Home Makala Hivi ndivyo virusi vya Corona vinavyoitikisa dunia

Hivi ndivyo virusi vya Corona vinavyoitikisa dunia

1254
0
SHARE

Hassan Daudi na Mitandao

UGONHWA utokanao na virusi vya Corona umekuwa gumzo duniani kote kutokana na kasi ya kusambaa kwake, ukianzia China, sasa ukielezwa kuzifia nchi mbalimbali.

Kwa China pekee, tayari watu 4,515 wameripotiwa kuwa na virusi hivyo, huku zaidi ya 100 wakiwa wameshapoteza maisha, kwa mujibu wa kile kilichoripotiwa na Shirika la Utangazaji nchini humo, Xinhua.

Marekani ni moja kati ya nchi zilizoupokea virusi hivyo, ambapo tayari watu watano wameripotiwa kuwa navyo, ikisemekana wapo wengine 26 wanaofanyiwa uchunguzi.

Mbali ya China na Marekani, pia nchi za Uingereza, Thailand, Taiwan, Australia, Singapore, Japan, Korea Kusini, Malaysia, Ufaransa, Canada, Vietnam na Ujerumani zimetajwa kuwa na wagonjwa.

Virusi hivyo pia vimebisha hodi Afrika, ambako mataifa ya Ivory Coast na Kenya yanasemekana kuwa na watu wanaosadikiwa kuwa navyo.

Tayari Serikali ya China imepiga marufuku safari za kuingia au kutoka Wuhan, pia hatua hiyo ikifanywa pia kwa miji mingine 12, kwa mujibu wa gazeti la New York Times.

Huko Taiwan, Serikali ya nchi hiyo nayo imezuia watu wanaotoka katika Jimbo la Hubei, kama zilivyofanya mamlaka za Hong Kong.

Marekani nayo imechukua tahadhari kwa kuweka mitambo ya kubaini waathirika wa virusi hivyo katika viwanja vyake vya ndege.

Virusi vya Corona ni nini?

Ni vizuri vinavyoathiri mfumo wa upumuaji, hivyo kusababisha magonjwa kama nimonia na mafua. Ni virusi maarufu kwa wanyama, mfano mbwa, licha ya kwamba huweza kuhama kutoka kwao na kumdhuru binadamu.

Katika utafiti wa hivi karibuni, wataalamu wa afya walichukua virusi hivyo, maarufu kwa jina la 2019-nCoV, kisha kuvilinganisha na vingine zaidi ya 200 vinavyodhuru wanyama duniani kote.

Ndiyo maana, moja kati ya mikakati ya Serikali ya China kwa sasa ni kupiga marufu uuzaji wa nyama pori madukani na migahawani.

“Tunaishukuru serikali kwa kuanza na hatua hii muhimu,” alisema Christian Walzer, mtaalamu wa Taasisi ya Uhifadhi wa Wanyamapori.

Kwa kile walichokibainika katika utafiti uliochapishwa katika jarida la Medical Virology, kuna uwezekano mkubwa kuwa virusi hivyo vimetokana na nyoka aina mbili wanaopatikana Kusini Mashariki mwa China, ambako ndiko ulikoibuka ugonjwa huo.

Wapo waliohusika kuvisambaza?

Lakini, yapo madai kuwa virusi hivyo vimetengenezwa na binadamu. Kwamba Taasisi inayojishughulisha na masuala ya virusi ya Wuhan ndiyo iliyovitengeneza.

Walioibua madai hayo wanatolea mfano kilichotokea mwaka 2004, ambapo vigogo watano wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha China waliadhibiwa baada ya kubainika kwa kusambaza virusi vya SARS. Ni virusi vilivyoua watu 800 kwa wakati huo.

Hii ya safari hii, inaelezwa kwamba taasisi hiyo imekuwa ikivifuatilia virusi vya Corona kwa miaka mingi katika maabara zake, kwamba huenda imeshindwa kuvizuia, hivyo kutoka nje kama ilivyokuwa kwa vile vya SARS.

Virusi vinaambukizaje?

Ni kweli virusi hivyo huweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Pia, virusi huweza kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.

