Home Makala Hofu ya Ukomunisti ilitupatia uhuru bila kutoka jasho

Hofu ya Ukomunisti ilitupatia uhuru bila kutoka jasho

520
0
SHARE

Na JOSEPH MIHANGWA

DUNIANI kote, nchi huru zilizokuwa makoloni ya mataifa mengine, ikiwamo Tanganyika [sasa Tanzania], zilipata uhuru kwa njia moja kati ya mbili zifuatazo: ama kwa njia ya kudai uhuru mezani na majukwaani bila kutoka jasho, kama ilivyokuwa kwa Tanganyika, Nigeria, Ghana, Uganda, India, Mauritius na zinginezo.  

Hizi zinatajwa kupata uhuru kwa kupewa kwenye sahani kwa shinikizo la nyakati [epoch] au kwa kuhurumiwa.

Mara nyingi uhuru wa nchi hizi ni dhaifu, usio na ulinzi kwa sababu hakuna mwenye uchungu kwa sababu ni wa bure; na kwa sababu hii ni rahisi kuingiliwa kwa njia ya ukoloni mpya, maarufu kama “ukoloni mamboleo” chini ya viongozi vibaraka wa mfumo huo hivi kwamba hapa na pale, nchi hizo huandamwa na ghasia au mapinduzi ya kijeshi. 

Au zilipata uhuru kwa njia za harakati za kimapinduzi na mapambano ya silaha ya umwagaji damu kufanya wakoloni kusalimu amri kwa nguvu ya umma. Hizi kwa mfano, ni pamoja na Cuba, Urusi, China, Zanzibar, Angola, Msumbiji Guinea Bissau, Algeria, Vietnam na zingine.

Mara nyingi, uhuru wa nchi hizi ni madhubuti kwa sababu kila raia anaguswa na gharama ya ulivyopatikana na hakuna mwenye kuuchezea akasalimika mkono wa chuma wa Serikali ya wananchi.  Ni nchi zilizopata uhuru kwa kuongozwa na itikadi ya mapambano ya mrengo wa Ki-Karl Max au Kikomunisti wa nyakati hizo.

Ni kwa bahati nzuri kwamba, katika kipindi cha miaka ya 1940 kufuatia kumalizika kwa vita ya pili ya dunia [WW II] hadi miaka ya 1960, harakati za uhuru duniani kote ziliendeshwa kwa njia mbili tulizozitaja hapo juu ambapo njia hii ya pili, ya harakati za Mapambano ya kisilaha kwa itikadi ya Ki-Karl Marx [Cuba, Vietnam, Algeria] ilizitia kiwewe nchi za Makoloni, hasa ilipobainika kwamba, nchi za Kambi ya Kisoshalisti/Kikomunisti [China, Urusi, Czechoslovakia, Bulgaria, Cuba, Albania na zingine] zilizokuwa zikiibukia kwa nguvu mpya kiuchumi na kijeshi, zilikuwa tayari kujitoa mhanga kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za dunia ya tatu kote ulimwenguni.

Ni kwa sababu hii, nchi za Kikoloni za Ulaya na ambazo tayari zilikuwa zimejijeruhi katika vita na kudhoofika kiuchumi na kijeshi, ziliona heri kuachia makoloni yake kuepuka kichapo cha harakati za Kikomunisti kwa kutoa “uhuru wa bendera”, lakini kwa lengo la kurejea kwa njia ya Ukoloni Mamboleo.

Japo si mahali pake hapa, lakini nitamke kwa kifupi tu kwamba, kuundwa kwa taasisi za uwakala wa ukoloni mamboleo chini ya dhana ijulikanayo kama “Truman Doctrine”, kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa [IMF], Benki ya Dunia [WB], kulikuwa na lengo la kuzirubuni “nchi huru” kwa misaada yenye sumu ziweze kunaswa kwenye utando wa Ukoloni-mamboleo bila kujijua, zoezi linaloendelea hadi leo.

Uhuru wa Tanganyika ulipatikana kwa njia hii bila jasho.  Ilikuwaje kwingineko duniani? Ni hivi: Kila chenye mwanzo, kina mwisho.  Ukoloni duniani, pamoja na matumizi ya nguvu ya vyombo vyake, haukuweza kuwageuza wananchi “mataahira” nyakati zote na siku zote.  Kadiri Wakoloni walivyozidi kutumia nguvu kuwanyamazisha wananchi, ndivyo walivyochochea upinzani na maasi ya ushindi kwa njia ya “nguvu ya umma”.

