Home Latest News HIVI TUNAWEZA KUZICHUKIA ILANI ZA VYAMA VYETU?

HIVI TUNAWEZA KUZICHUKIA ILANI ZA VYAMA VYETU?

4763
0
SHARE

Na Markus Mpangala    |    


WANAZUONI wa sayasinsi ya siasa wanatufundisha kuwa siasa ni uchumi; tunazingatia serikali za mitaa, uzalishaji wa wananchi, serikali, falsafa ya ujenzi wa uchumi na taifa linapofanya juhudi kujipatia pato. Tumefunzwa siasa ni jamii; kuzingatia mahusiano kati ya utaifa au taifa, jamii, na wananchi wake. Tumeambiwa siasa ni utamaduni kwamba inahusika kurekebisha mawaidha, fikra, imani, uadilifu na maisha.

Aidha, tumenolewa kuwa siasa ni michezo na burudani au wengine wasemavyo diplomasia ya michezo kama ilivyotokea mwaka huu kati ya mahasimu Korea kaskazini na Korea kusini. Kwamba michezo na burudani inatumiwa kama nyenzo ya kuvutia na kujenga mahusiano mema katika nyanja za diplomasia, kijamii na kisiasa na kuondoa tofauti zote ili kuweka jamii pamoja.

Siasa ni maisha; utekelezaji wa ahadi kwa wananchi au mtu binafsi, kikundi fulani au makundi yanayohitaji kukamilisha masuala mbalimbali ndani ya taifa. Tunaelekezwa kuwa siasa ni vile hata mchezaji anavyompiga chenga mchezaji wa timu pinzani iwe kwenye soka, kikapu, mpira wa pete, mikono na kadhalika.

Kwa mantiki hiyo unapozungumzia siasa inagusa maeneo mengi na sababu zake ni nyingi. Haiwezekani ukachakua sababu moja na kuifanya ndiyo siasa pekee.

Hivyo basi, vyama vya siasa navyo hutakiwa kujihusisha kwenye masuala ya michezo, jamii na kadhalika kama mojawapo ya nyenzo za kisiasa. Ilani za vyama vya siasa nchini kila ninaposoma huwa nacheka peke yangu. Nikiwasikiliza wanasiasa pia huwa nachekeshwa mno. Lakini sasa nimeanza kujiuliza swali hili, hivi inawezekana sisi wananchi tukafika mahali tukazichukia ilani za vyama vyetu pendwa vya siasa? hivi inawezekana mwanasiasa akawa anaichukia ilani ya chama chake anayoinadi au aliyoinadi wakati fulanki? Tazama mifano hii na mwishowe unawezakupata jawabu kwamba tunaweza kuzichukia ilani zetu au la.

“CHADEMA ITAFANYA NINI?

Hiki ni kichwa cha habari cha Ilani ya Chadema kupitia Ilani ya Ukawa ya 2015-2020. Katika ukurasa wa 11. Nanukuu sehemu ya maelezo;-

 • Katiba ya wananchi ni kipaumbele namba moja,
  hivyo serikali ya CHADEMA itaanzisha tena mchakato
  wa katiba uliozingatia maoni ya wananchi. Lengo ni
  kuhakikisha kwamba vifungu vinavyohusu tunu, maadili
  na miiko ya uongozi vinakuwa kwenye katiba mpya ili
  sheria na kanuni mpya ziweze kutungwa na kudhibitiwa
 • Kujenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini
  mchango wake kwa taifa kila siku
 • Kuimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika
  Sekta ya Umma
 • Kuimarisha mchango wa Wataalam katika uendeshaji
  wa nchi
 • Kusimamia ukusanyaji na matumizi mazuri ya kodi na
  mapato ya serikali na kupunguza mzigo wa kodi kwa
  wananchi
 • Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa watumishi wa
  Umma
 • Ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi kwa wafanyakazi
  ili kupunguza ukali wa maisha
 • Kwa mtumishi atakayependa, atalipwa mshahara wa
  mwezi kwa awamu mbili katika mwezi ili kwendana
  na uhalisia wa hali ya maisha na kupunguza kukopa
  kopa kusiko kwa lazima
 • Kudhibiti na kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni
  pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa
  muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku
  matumizi ya magari ya anasa serikalini (mashangingi)
  Kudhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi wa
  madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi yalivyotumika
 • Kuimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za
  serikali na kuweka bayana mikataba yote ya nchi
  ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia
  ili watanzania waweze kuihakiki na Bunge lao liikubali
  kabla ya kupitishwa na serikali
 • Kuzingatia na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari
  kwa kuhakikisha kwamba tunafuta sheria zote ambazo
  zinaingilia uhuru wa vyombo hivyo
 • Kuimarisha serikali za mitaa ili wananchi washiriki
  kikamilifu katika maendeleo yao. (mwisho wa kunukuu).