Je, ni njia zipi zinazoweza kurahisisha kuhama kwa virusi hivyo? Mosi, ni kwa njia ya hewa na hapo ni pale mwathirika anapokooa au kupiga chafya.

Pili, virusi hivyo huhama kwa njia ya kushikana, mathalan mikono, kati ya mwathirika na asiyenavyo, bila kusahau mate.

Mbaya zaidi, mwathirika huweza kuambukiza virusi hivyo, hata kama yeye hatakuwa ameanza kuonesha dalili. Ni kama ilivyotokea kwa kijana wa umri wa miaka 15 huko Wuhan.

Dalili zake ni zipi?

Licha ya kwamba zinaweza kuwa dalili za magonjwa mengine, mwathirika wa virusi vya Corona huwa na homa kali, kikohozi na upumuaji wa shida.

Kwa upande mwingine, kuharisha, kuumwa kichwa, kuvuja makamasi, kupiga chafya na maumivu ya koo ni dalili zingine za mtu mwenye virusi hivyo vya Corona.

Inaelezwa na wataalamu wa afya huko Marekani, kwamba mtu huanza kuhisi dalili hizo kati ya siku mbili hadi 14 baada ya maambukizi.

Vilevile, licha ya kwamba maambukizi ya virusi hayachagui jinsia, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa robo tatu ya waathirika 41 wa awali walikuwa wanaume.

Vipi kuhusu tiba?

Hadi sasa, hakuna tiba ya virusi ya Corona. Hata hivyo, mgonjwa atashauriwa kupata muda wa kupumzika na kutumia njia za kukabiliana na dalili zilizopo.

Mathalan, kuoga maji ya moto inaweza kupunguza kwa kiasi fulani, kama si kuondoa kabisa, maumivu ya koo au kikohozi. Wakati huo huo, kunywa maji mengi kutamsaidia mwathirika wa virusi hivyo anapokuwa anaharisha.

Kwa kuwa hakuna tiba iliyothibitishwa hadi sasa, basi kupona kwa mwathirika kutokana na uimara wa kinga yake ya mwili. Katika hilo, wengi kati ya waliofariki ni wale waliokuwa na ‘afya mgogoro’ kabla ya kupata maambukizi ya virusi hivyo.

Zipo jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Afya ya Taifa ya Marekani juu ya tiba, huku kampuni ya dawa ya Regeneron ikiweka wazi kuwa ni mapema kupata tiba ya virusi hivyo.

Tutarajie madhara zaidi?

Ndiyo. Tayari kuna hofu kuwa virusi hivyo vitasambaa zaidi katika maeneo mengi duniani, licha ya mataifa mbalimbali kuchukua tahadhari, hasa katika viwanja vyake vya ndege.

Lakini pia, tishio jingine ni sifa ya virusi hivyo vya Corona, kwamba huwezi kusambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hata kama mwathirika atakuwa hajaonesha dalili za kuwa navyo.

Ni wazi bado kuna changamoto kubwa ya kukabiliana na kasi ya maambukizi, hasa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Unajikangaje na virusi hivyo?

Kwa wakazi wa China, hasa Wuhan, eneo ambalo virusi hivyo vilianzia, tahadhari ya kwanza ni kuwa mbali na mwathirika. Wakati huo huo, ni kwa kuepuka kusogelea wanyama (hata waliokufa), au nyama ambazo hazijapikwa, mathalan zile zilizo buchani.

Aidha, tahadhari nyingine iliyotolewa ni kuosha mikono kwa sabuni kila baada ya sekunde 20.

Mwathirika anaweza kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi kwa kuchukua hatua zifuatazo; kujitenga na wengine na kuvaa kinyago (mask) ili virusi vishindwe kuhama kwa njia ya hewa endapo utakooa au kupiga chafya.

Juu ya hilo la mask, wataalamu wa afya wanaonya, wakisema si yoyote inaweza kumzuia mvaaji kupata maambukizi ya virusi vya Corona. Hiyo ni kwa sababu zingine, badala ya zilizothibitishwa, hazina uwezo wa kuzuia kwa ukamilifu virusi hivyo.