Home Uchambuzi Afrika Hizi ndizo njia alizozitumia Rais Biya kung’ang’ania Ikulu

Hizi ndizo njia alizozitumia Rais Biya kung’ang’ania Ikulu

1084
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO

MAPEMA wiki hii, matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Cameroon yalitangazwa, ambapo Rais aliyekuwa madarakani, Paul Biya ndiye aliyeibuka kidedea kwa mara ya nyingine baada ya hapo awali kufanya hivyo katika awamu sita.

Biya, ambaye kwa umri wake wa miaka 85 ndiye rais ‘mzee’ zaidi barani Afrika, alipata ushindi wa kishindo, akijikusanyia asilimia 71.3 ya kura zilizopigwa wiki mbili zilizopita, huku mpinzani wake mkubwa wa chama cha upinzani cha CRM, Maurice Kamto, akiambulia asilimia 14.2 pekee.

Kabla na hata saa chache baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, tayari wapinzani walishaonesha kutokubaliana na namna uchaguzi ulivyoendeshwa,  ikiwamo asilimia kubwa ya vijana kushindwa kwenda katika vituo vya kupiga kura kutokana na vitisho vya jeshi la polisi.

Ifahamike kuwa, kiongozi huyo ni miongoni mwa madikteta wanaotajwa kuwahi kutokea barani Afrika na ushindi wake umemfanya kuwa Rais wa Cameroon kwa miaka 37 sasa, akiwa ndiye rais aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi katika historia ya siasa za Afrika baada ya swahiba wake, Teodoro Obiang Nguema, anayeiongoza Guinea ya Ikweta (39).

Lakini je, ni mbinu gani ambazo Biya, Teodoro Obiang Nguema na madikteta wengine barani Afrika na kwingineko ulimwenguni wamekuwa wakizitumia kung’ang’ania madarakani? Makala haya yanachambua.

‘kubaka’ uhuru wa habari

Madikteta wengi wamekuwa wakifanya hivyo, kuviweka vyombo vya habari katika wakati mgumu, lengo likiwa ni kuvifanya viache ukosoaji dhidi yake.

Wakati huo huo, vile vinavyoonekana kupaza sauti juu ya vitendo vya rushwa na maovu mengine yanayofanywa na Serikali, huishia kufungiwa kwa mujibu wa sheria kandamizi zilizopo.

Kwa upade mwingine, waandishi wake huishi maisha ya hofu kutokana na uwepo wa matukio ya kutekwa na kuteswa na hata kuuawa.

Aidha, si tu Serikali ya Biya ilizuia taarifa zilizokuwa zikiikosoa, bali pia ilitumia redio, televisheni, magazeti au vyanzo vingine vya habari kueneza propaganda.

Ni kama ilivyo nchini Guinea ya Ikweta, ambako hadi leo hii Serikali imeamua kutoruhusu uwepo wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi, lengo likiwa ni kuzuia ukosoaji.

Huko Gabon, mbali ya kuwa ni vituo vichache vya redio na televisheni vinavyomilikuwa na watu binafsi, vyote viko chini ya wafanyabiashara walio karibu na serikali, hivyo vinaendeshwa kwa masilahi ya ‘wachache’.

Kazi kubwa ya vyombo vya habari vya watu binafsi katika nchi zinazoongozwa na madikteta ni kujisalimisha kwa serikali, yaani kwa sauti ya viongozi walio madarakani na si kufichua maovu yao.

Ubabe wa vyombo vya dola

Kama ilivyo nchini Cameroon, hiyo ni moja kati ya sifa kubwa za serikali zinazoongozwa na madikteta, kutumia vyombo vya dola kuwahenyesha wananchi na wakosoaji wake.

Lengo ni kuhakikisha wananchi wanajawa hofu katika kukosoa mwendendo usioridhisha wa viongozi walio madarakani.

Kwa hali hiyo, ni ngumu kushuhudia serikali ikikosolewa, zaidi ya kusifiwa hata kwa mambo yasiyo na tija. Chini ya uongozi wa Biya, imekuwa hivyo nchini Cameroon. Jeshi limekuwa mwiba mchungu kwa watu wake, hasa jamii ya wanaozungumza Kiingereza.