Kwa mfano, ushindi wa wafanyakazi na wakulima wa Urusi dhidi ya utawala wa kiimla wa mtawala wa Urusi [Tsar] mwaka 1917 [maarufu kama “Mapinduzi ya Oktoba], yalikuwa ni kichocheo cha harakati kwenye makoloni dhidi ya utawala na ubeberu kote duniani.

Kwa mwaka 1919 pekee, ukoloni kwa nchi za mashariki ya mbali ulitikiswa na matukio matatu muhimu kihistoria, nayo ni maasi ya Machi 1 nchini Korea; harakati za kimapambano za kundi la “the Fourth of May” nchini China na harakati za chama cha kiharakati cha “Ceylon National Congress” [CNC] nchini Ceylon, ambayo sasa inaitwa Sri Lanka.  

Matukio haya yaliyosambaza mawimbi ya mlipuko wa migomo na maandamano nchini India, yalizimwa na Waingereza kwa ukatili mkubwa.

Mwaka 1920, mbali na mgomo mkubwa nchini Burma, dunia ilishuhudia harakati za Vyama vya kisiasa na makundi ya kupigania demokrasia yakiibuka kama uyoga nchini Misri, Tunisia na Afrika Kusini; na vivyo hivyo migomo mikubwa nchini Kenya na maasi huko Morocco, yaliyojulikana kama “The Rif Rebellion”  

Kufikia mwishoni mwa vita ya Pili ya Dunia mwaka 1945, “upepo mkali wa mabadiliko” ulikuwa ukivuma kwa nguvu dunia nzima na kupatikana kwa uhuru kwa nchi za India na Pakistan mwaka 1947 na kufuatiwa na Burma, Sri Lanka na Indonesia.  

Kati ya  mwaka 1948 na 1959, China, Korea Kaskazini, Vietnam, Tunisia, Guinea, Ghana na Cuba, kwa kutaja chache tu, nazo zilipata uhuru.

Uhuru wa nchi hizi una umuhimu wa kipekee katika historia ya ukoloni, ubeberu na mageuzi ya kisiasa kwa nchi zilizotawaliwa.  Kwamba, nchi hizi ambazo kimsingi zilikuwa za wakulima wanyonge na zenye umwinyi wa kati, ziliweza kuvunja kwa kishindo mfumo wa uchumi uliopitwa na wakati na kupasua njia kuelekea kwenye mfumo wa Ujamaa na kuimarisha kambi ya mshikamano wa Kijamaa [kikomunisti] duniani.

Hivyo, wakati kambi ya kijamaa ikiendelea kupanuka, sambamba na juhudi za kupinga ukoloni na uelewa wa watu juu ya uhuru kupevuka kwa kasi kubwa, wigo wa ubeberu wa kinyonyaji nao uliendelea kusinyaa kwa haraka.

Kwa nchi za Afrika Mashariki, kipindi chote kufuatia kumalizika kwa vita ya Pili ya dunia, kilighubikwa na machafuko na maandamano [kama yale ya India ya mwaka 1940], wakati dunia nayo ilighubikwa na migomo na mzizimo wa chuki dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji wa kikoloni.

Kwa mfano, nchini Uganda, Wakulima na Wafanyakazi walichoma majengo ya Utawala na nyumba za Machifu [Watemi] kupinga kodi kubwa, bei ndogo ya mazao na mfumo wa kikandamizaji uliowanyima haki za kidemokrasia.  Mara nyingi Polisi waliitwa kutuliza ghasia, na kwa mwaka 1947 pekee, watu 1,724 walikamatwa [Soma: D. W. Nabudere:  Imperialism and Revolution in Uganda, uk. 133-4].

Nchini Kenya, hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana  na mapambano ya Wanaharakati dhidi ya Ukoloni, katika vita vya msituni vya “Mau Mau”.

Nchini Tanganyika, wafanyakazi waliunda Vyama vya Wafanyakazi na kutikisa Serikali ya wakoloni kwa migomo. Kwa mfano, mwaka 1951, wafanyakazi waliendesha mgomo mkubwa ambapo katika ujumla wao, siku 12,775 za kazi [man-days] zilipotea.  Na mwaka 1956, mwaka mmoja tu kufuatia kusajiliwa kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini [TFL] lenye vyama 17, upotevu wa muda kazini kwa watumishi 17,695 waliogoma, ulifikia saa 58,066, na kupanda kufikia 1,494,773 mwaka 1960 kwa watumishi 89,495.

