Home Latest News HOJA YA MALEMA IUNGWE MKONO NA WANAMAJUMUI WA KIAFRIKA

HOJA YA MALEMA IUNGWE MKONO NA WANAMAJUMUI WA KIAFRIKA

5696
0
SHARE

NA ABDALLAH MAJID


AGOSTI 30 mwaka huu, Kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters cha Afrika ya Kusini (EFF), Julius Malema alitoa hoja ya kutumika kwa Kiswahili kama lugha ya Bara la Afrika. Malema alitoa kauli hiyo ofisini kwake wakati alipokuwa akiongea na wanahabari nchini humo. Hata hivyo, ieleweke kuwa ndugu Malema si mwafrika wa mwanzo kuwa na hoja hii. Hoja hii pia imewahi kutajwa na Kwame Nkurumah, Julius Nyerere, Muamar Gadafi, Robert Mugabe na Joachim Chisano.

Kwa mintarafu hii, vyombo vya habari kama Redio One, Uhuru fm na Uhai fm kwa kuvitaja vichache vyote vya Tanzania viliomba maoni yangu kuhusu hoja ya Malema.

Nilichojaribu kukieleza kilijikita katika hoja kuu tatu. Mosi, hoja ya kukua na kutandawaa kwa lugha ya Kiswahili. Ni kwamba, Malema na wengine wa mfano wake wanaamini kuwa lugha ya Kiswahili imekuwa na kutandawaa kiasi cha kufikia upeo wa kuaminika kutumika kama chombo cha kuwaunganisha waafrika ndani na nje ya bara lao.

Hoja hii inapewa ithibati na takwimu za lugha duniani ambapo Kiswahili kinatajwa kuwa ni lugha ya 10 kati 6000 zinazosemwa duniani kote.

Aidha, lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili baada ya Kiarabu inayosemwa na idadi kubwa ya watu hapa Afrika.

Ama kuhusu Kiarabu kwa maoni yangu, ingawa kinasemwa na idadi kubwa zaidi ya Kiswahili lakini ushawishi na ukubalifu wake si  mkubwa sana. Kwa maoni yangu sababu za Kiarabu kutokuwa na ushawishi na ukubalifu zaidi ni kunasibishwa kwake na dini ya Kiislam, baadhi ya watu wanakinasibisha na ugaidi (Hata hivyo, hoja hii si ya kweli ) na mwisho, Kiarabu baadhi ya watu hukufikiri ni lugha yenye mizizi yake nje ya Afrika hasa katika Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali.

Kwa hiyo, Kiswahili kinatajwa kuwa na ushawishi mzuri zaidi hasa kwa kuwa kinatajwa kuwa lugha ya diplomasia zaidi katika kutafuta suluhu ya mizozo kadha wa kadha ndani ya Afrika ya Mashariki (Rwanda, Kenya, Burundi , nk).

Hoja ya pili ni kuwa Kiswahili ni kama alama ya Umajumui wa Kiafrika. Kwa hiyo, ndugu Malema kama walivyofikiri akina Nkurumah, J.K. Nyerere, na wengine mnamo miaka ya 1950, na sasa akina, Chisano,  Mugabe na Gadafi mnamo miaka ya 1990 kuwa Kiswahili kitumike katika kuutambulisha utu wa Afrika, kutuunganisha Waafrika, kutusemea kwa sauti moja na kutuwakilisha kwa kadri inavyopaswa kuwa.

Malema akiwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi wa siasa za mrengo wa kushoto nchini Afrika ya Kusini, anafikiri kuwa Waafrika hatuwezi kufikia katika Uhuru kamili wa kiuchumi iwapo hatutaanza na Uhuru wa kiutamaduni.

