Home Latest News HOFU YA UKOMUNISTI ILILETA UHURU BILA MAPAMBANO

HOFU YA UKOMUNISTI ILILETA UHURU BILA MAPAMBANO

746
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

DUNIANI kote, uhuru wa kisiasa wa nchi hupatikana na umepatikana kwa njia kuu mbili zifuatazo; ama kwa mapambano ya silaha pale wananchi wanapoamua kuuondoa utawala wa kikoloni; au kwa njia ya mitafaruku ya kijamii ya ndani dhidi ya ukoloni kulazimisha maridhiano kwa wakoloni kutoa uhuru kwa Wazalendo.

Nchi zilizopata uhuru kwa njia ya mapambano ya silaha na mapinduzi, zina tabia ya kulinda matunda yake ya uhuru kwa nguvu zote kwa mbegu ya uzalendo iliyofanya zishike silaha (Urusi, China, Cuba, Vietnam, Algeria); tofauti na zilizopata uhuru mezani kwa maridhiano (Nigeria, Tanzania, Ghana, Zambia) ambazo mara nyingi hazina  machungu ya kutawaliwa na hivyo kujiendesha kishaghalabaghala kwa sababu hazina gharama wala jasho la kukumbukwa.

Ukaidi wa nchi za kikoloni kutoa uhuru kwa makoloni yake ulilegea kufuatia vita ya Pili ya Dunia (WWII) zilipoanza kushuhudia upepo na mabadiliko, vuguvugu la kudai uhuru na maasi duniani kote kuashiria kupita kwa enzi za ukoloni mkongwe.

Ili kuepuka ghadhabu ya kihalaiki ya wananchi wa makoloni, wakoloni walibuni mtindo wa kutoa uhuru kwa maridhiano kwa kukaa mezani na wenye kudai uhuru. Mapambano ya silaha hayakukwepeka pale  wakoloni wachache waliposhindwa kusoma alama za nyakati na maandiko ukutani kama ilivyotokea huko South West Africa (Namibia), Rhodesia Kusini (Zimbabwe), Angola na hata Kenya kwa kuzua vita ya ‘Mzungu arudi Ulaya, Mwafrika apate Uhuru’ maarufu kama ‘MAU MAU’.

Pigo kubwa kwa nchi za kikoloni baada ya WWII (huku zikiwa zimejeruhiana na kudhoofika kwa vita), lilikuwa pale nchi za kuibukia za Kambi ya Kisoshalisti na ambazo hazikuguswa na madhara ya vita, zikiongozwa na Urusi na China zilipoamua kusaidia kwa njia ya mapambano ya silaha nchi za makoloni zilizodai uhuru. Ni kuanzia hapo, pale hofu ya Ukomunisti (Usoshalisti) ilipozikumba nchi hizo za kibeberu, zilikalegea na kukubali kutoa uhuru wa ‘bendera’ kwa mkono wa kulia na kuunyakua papo hapo kwa mkono wa kushoto kwa njia ya ‘ukoloni mamboleo’ uliodumu hadi leo.

Uhuru wa Tanzania na wa nchi nyingi za dunia ya tatu ulipatikana kwa ridhaa ya aina hii. Na ingekuwa vivyo hivyo kwa nchi kama Angola, Zimbabwe, Namibia na Msumbiji ambako wananchi walilazimika kuchukua silaha, kama watawala wa enzi hizo, japo walikuwa weupe, wangekubali kuongoza nchi kwa kuheshimu na kuzingatia matakwa ya wananchi wote bila ya ubaguzi.

Walichopinga wanaharakati wa ukombozi, kwa mfano, nchini Rhodesia Kusini (Zimbabwe) hadi kubeba silaha, haikuwa (kwa kumnukuu Mwalimu Nyerere): “Ian Smith (mweupe) kuongoza Rhodesia Kusini, bali sera zake za kibaguzi na ukandamizaji dhidi ya walio wengi nchini humo.” Maana ukoloni haikuwa ajenda tena zama hizo, bali ajenda ilikuwa demokrasia na utawala bora ambao ndio uhuru wenyewe.

Kosa la Smith pia lilikuwa ni hatua yake ya kujitangazia ‘Uhuru’ kwa mabavu (Unilateral Declaration of Independence) – UDI, mwaka 1964 bila kutumia sanduku la kura, kwa kuwa huo aliotangaza haukuwa uhuru wa kweli bali ilikuwa kupoka mamlaka ya wananchi; vinginevyo kama angefuata taratibu, Smith angekuwa mtawala wa Zimbabwe huru bila kukaribisha vita kwa sababu, japo alikuwa mweupe kwa rangi, lakini alikuwa raia wa Zimbabwe kwa vigezo vyote kustahili kuongoza nchi.