Mmoja wa migomo hiyo ni ule “mgomo wa kunywa bia” wa mwaka 1958, ambapo Mwalimu Nyerere aliwaambia wafanyakazi na wananchi “mkinywa bia, mnakunywa damu ya watu wenu wenyewe”.  Na kweli uzalishaji na unywaji bia ukasusiwa nchi nzima.

Nyerere ananukuliwa akielezea jinsi wananchi walivyohamasika kuchukia ukoloni, anasema: “Kufikia mwaka 1958, Waingereza waliogopa na kufadhaika kiasi kwamba kama ningeamuru wananchi wawapige, wangefanya hivyo bila kusita.  

Ukweli kulikuwa na Serikali mbili, [ya Waingereza na yangu kwa uficho] na “Serikali” yangu kusema kweli, ndiyo iliyokuwa na nguvu kuliko Serikali rasmi madarakani”.

Mwalimu anaongeza kwa kusema:  “Enzi hizo, utawala wa kikoloni haukutilia maanani “kelele” zetu kwa sababu nchi yetu haikuwa na mwamko wa kisiasa; kwa hilo tulikuwa na bahati ya kutofuatwa fuatwa au kubanwa banwa kwa “kelele” zetu za kudai uhuru, kama ilivyokuwa kwa wenzetu huko Kenya na Uganda; sisi tulichukuliwa kama watu tusioendelea kuweza kuzua ghasia”.

Hatimaye, Uingereza ambayo tayari ilikuwa imedhoofu kwa majeraha ya kiuchumi iliyopata katika Vita ya Pili ya Dunia, ilisalimu amri kwa nguvu ya umma iliyotaka mabadiliko ya kisera.  Ukweli ni kwamba, Serikali ya Kikoloni tayari ilikuwa imeanza kufanya mabadiliko ya geresha tangu mwaka 1945 ili kupunguza upinzani kwa Serikali hiyo, ambapo Novemba mwaka 1945, iliwateua Watanganyika [Waafrika] wawili, wote Machifu, kuingia kwenye Bunge la kutunga Sheria [LEGCO].  

Hao walikuwa ni Abdiel Shangali na Kidaha Makwaia na kuapishwa na Gavana William D. Battershill, Desemba 3 mwaka 1945. Waliongezwa wengine wawili baadaye, nao walikuwa Chifu Adam Sapi Mkwawa, aliyeteuliwa Juni 3, 1947 na Juma Mwindadi [Mwalimu wa Shule], aliyeteuliwa Aprili 1, 1948.Lengo la uteuzi huo lilikuwa ni kuwahadaa Watanganyika kwamba, waliwakilishwa katika kusimamia Serikali hiyo ya Kikoloni. 

Katika miaka yote ya 1950, wakati Serikali ya Kikoloni ikizidi kukabiliwa na machafuko nchini, iliamua kulipa hadhi Bunge [LEGCO] kwa kupitisha Sheria ya Uchaguzi [Legislative Council Election Ordinance] Namba 388, ya mwaka 1957, ambapo kwa mara ya kwanza katika miaka 75 ya utawala wa kikoloni wa  Wajerumani na Waingereza, Watanganyika waliruhusiwa kuchagua wawakilishi wao mwaka 1958.

Uchaguzi Mkuu wa 1958-9 ulifanyika chini ya masharti magumu kwa Watanganyika, hususani, juu ya kupiga na kupigiwa kura, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuwa na elimu isiyopungua darasa la 8, umri usiopungua miaka 21, kipato kisichopungua Sh 3,000 kwa mwaka; kujua kusoma na kuandika Kiingereza au Kiswahili au kuwa mwajiriwa wa Serikali.

Lengo lilikuwa ni kujaribu kulipa uhalali Bunge kwa uwakilishi wa kitabaka. Hata hivyo, ingawa wajumbe wa kuchaguliwa walikuwa 30, idadi yao ilizidiwa kwa mbali na idadi ya wajumbe 51 wa kuteuliwa.  Kati ya wajumbe hao 30 wa kuchaguliwa, 10 walikuwa Waafrika, 10 Waasia na 10 Wazungu; wote wakiwakilisha majimbo 10 ya uchaguzi kwa mfumo wa kura tatu [tripartite vote].

