Home Makala Hivi ndivyo utwala wa kikoloni ulivyokuwa

Hivi ndivyo utwala wa kikoloni ulivyokuwa

2299
0
SHARE

>>Naukumbuka mkono na Gavana Twining

NA HILAL K SUED

Ni wananchi wachache walio hai, ambao walipata nafasi ya kuushuhudia utawala wa kikoloni katika nchi hii.

Hapa nasemea wananchi wote ambao walikuwa na umri wa kiasi cha kukumbuka siku ya uhuru Desemba 9 1961 – yaani wale ambao siku hiyo waliokuwa na umri kati miaka angalau 12 na kwenda juu (yaani sasa hivi wenye umri wa miaka 70 na kwenda juu). Hawa nadhani idadi yao haizidi asilimia 10 au chini – yaani chini ya watu milioni 5.

 Madhumuni ya makala hii ni kueleza, ingawa kwa kifupi tu ukoloni ulikuwaje, kadri jinsi nilivyokuwa naufahamu na nilivyokuwa nikihadithiwa na wakubwa. Ingawa maeneo ya vijijini watawala wa kikoloni, yaani Wazungu wa Uingereza hawakuwa wanaonekana sana, lakini mimi nilikuwa na bahati ya kuwaona kutokana na kusoma kwangu, hasa katika Shule za Kati (Middle Schools) ambazo nyingi zilikuwa katika makao makuu za wilaya.

Napenda kwa ufupi tu nisimulie tukio moja ambalo liliniwezesha kupeana mkono na “Mkoloni na 1” hapa nchini – Gavana wa Uingereza Sir Edward Twining mwaka 1958 nikiwa Darasa la Nne.

Shule ya msingi niliyokuwa nikisoma ilikuwa katika kijiji ambacho kilikuwa katika barabara kati ya Sumbawanga na Abercorn (sasa Mbale) mji karibu na mpaka wa Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia) nchi ambayo pia ilikuwa ni koloni la Uingereza.

Pamoja na kwamba ni mzaliwa wa wialaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora elimu yangu ya msingi niliipata wilaya ya Sumbawanga ambayo ilikuwa katika Jimbo la Mgharabi lililojumuisha mikoa ya sasa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.

Katika bendi ya shule (school band) mimi nilikuwa ni kiongozi yaani band master na headteacher wetu alitutangazia kwamba siku inayofuata asubuhi tutakwenda kumpokea Gavana Sir Edward Twining akipita kwenda Abercorn akitokea Sumbawanga. Bila shaka Gavana huyu alikuwa anamtembelea mwenzake wa Rhodesia ya Kaskazini.

Iliamuliwa kwamba wanafunzi wa darasa la tatu na la nne tu ndiyo watahusika na hivyo tuliambiwa tuvae sare safi siku inayofuata na tuwahi shuleni hapo asubuhi kabla ya saa moja.

Asubuhi tulikusanyika shuleni pale na kujipanga katika mstari na tukaondoka kuelekea barabara ya Sumbawanga atakakotokea mgeni. Umbali wa kama maili mbili hivi (kilomita 3) tukaamrishwa kusimama na kuambiwa tupumzike kando ya barabara.

Ilipotimia mishale ya saa tano hivi tukasikia mngurumo wa gari (kwani kulikuwa hakuna mawasiliano mengine) na tukaamrishwa na walimu wetu kusimama mistariini haraka haraka huku bendi ya shule ikiwa mbele nami kiongozi wake mbele kabisa na kifimbo changu. Pembeni kwa nyuma yangu alisimama mwanafuni mwingine ameshika bendera ya Uingreza (Union Jack) iliyowekwa kwenye mti mrefu.

Gari la mbele la msafara huo lilipoanza kutuona tumesimama katikati ya barabara likalegeza mwendo huku dereva wake akiashiria yale ya nyuma nayo kusimama. Yalikuwa kama magari manne tu – la mbele Land Rover ya polisi wa Kiafrika na wakubwa wao wa Wazungu, ikifuatiwa na gari saloon ya gavana mwenyewe na mkewe na nyuma yake gari la maafisa wengine Wazungu. Gari la mwisho pia lilikuwa na walinzi wa Kiafrika na maafisa wao wa Kizungu.

Mara tu magari yaliposimama walinzi wakaruka nje, wale wa Kiafrika walivalia sare za khaki na kofia ndefu nyekundu za aina ya tarabushi. Mmoja akaenda kufungua mlango wa gari la Gavana ambaye aliteremka. Alikuwa amevalia sare nyeupe na kofia iliyowekwa manyoya ya mbuni.

Pale pale nikaamrisha kuimbwa wimbo wa taifa la Uingereza (God Save Our Glorious Queen) kwa tafsiri ya Kiswahili ambayo tulikuwa tumefundishwa na ambayo sasa hivi siikumbuki vizuri. Nilikuwa namuona Gavana amesimama wima pembeni mwa gari lake kwa ukakamavu huku mkono wake wa kulia ukiwa kwenye saluti. Vivyo hivyo kwa wale maafisa wengine na walinzi.

Wimbo ulipoisha Gavana akanisogelea na kunipa mkono, kisha akawapa mikono walimu wetu wawili waliokuwapo. Hakuna neno lililozungumzwa. Baada ya hapo wakaingia ndani ya magari yao, nami nikatoa ishara ya wanafunzi kujiweka pembeni kuwapisha, kisha hao wakaondoka zao.

Labda niongezee tu hapa kwamba tukio hilo lilionyesha kwamba enzi zile Gavana wa kikoloni hakuwa anatembea na misafara mikubwa ya wapambe, magari na kadhalika kama ilivyo sasa kwa wakuu wetu wa nchi.