Taathira ya ukoloni imetufanya  baadhi ya Waafrika tujipuuze, tujidharau na kujikataa kwa kuacha mila na desturi zetu ikiwemo lugha zetu. Baadhi ya Waafrika wamekwenda mbali zaidi kiasi cha kukataa rangi zao kwa kujichubua, kukataa nywele, kucha, kope, nk. Wao hudhani mtu mweupe ni bora na Utamaduni wake ni bora zaidi ya wetu. Unyonge huu pia unatajwa na Ngugi wa’ Thiong kupitia andiko lake la ‘Decolonized Mind ‘ na Fratz Fanon kupitia andiko lake la ‘Black Skin White Mask’. Kwa hakika Malema anataka unyonge huu tuupinge kwa nguvu zetu zote kwa kuanzia na lugha ya Kiswahili kuwa nyenzo ya Umoja,  Mtangamano na Mtagusano wa Afrika.

Ni lazima tuseme au tueleze na tuoneshe thamani yetu kama Waafrika kwa lugha yetu wenyewe ( Kiswahili).

Ni muhimu ikieleweka kuwa lugha za kigeni ni muhimu kwa Waafrika kama ilivyo kuwa muhimu kwa watu wa mabara mengine. Hata hivyo, ni vyema kutambua kuwa umuhimu huo hauondoi ulazima na umuhimu wa kutumia lugha zetu ktk kujifunza na kufundishia na ktk maeneo mengine muhimu.

Hoja ya tatu ni Diplomasia ya Uchumi kupitia lugha ya Kiswahili ( Hoja hii haisemwi sana). Kwa dahari nyingi lugha ya Kiswahili imetumika kama  nyenzo ya mawasiliano miongoni mwa jamii. Shabaha  hii ya awali haikuwa mbaya lakini hivi sasa ni lazima tutazame tofauti.

Hoja ya Malema inakuja wakati washititi wa Kiswahili wanaona kuwa wakati huu ni  mwafaka wa  kuibidhaisha lugha ya Kiswahili.

Hoja hii  imesimama katika kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kibiashara , mtaji  wa uwekezaji na biashara ya huduma. Iwapo tutakibidhaisha Kiswahili tutakiongezea thamani ili lugha hii *iweze kushindana katika soko la bidhaa za lugha duniani.*

Ubidhaishaji utafanya biashara ya bidhaa za Kiswahili zipate soko kubwa zaidi Afrika na nje ya Afrika. Huduma za tafsiri, ukalimani, filamu, muziki, utalii wa kitamaduni, kufundisha wageni Kiswahili, nk vitapata soko mara dufu.

Kwa kufanya hivi tutaweza kutengeneza ajira nyingi za moja kwa moja  za wataalam wa Kiswahili na zisizo za moja kwa moja. Ajira hizi zingetengeneza kipato kwa watu wetu na kodi kwa serikali. Bila shaka, Kiswahili kikiwa bidhaa kitaweza kuchangia ktk pato la taifa/ mataifa yetu.

Kwa ujumla, ukitafakari hoja zote hizi itabainika kuwa ndugu Malema ameirejesha hoja hii ktk wakati ambao vuguvugu la Uhuru wa kiuchumi ambapo kutafanya Waafrika waweze kujitegemea na kuheshimika na jamii nyinginezo za nje ya Afrika. Hata hivyo, mawazo haya hayaondoi muhimu wa kuwa na lugha zetu za makabila au kujifunza lugha za kigeni.

Nini cha kufanya ktk nchi za Afrika/ Tanzania?

Kwanza serikali ya Tanzania ifanye maamuzi ya kukitumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia kutoka elimu msingi hadi sekondari na vyuo.( Tunahitaji sera madhubuti ya lugha hapa nchini pengine BAKITA imeanza kufanya jambo ).

Pili, Kiswahili kitumike katika vyombo vya maamuzi na vya kisheria nchini Tanzania.

Tatu, isaidie nchi nyingine katika harakati za Kiswahili kwa kadri inavyowezekana.

Nne, Balozi zetu pamoja na kazi nyingine zifanye kazi za uwenezi juu ya lugha hii ya Kiswahili. Ninapendekeza balozi zetu zitumike kuwa sehemu mahususi na kufundishia Kiswahili na utamaduni.

Aidha, iwekwe mikakati madhubuti ya kuliendea jambo hili hatua kwa hatua. 

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa lugha, fasihi na fasaha ya Kiswahili. Email: majidkiswahili@gmail.com.