Katika hilo, video zinazowaonesha wakiwaua wanawake na watoto zimekuwa zikisambaa mitandaoni na kuzua gumzo katika mijadala ya wadau wa siasa na watu wa haki za binadamu.

Kuwanunua, kuwabana wapinzani

Kutibitisha hilo, kuna kipindi vyombo vya habari viliwahi kuripoti kuwa Rais Biya na washirika wake wamekuwa wakiwanunua viongozi wa vyama vya upinzani, wakilazimisha uungwaji mkono.

Ndiyo maana haikushangaza kuona vyama vya upinzani 20 vikitangaza kumsapoti kiongozi huyo mara tu alipotangaza nia ya kugombea tena katika Uchanguzi Mkuu wa mwaka huu.

Ukiacha wapinzani, pia alihusishwa na mpango wa kuwashawishi kwa fedha baadhi ya wenzake ndani ya Chama cha Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM) ili wampitishe katika kinyang’anyiro cha kugombea urais.

Si tu kuwanunua, pia kama wafanyavyo madiketa wenzake, Biya amekuwa akiwatia mbaroni wanaomkosoa, ambapo kwa nyakati tofauti maprofesa na wasomi wengine wamejikuta wakiingia katika majanga hayo.

Ukiacha Biya, madikteta wengine wa Afrika walishawahi kutumia njia hiyo kung’ang’ania Ikulu, hata wakienda mbali zaidi kwa kuwatishia uhai, kuwabambikia kesi, na hata kuwaua viongozi wa upinzani walioonekana kuwa kizingiti kwao.

Kubadilisha katiba

Kama walivyowahi kufanya madikteta wengine, baada ya kukaa madarakani kwa awamu mbili, Biya alibadili Katiba ya Cameroon ili tu imruhusu kugombea tena nafasi ya Urais, yaani kwa mara ya tatu. Hiyo ilikuwa mwaka 2008.

Kipindi hicho, tayari alishakaa Ikulu kwa miaka 25 lakini hakuridhika. Nguvu ya ushawishi aliyonayo, ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na rushwa na vitisho, ilimwezesha kupata kura 153 kati ya 180 zilizopigwa na wabunge.

Pia, hilo la kubadili katiba huwa ni kwa lengo la kuondoa kipengele cha umri anakotakiwa kuwa nao mgombea wa kiti cha urais, kigezo ambacho wanakiona kuwa ni kizingiti kwao.

Kwa kubadilisha katiba kwa dhamira ya kubaki madarakani, Biya anaungana na marais Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Denis Sassou Nguesso (Congo-Brazaville).

Pia, wafuatiliaji wa mwenendo wa siasa za Afrika hawajasahau kuwa hilo limefanywa kwa nyakati tofauti na Idriss Deby (Chad), Pierre Nkurunziza    (Burundi) na Lansana Conte (Guinea).

Kupandisha ada fomu za Urais

Hapa lengo la madikteta huwa ni kuwazuia wanasiasa wengine wenye uwezo na ubora wa kugombea nafasi ya urais na kuongoza mataifa hayo.

Wengi wa wanasiasa hao ni wale wa kizazi kipya ambao wanaongozwa na mitazamo mipya ya kuzijenga nchi za Afrika. Mafano, Julius Malema (Afrika kusini), Bob Wine (Uganda) kwa kuwataja wachache.

Hivi karibuni, Serikali ya Biya ilitangaza kupanda kwa ada ya kuchukua fomu za Urais, kutoka Dola za Marekani 8750 (zaidi ya Sh mil. 20 za Tanzania) hadi Dola 52460 (zaidi ya Sh mil 120).

Kwa mazingira hayo, hata kama ni wengi wanaotamani kuingia Ikulu, wachache pekee ndiyo watakaoweza kumudu gharama hizo, akiwamo Biya  mwenyewe anayetajwa kuwa na utajiri wa kutisha.