Kwa kutumia dhana ya “wabunge wa kuteuliwa”, kama ilivyo kwa “wabunge wa kuteuliwa na wa viti maalumu” hapa kwetu hivi leo, Bunge hilo halikuwa na nguvu dhidi ya Serikali yake; lilikuwa Bunge la kiini macho ambapo kazi yake ilikuwa ni kuhalalisha tu maamuzi ya Serikali.

Bunge la pili kufuatia uchaguzi mkuu wa Agosti 30 mwaka 1960, ambapo Chama cha “Tanganyika African Union [Tanu], kikiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilishinda kwa kunyakua viti 70 kati ya viti 71, lilikuwa na mabadiliko kidogo kulinganisha na lile la mwaka 1959.  Safari hii lilikuwa na wabunge 71 wa kuchaguliwa na 10 wa kuteuliwa.  Kati ya wabunge hao 71, viti 10 vilikuwa kwa ajili ya Wazungu na 11 kwa Waasia.

Hatimaye Septemba mwaka 1960, Uingereza ilisalimu amri kwa shinikizo la Watanganyika, kwa kukubali kuundwa Serikali yenye mamlaka ya ndani [Responsible government] na kufuatiwa na Mkutano wa Katiba [Constitutional Conference] uliofanyika mjini Dar es Salaam, Machi 27-29, 1961, chini ya uenyekiti wa Waziri wa Makoloni wa Uingereza, Ian Macleod.

Ilikuwa ni utamaduni enzi hizo, kwa mikutano kama huo kufanyika “Lancaster House”, nchini Uingereza, kwa nchi zote zilizokuwa zinapata uhuru kutoka kwa Waingereza.  Lakini kwa sababu ambazo hazijapata kuelezwa, Tanganyika ni nchi pekee iliyopata heshima ya Mkutano huo wa kuzungumzia uhuru kufanyika nchini mwake.

Kwenye Mkutano huo, ilikubaliwa Tanganyika iwe na Serikali kamili ya Madaraka ya Ndani ifikapo Mei 1961, kama hatua ya mwisho kuelekea uhuru kamili, Desemba 9, 1961. Walielewa fika kwamba, kuendelea kuwakandamiza wananchi, kungekaribisha Serikali za Kikomunisti kuingilia kati kuwasaidia wanyonge, kama ilivyotokea huko China, Korea Kaskazini na Vietnam.  

Je, tumeweza kuruka kihunzi cha “Truman Doctrine” kama nchi huru?.  Jibu ni ndiyo na hapana, japo si jibu.  Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa makini sana katika siasa za Kimataifa kwa kutofungwa nira na ama sera za ubepari wa Kimagharibi au sera za Usoshalisti wa Kimashariki kufikia yeye na Viongozi wengine wanaharakati wa nchi za dunia ya tatu kuanzisha Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote.

Hata hivyo, hatua ya kuanzisha Ujamaa nchini, ambao yeye alikataa kuuhusisha au kuufananisha na “Usoshalisti”, ilimweka katika kitabu cheusi cha nchi za Kimagharibi kwamba aliegemea zaidi kwenye kambi ya Usoshalisti na Ujamaa ukapigwa vita kwa jino na ukucha hadi kuzikwa kwa koleo la “Azimio la Zanzibar” mwaka 1992.

Hapo kale tulituhumiwa na nchi za Magharibi kuitika mwangwi wa nchi za Kikomunisti kikondoo; sasa nchi hizo zinataka tuzifuate kwa kuitika mwangwi wa utandawazi chini ya sera za IMF na WB, wakielewa kwa kufanya hivyo kwetu ndiyo itakuwa “Kwa heri Uhuru” na historia ya ukoloni kujirudia.  

Kuepuka shari hii, yataka Uongozi wenye maono zaidi ya “Uhuru na Kazi” wala “Uhuru ni Kazi”; bali kwa kuwa Uhuru tulikwishapata, kinachotakiwa hapa ni “Kazi tu” bila kusikiliza wala kuitika mwangwi kwa kiashirio cha utegemezi na kifo cha uhuru na usitawi wa Taifa, maana safari hii tukiteleza, hakuna mtu wala Ukomunisti wa kutukomboa.

 HYPERLINK “mailto:jmihangwa@yahoo.com/0713-526972” jmihangwa@yahoo.com/0713-526972