Home Makala Hili halikubaliki maduka ya vyakula

Hili halikubaliki maduka ya vyakula

2059
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI

KWA kumbukumbu zangu, ni kitambo sasa tangu nilipoanza kuona wafanyabiashara wa maduka ya vyakula wakiwa na utamaduni wa kutumia paka katika ulinzi wa bidhaa zao dhidi ya panya. Sina shaka kuwa nitaendelea kuuona kisha kuuacha kwa vizazi vijavyo.

Hata msomaji wangu wa ‘Macho Yameona’ unaweza kuwa shuhuda mzuri katika hili, kwamba aghalabu maduka ya vyakula yamekuwa yakienda sambamba na ufugaji wa paka.

Sioni haja ya kuishusha orodha ndefu ya hasara za panya anapokuwa dukani na ni kwa maana hiyo basi si rahisi kupuuza umuhimu wa paka kwa wafanyabiashara katika kukabiliana nao.

Lakini je, ni kwa namna gani afya ya mtumiaji/mteja inaweza kuhakikishiwa usalama? Hilo ndilo swali la msingi katika hoja yangu hii ya kuzitaka mamlaka husika ziuangaliwe kwa jicho la tatu utamaduni huu.

Kwa kuwa imekuwa ni kawaida na hakuna anayehoji wala kuonesha jitihada za kuchukua hatua, itoshe kujiridhisha kuwa uwepo wa paka pale kwa ‘Mangi’ ni salama kwa afya zetu? Jibu sahihi ni hapana.

Mbaya zaidi, ikiwa si hivyo nikosolewe, wafanyabiashara wenyewe wamekuwa na umakini mdogo katika kuwadhibiti wanyama hao, achilia mbali kuwahudumia, jambo linalochochea zaidi hisia za shaka.

Kulifafanua hilo, si ajabu kwenda dukani na kukuta paka akiwa juu ya kiroba cha unga au mchele, huku mfanyabiashara akiendelea na kazi zake bila hofu yoyote. Ni kusema kuwa, ndani ya duka hakuna mpaka kati ya paka na eneo ziliko bidhaa.

Je, vipi kuhusu manyoya yanayochomoka kutoka katika miili ya wanyama hao na kuzifikia bidhaa kama mafuta ya kula? Labda tunatakiwa kujiuliza na kisha jibu liambatane na hatua stahiki.

Lakini pia, mara kadhaa wafanyabiashara hao wamekuwa wakijisahau, ambapo haishangazi tena kukuta wakiwashika na hata kuwabeba paka wao na kisha kuendelea kutoa huduma kama kawaida.

Huenda tunaishia kwa mazoea na kisha mazoea yanatujenga kiasi kwamba tumefikia hatua ya kucheza na afya zetu. Ndiyo, mfanyabiashara amesahau kuwa kucheza kwake na manyoya ya paka hatari kwa afya za wateja na yake pia!

Tumejiuliza juu ya afya za paka hao, ambao hata kwa macho tu, wengi wao huonekana dhaifu? Ni kila baada ya muda gani wafanyabiashara wamekuwa na kawaida ya kuwapa huduma za afya wanyama hao ili kujiridhisha kuwa uwepo wao dukani ni salama kwa bidhaa zilizopo?

Hata hivyo, kwa mazingira hayo tu, ni kwa utafiti gani wa kitaalamu unaweza kuondoa shaka kuwa afya ya mlaji iko hatarini?

Kama nilivyokiri hapo awali, hakuna anayeweza kukataa faida kubwa ya paka anapokuwa dukani, lakini je, kama unahatarisha afya ya mlaji, kuna umuhimu gani wa kuendelea kuwapo?

Hakika juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa, nikitamani kuona zikianzia katika ngazi za chini, kwa maana ya kila mmoja kuondokana na utamaduni wa kuishi kwa mazoea, kabla ya kuzifikia mamlaka husika.