Ukiondoa nchi hizo na zingine, sehemu kubwa ya Afrika ilipata uhuru kwa kupewa kwenye sahani mezani kwa mazungumzo na maridhiano na wakoloni. Kwa makoloni ya Uingereza, sahani ilikuwa ‘Lancaster House’, ambapo Katiba za uhuru (Independence Constitutions) zilitolewa(kwa Malkia) na kushushwa kwetu kama ‘manna’ kutoka mbinguni kutoa ramani ya madaraka na namna ya kujitawala. Ni mazingira yapi duniani yaliyosukuma hayo mpaka kutokea?

Ni hivi: Ukoloni duniani pamoja na matumizi ya nguvu ya vyombo vyake, haukuweza kuwageuza wananchi ‘mataahira’ nyakati zote na siku zote.  Kadiri wakoloni walivyozidi kutumia nguvu kuwanyamazisha wananchi, ndivyo walivyochochea upinzani na maasi kwa ushindi mkubwa. Kwa mfano, ushindi wa wakulima na wafanyakazi wa Urusi dhidi ya utawala wa kiimla wa Mtawala wa Urusi [Tsar] mwaka 1917 [maarufu kama “Mapinduzi ya Oktoba”], yalikuwa kichocheo kikubwa kwa harakati za wananchi kwenye makoloni kuasi dhidi ya ukoloni na ubeberu kote duniani. Kwa mwaka 1919 pekee, ukoloni kwa nchi za Mashariki ya mbali, ulitikiswa na matukio matatu ya kihistoria, ambayo ni maasi ya Machi 1, nchini Korea; harakati za kimapambano ya kundi la “the Fourth of May” nchini China, na harakati za Chama cha kiharakati cha “Ceylon National Congress” [CNC] nchini Ceylon (sasa Sri Lanka). Matukio haya yaliyosambaza mawimbi yenye mlipuko wa migomo na maandamano nchini India, yalizimwa na Waingereza kwa ukatili mkubwa.

Mwaka 1920, mbali na mgomo mkubwa nchini Burma, dunia ilishuhudia harakati za Vyama vya kisiasa na makundi ya kupigania demokrasia, yakiibuka kama uyoga nchini Misri, Tunisia na Afrika Kusini; na vivyo hivyo migomo mikubwa nchini Kenya na Morocco, maarufu kama “The Rif Rebellion”

Kufikia mwishoni mwa WW II mwaka 1945, “Upepo mkali wa Mabadiliko” ulikuwa ukivuma kwa nguvu dunia nzima na kushuhudia kupatikana kwa uhuru kwa nchi za India na Pakistani mwaka 1947, na kufuatiwa na Burma, Sri Lanka na Indonesia.Na kati ya  mwaka 1948 na 1959, nchi za China, Korea Kaskazini, Vietnam, Tunisia, Guinea, Ghana na Cuba, kwa kutaja chache tu, nazo zilipata uhuru. 

Uhuru wa nchi hizi una umuhimu mkubwa na wa kipekee katika historia ya ukoloni,ubeberu na mageuzi ya kisiasa kwa nchi zilizotawaliwa.  Kwamba, nchi hizi ambazo kimsingi zilikuwa za wakulima wanyonge na zenye umwinyi wa kati, ziliweza kuvunja kwa kishindo mfumo wa uchumi uliopitwa na wakati, na kupasua njia kuelekea kwenye mfumo wa Ujamaa na hivyo kuimarisha kambi na mshikamano wa Kijamaa [kikomunisti] duniani kwa kushibishana.

Hivyo, wakati kambi ya kijamaa ikiendelea kupanuka, sambamba na juhudi za kupinga ukoloni pamoja na mwamko na uelewa wa watu juu ya uhuru kuota mizizi na kukomaa kwa kasi kubwa, wigo wa ubeberu wa kinyonyaji nao uliendelea kusinyaa haraka na kwa hofu kubwa.Kwa nchi za Afrika Mashariki, kipindi chote kufuatia kumalizika kwa WW II [1945], kilighubikwa na machafuko na maandamano [kama yale ya India ya 1940], wakati huo dunia nzima ikighubikwa pia na migomo mzizimo, chuki na upinzani dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji wa kikoloni. 

Kwa mfano, nchini Uganda, Wakulima na Wafanyakazi walichoma majengo ya Utawala na nyumba za Machifu [Watemi] kupinga kodi kubwa, bei ndogo ya mazao na mfumo wa kikandamizaji uliowanyima haki za kidemokrasia.  Mara nyingi Polisi waliitwa kutuliza ghasia, ambapokwa mwaka 1947 pekee, watu 1,724 walikamatwa [Soma: D. W. Nabudere:  Imperialism and Revolution in Uganda, uk. 133-4].Nchini Kenya, hali ilikuwa mbaya zaidi dhidi ya Ukoloni, katika vita iliyojulikana kama“Mau Mau”. Itaendelea wiki ijayo