Home Burudani HONGERA QUEEN ELIZABETH, MTIHANI ULIONAO NI HUU

HONGERA QUEEN ELIZABETH, MTIHANI ULIONAO NI HUU

3357
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI


Wiki iliyopita, kulikuwa na mambo mawili yaliyoteka sehemu kubwa ya mijadala ya mitandao ya kijamii. Kuanzia Facebook, Twitter hadi Instagram, hayo ndiyo yaliyokuwa yakijadiliwa zaidi na mashabiki wa tasnia ya burudani.
Kwanza, ni mtifuano uliotokea kati ya ‘timu’ za mastaa wa kike, ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwimbaji wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond Platinumz’.
Kisanga kilianza pale Mobeto alipotajwa kumwendea kwa mganga Diamond, ambaye katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, nilimsikia akisema ni kweli bibiye huyo alifanya hivyo.
Huenda ukajiuliza Wema aliingia vipi katika mkasa huo. Iko hivi, mshindi huyo wa taji la Miss Tanzania mwaka 2006 alijikuta akiingia katika janga hilo baada ya kuonekana kulishabiki suala hilo.
Kilichofuata ni kuyaoga matusi kutoka kwa mashabiki wa Mobeto ambao walihoji sababu ya Wema kufurahia kudhalilika kwa mwanamke mwenzake. Tuachane na hilo kwani si lengo la makala haya.
Tukio la pili lililokuwa gumzo mitandaoni ni kurejea kwa shindano lenye mashabiki wengi la Miss Tanzania ambalo kwa mara ya kwanza nchini lilianza kufanyika mwaka 1994.
Ikumbukwe kuwa ni takribani mwaka mmoja umepita tangu lilipofungiwa na Wizari ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kwa mara ya mwisho, shindano hilo lilifanyika mwaka 2016, ambapo bibiye Dianna Edward aliiibuka kidedea.
Kupitia Baraza la Sanaa la Tanzania (Basata), sababu ya kufikiwa kwa uamuzi huo ulioikera asilimia kubwa ya wapenzi wa Miss Tanzania ilikuwa ni kugubikwa na ubabaishaji kwenye utoaji wa tuzo hiyo.
Baadaye, Mkurugenzi wa kampuni ya Lino iliyokuwa ikiziandaa mbio za kuliwania taji hilo, Hashim Lundenga, alitangaza kuachia ngazi, akisema anataka kuwaachia wengine waendeleze jahazi.
Kijiti kikatua kwa kampuni ya The Look Compay Ltd ya mshindi wa Miss Tanzania mwaka 1998, Basilla Mwanukuzi, na Jumamosi ya wiki iliyopita iliwathibitishia wapenzi wa shindano hilo kuwa limerejea kivingine.
Katika ya warembo 20 waliokuwa kambini, Queen Elizabeth aliibuka kidedea, ambaye mbali ya kujishindia zawadi kibao, likiwamo gari, pia amepata tiketi ya kwenda kuiwakilisha Tanzania katika shindano la Urembo la Dunia ‘Miss World’.
Kwa wasiomfahamu, Queen ndiye aliyekuwa kiboko ya walimbwende wengine waliokuwa wakilitolea macho taji la Miss Kinondoni, na Jumamosi alifanya hivyo pia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kuna changamoto kubwa zinazomkabili mshindi huyo, na kama atashindwa kujipanga kukabiliana nazo, huenda akaingia katika orodha ya warembo wengi tulionao sasa, ambao wamebaki kukumbukwa kwa matukio mengine na si mafanikio yao.
Nini wanachokihitaji zaidi Watanzania wanaopenda mashindano ya urembo? Ni kuiona bendera ya nchi yao ikiwakilishwa vema katika vita ya kuliwania taji la dunia litakalofanyika Desemba 8, mwaka hu, huko Sanya, China.
Ikizingatiwa kuwa hakuna mwakilishi wa Tanzania aliyewahi kulibeba taji hilo tangu kuanzishwa kwa shindano hilo mwaka 1957, huenda mtihani alionao Queen ni kuifuta historia hiyo mbaya na kuandika yake itakayobaki kwa miaka mingi katika kumbukumbu za taifa hili.
Pia, endapo atafanikiwa kurudi nalo nyumbani, rekodi kubwa inayomsubiri Queen ni kuwa Mwafrika wa kwanza kurudi nalo nyumbani kwani kwa miaka yote ya uhai wa shindano hilo mshindi amekuwa akitoka nje ya Bara hili.
Aidha, mtihani mwingine alionao sasa Queen ni kuhakikisha haiishii katika shimo la skendo ambazo mwishowe zitamchafua na kumharibia sifa aliyonayo ya ubalozi wa utamaduni wa Tanzania.
Katika hilo, mtihani mkubwa ninauona kwake ni kuishi maisha aliyokuwa nayo awali na si kupumbazwa na jina alilopata. Wengi walichemsha, wakaacha ‘staili’ zao za maisha ya maadili waliyopatiwa na wazazi wao na kuanza kuishi kama ‘wendawazimu’.
Lakini je, atafanikiwa kuliepuka janga lililowakumba watangulizi wake, ambao wengi wao maisha yao yamebaki kutegemea skendo? Itafika kipindi Queen atakuwa akikumbukwa kwa picha zake chafu mitandaoni na si taji la Miss World?