Hivi ni wenye Ilani hii ndiyo wanaomwita Rais John Magufuli ni dikteta? Ni mambo mangapi Magufuli ameyatekeleza kupitia Ilani hiyo? Ni vyanzo gani vipya vya ukusanyaji kodi vingefanywa na Chadema nje ya vilivyobuniwa sasa?

ACT-WAZALENDO WANGEFANYA NINI?

Kwenye ilani ya chama hiki katika ukurasa wa 21 , unajieleza kama ifuatavyo;-

6.3 Kuimarisha uongozi bora, kupiga vita rushwa na kusafisha uozo ili kudhibiti mapato na matumizi ya serikali kwa kuchukua hatua zifuatazo:

 • Kutekeleza kikamilifu sera ya serikali ya uwazi (Open Government Policy)
 • Kuweka mazingira ya kisheria ili kuimarisha na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari ili viweze kutoa habari za kweli na kwa wakati kwa wananchi kuhusu utendaji wa serikali
 • Kuipa mamlaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mamlaka zaidi ya kukamata na kushtaki watu na taasisi wanaotuhumiwa kwa rushwa
 • Kubadili mfumo wa kisheria kwenye masuala ya rushwa kwa kugeuza uthibitisho wa mali halali kutoka kwa Jamhuri kwenda kwa mtuhumiwa (reverse of burden of proof).
 • Kuliunda upya Jeshi la Polisi ili kuliimarisha kitaalamu na kiweledi na kulinasua na umateka wa kisiasa ambao limo katika utawala wa sasa.
 • Kupiga marufuku mtu yeyote aliyepatikana na hatia ya kula rushwa kufanya kazi na/au biashara katika taasisi ya serikali
 • Kuweka utaratibu wa kisheria utakaohakikisha kwamba makampuni yote yatakayopatikana na hatia ya kutoa na kupokea rushwa mali zao zinataifishwa
 • Kuhuisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuanzia pale iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipoishia
 • Kuibadili Taasisi ya Taaluma ya Mwalimu Nyerere (Kigamboni) kuwa Chuo cha Mafunzo ya Uongozi. Utawekwa utaratibu wa kisheria kuhakikisha kwamba sifa mojawapo ya mtu yeyote anayewania uongozi wa kitaifa/kuanzia ubunge awe amepata mafunzo kutoka katika chuo hiki.
 • Kupanua wigo wa kodi kwa kuhakikisha kila raia mwenye kipato analipa kodi kwa kujaza ‘ tax returns’ kila mwaka na kuweka mfumo Mpya wa kodi za kimataifa kuzuia makampuni ya kimataifa ( MNCs) kumomonyoa wigo wa kodi (Base erosion and profit shifting ). Vile vile maduhuli yote ya Serikali yatakusanywa Kielektroniki na Hati zote za ardhi zitaunganishwa na namba ya mlipa kodi
 • Kupitia upya mikataba ya uwekezaji katika maeneo ya raslimali ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwiano mzuri wa kimapato kati ya serikali na wawekezaji
 • Kuipa uhuru na mamlaka zaidi ya kisheria Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuondoa uingiliwaji na viongozi wa kisiasa ili iweze kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi, (mwisho wa kunukuu).

Tafakari.