Wakuu wa Wilaya (ma-DC) na wakuu wao wa utawala (ma-DO – District Officers) walikuwa Wazungu, ingawa katika miaka ya mwishoni ya ukoloni kulikuwapo Waafrika wachache waliokuwa ma-DC na ma-DO. Kwa Kiswahili hawa ma-DO walikuwa wanaitwa Mabwana Shauri kwani pia walikuwa kama mahakimu wa wilaya (District Magistrates). Na vivyo hivyo ilikuwa kwa wakuu wa idara mbali mbali wilayani.

Hali kadhalika ilikuwa vivyo hivyo katika ngazi za majimbo – yaani kwa ma-PC na wasaidizi wao ingawa hakuwahi kuwepo PC Mwafrika. Kitaifa ilikuwa ni Gavana aliyekuwa akimwakilisha Malkia wa Uingereza akisaidiwa na wakuu wa idara mbali mbali ambazo baada ya uhuru hizi zikawa wizara zikiongozwa na mawaziri.

Kama ilivyokuwa katika nchi nyingine nyingi Barani Afrika wakoloni waliwatumia sana watemi wa jadi katika kuimarisha utawala wao. Maeneo ya vijijini utawala wa kikoloni uliwakilishwa na watemi (machifu) katika maeneo mbali mbali na hawa walikuwa chini ya mtemi mkuu. Kwa eneo letu la Tabora (Unyanyembe) mtemi mkuu ulikuwa ni wa ukoo wa Fundikira.

Kuacha mtemi mkuu kulikuwapo watemi wadogowadogo wa maeneo ya vijijni ambao walikuwa wanalipwa mishahara na utawala wa kikoloni na kazi yao kuu ni kuwaunganisha wananchi katika kuitii serikali ya kikoloni. Katika miji kulikuwapo maliwali, ingawa hawa walikuwa ni weateule wa serikali ya kikoloni.

Kusema kweli mengi ya haya yote nilikuja kuyafahamu baadaye lakini wakati huo nilikuwa naamini kwamba uwepo wa watawala wa Wazungu nchini ni kitu cha kawaida tu. Yaani sikujuwa kwamba kutawaliwa ni kitu kibaya.

Ninaweza kusema kwamba wengi wetu wakati huo, hasa wa umri kama niliokuwa nao walikuwa wanalikubali hili – kwamba ni halali yetu kutawaliwa na Wazungu, kwani wao kwanza ni wasomi, waliostaarabika na wenye ujuzi mkubwa wa kutengeneza mambo mengi, kama vile treni, magari, ndege nk. Mwanzoni kabisa nilikuwa nafikiria kwamba hawa Wazungu walitokea (walizaliwa) humu humu nchini ila tu kwa sababu ya rangi yao ndiyo wakaweza kuwa watawala.

Hata zilipoanza harakati za kudai uhuru, mimi sikuelewa maana yake – yaani wananchi Waafrika wanataka kujitawala wenyewe? Haikuingia akilini hata kidogo. Watawezaje kujitawala wakati hawana chochote cha kuwawezesha kufanya hivyo?

Halafu hawa Wazungu wangeweza kweli kuachia nchi na kuviacha vitu vyote walivyoleta na/au kuvijenga kama vile treni, viwanja vya ndege, bandari, simu, majengo ya serikali? Tena kwa bure tu? Kwani haikuingia akilini wananchi Waafrika wangepata wapi pesa za kuvilipia vitu hivyo kwa namna ya kuvinunua.

Nilikuwa na mawazo haya hasa baada ya kusikia wakubwa wakiyazungumza. Aidha hapo (katika miaka ya mwishoni ya 50) nilianza kusikia habari za Julius Nyerere akihamasisha kudai uhuru, nami nilimuona ni kama vile anafanya dhihaka kubwa. Kitu gani alichokuwa nacho cha kumuwezesha kuwaondoa Wazungu? Yumkini akili zake hazikukaa kisawasawa!

Na wakati huo tulikuwa tunapata habari ya vita ya Mau Mau nchini Kenya ambapo wazalendo walikuwa wanapambana na Wazungu ili waondoke. Baba alikuwa na radio (nadhani kati ya mbili au tatu katika kijiji chetu) – radio zile za wakati huo ziko kama sufuria na betri yake ya ukubwa kama tofali.

Kila jioni tukawa tunasikia taarifa ya habari ya radio ya Kenya wakati huo ikiitwa KBS mtangazaji wake maarufu akiwa Stephen Kikumu akitangaza mwenendo wa vita ya Mau Mau nchini Kenya, jinsi wazalendo walivyokuwa wanakamatwa na Wazungu akiwemo kiongozi wao Jomo Kenyatta na mwingine akiitwa Dedan Kimathi. Pia ilinishangaza kusikia kuna wengine katika viongozi hao wa MauMau wakiita Jenerali Tanganyika na Jenerali China!

Nikazidi kujawa na mawazo: Hivi kweli Nyerere na chama chake cha TANU wana majeshi ya kupigana na Wazungu ili waondoke na kuacha vitu vyao vyote walivyovileta na kuvijenga?

Lakini jinsi miaka ilivyokuwa ikienda, ndivyo jinsi nilivyokuwa nikayaelewa mambo haya, hasa habari zilipoanza kutufikia kwamba Uganda pamoja na nchi nyingine za jirani kama vile Congo, Rwanda na Burundi nao pia walikuwa wakidai uhuru.

Mwaka 1960 ikaja Serikali ya Madaraka na baadaye ikatangazwa rasmi kwamba Waingereza wamekubali kutoa uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 1961. Nikaona haya makubwa sasa! Lakini tusubiri. Shauku yangu ilikuwa huu uhuru ungekuja vipi?