia mahakama ya chini yake.

Kutokana na vurugu za wafuasi hao, askari waliokuwa na silaha walielekezwa kuzingira eneo hilo la mahakama, ili kuwadhibiti.

Akizungumza na wabunge kutoka chama chake pamoja na wachache wa kujitegemea, Mutharika alishutumu upinzani akidai kuwa wamekuwa wakijaribu kuyumbisha uchumi na kuhusisha wanajeshi wasio rasmi kueneza machafuko.

Katika uchumi, aliahidi kuendelea na juhudi za kushusha mfumuko wa bei na kushusha viwango vya riba, pia kufuata masharti ya sera kwa mkopo wa Dola milioni 112 unaodaiwa na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) .

Mutharika, mwenye umri wa miaka 78, aliyekuwa profesa wa sheria, aliongoza maboresho ya miundombinu na kushuka kwa mfumuko wa bei wakati wa miaka mitano ya kwanza, lakini wakosoaji wanamshutumi kwa rushwa, ubadhirifu na udanganyifu.

Alisema ukuaji wa uchumi wa mwaka huu kwa asilimia tano, kutoka iliyokuwa asilimia nne  mwaka 2018, utaendeshwa na kukua kwa uzalishaji wa kilimo, na kuungwa mkono na madini, ICT na huduma za kifedha.

Taifa hilo ndogo, lililo katika mazingira ya kutokuwa na bandari inayopakana na bahari lina idadi ya zaidi ya watu milioni 20, ambalo lilipata uhuru kutoka Uingereza mwaka wa 1964.

Baada ya kipindi cha awali cha utulivu wa kiuchumi na kijamii, sasa ni kati ya nchi zilizo masikini zaidi duniani, ikitegemea fedha za wafadhili na mauzo ya tumbaku na chai. Malawi pia inakabiliwa na ukosefu wa ajira kwa kiwango cha juu.

Nina “huruma” na wanaoshindwa uchaguzi.

Wakati wa kuandaa chakula cha mchana kwa wajumbe wapya wa Bunge katika Kasri ya Kamuzu huko Lilongwe, Rais Mutharika alisema alielewa uchungu wa wale wanaojitahidi wanaopinga ushindi wake, akisema kupoteza uchaguzi ni jambo la kusikitisha, tena linaloumiza.

“Asante Mungu. Sijawahi kupoteza uchaguzi. Lakini najua kuwa kupoteza uchaguzi kunaweza kuwa jambo lenye uchungu sana, hasa wakati mtu anapokuwa na matarajio yasiyo ya kweli,” alisema Mutharika.

Mutharika pia alielezea haja ya amani na umoja wa taifa, akisema licha ya tofauti za kisiasa, nchi ina watu wamoja ambao wanashirikisha na wanafaidika na rasilimali zao.

“Kampeni imekwisha. Mbio zimekwisha. Hebu tuendelee. Pamoja na siasa, sisi ni familia moja na tunashiriki nyumba moja. Tunatumia barabara sawa na kushiriki rasilimali hizo,” alielezea Mutharika.

Rais huyo alisema pia kuwa ni muhimu kwa waungwana kuungana na kushirikiana, akisema wale walioshiriki wakati wa chakula cha jioni baada ya hotuba yake bungeni ambayo ilisusiwa na wapinzani walishiriki zawadi ya thamani ya maisha.

Chama cha Congress cha Malawi na chama cha United Transformation Movement vimedai vitaendelea kupinga ushindi wa Mutharika mahakamani.