Home Makala Huduma za kibingwa zinazobeba Mloganzila ndani ya muda mfupi

Huduma za kibingwa zinazobeba Mloganzila ndani ya muda mfupi

433
0
SHARE
Daktari akisubiri kumpima mgonjwa kwa kipimo cha MRI -MLOGANZILA

Na AVELINE KITOMARY

TANGU kuanzishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila mwaka 2017, watu mbalimbali wamekuwa wakipata huduma za matibabu jambo ambalo limepunguza msongamano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga.

Hivi karibuni akizungumza na RAI, Yusuph Mbega Mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam anasema kuanzishwa kwa hospitali hiyo imewapunguzia wananchi adha ya kufunga safari kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga kwa ajili ya kufuata huduma za matibabu.


“Huduma ambazo tulikuwa tukizifuata Upanga sasa zipo
katika hospitali hii, pia mazingira ya ujenzi wake upo karibu na wananchi hivyo hizi ni juhudi kubwa ambazo serikali imekuwa ikifanya kuhakikisha afya ya Watanzania inaimarika,”anasema.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Mloganzila, Dk. Julieth Magandi anasema hospitali hiyo, imetimiza miaka miwili na miezi kadhaa tangu ilipoanza kutoa huduma Julai mwaka 2017 kwa kuona wagonjwa wa nje.

“Ukiacha Muhimbili – Upanga ambayo ina vitanda 1500 vya kulaza wagonjwa, Muhimbili – Mloganzila ina vitanda
608, hatua ambayo inatufanya kuwa na ukubwa nchini.

“Kati ya vitanda hivyo, 31 ni kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), 17 ni kwa ajili ya kutoa dawa na 14 ni vya ‘upasuaji’, vitanda 12 ni vya huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo,”anasema.

Anasema kitanda kimoja kimetengewa maalumu kuhudumia wagonjwa wa figo wenye maambukizi mbalimbali kama Ukimwi, Hepatitis B na mengineyo, huku kukiwa na 27 kwa ajili ya wodi maalumu (VIP).

HUDUMA ZA FIGO
Licha ya kutoa huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, Dk. Magandi anasema wakati wowote wataanza kutoa
huduma bobezi ya upasuaji wa kuondoa mawe katika figo kwa kutumia mionzi ambayo njia hiyo haitahusisha upasuaji mkubwa.

“Huu ni mpango wa serikali katika kuimarisha mtandao wa hospitali za taifa na huduma za ubingwa wa juu zikiwemo za upasuaji wa moyo, huduma kwa wagonjwa wa saratani, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kupitia tundu dogo kwa kutumia kifaa maalumu ikiwa ni kuchuja damu na kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye matatizo.

Dk. Magandi anasema katika matibabu ya figo teknolojia ambayo sasa inatumika ni bora zaidi, kwani watu wengi hawapendi kufanyiwa upasuaji mkubwa kutibu matatizo mbalimbali, hivyo kwa kutumia vifaa vya kisasa walivyo wanahakikisha wagonjwa kupata huduma hiyo.


Anasema kwa mgonjwa wa figo mwenye mawe watatumia teknolojia kuvunja vunja na kuyatoa mawe hayo kwa njia ya haja ndogo.

“Tunazidi kuimarisha huduma za ICU, jengo lipo, vifaa tunavyo lakini changamoto hatuna wataalamu wabobezi
katika eneo hili, kwa kushirikiana na Cuba tayari tumepata wataalamu sita.

“Wamesoma ubobezi wa ICU, wawili ni madaktari na wanne ni wauguzi, watashirikiana na wataalamu wetu ambao wengine hivi sasa wapo masomoni na watakavyokuwa wakishirikiana watazidi kuimarika zaidi na kupata ujuzi, ili siku zijazo tuwe na wabobezi wa ICU,”anasema.

Anasema wameendelea kufadhili masomo ya wataalamu 45 wa fani mbalimbali ikiwamo ya ubobezi wa ICU.

HUDUMA YA UBINGWA WA JUU

Huduma za upandikizaji uloto ni ya kibingwa ambayo inatarajiwa kuanza hapa nchini hii ikiwa ni huduma ambayo inauhitaji mkubwa.

Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili – Upanga zinaonesha kuna wagonjwa takribani 130 hadi 140 ambao huhitaji huduma ya kupandikizwa uloto kila mwaka, zaidi ya theluthi mbili ya wagonjwa hao hufariki dunia kwa kukosa huduma hiyo.

Dk. Magandi anasema wanatarajia kuanza rasmi kupandikiza uloto na maandalizi yamekamilika kwa kiwango kikubwa.

“Haya ni matibabu ya ubingwa wa juu katika kutibu magonjwa mbalimbali hasa saratani na selimundu, wataalamu wa Mloganzila tutatoa huduma hii kwa kushirikiana na wataalamu wa muhimbili – Upanga,”anasema.

Dk. Magandi anasema huduma hiyo haijawahi kutolewa popote nchini.

“Tutaanzisha hapa Mloganzila, tutashirikiana na wataalamu wa Upanga hasa upande wa vipimo vya maabara, upandikizaji utafanyika Mloganzila,”anafafanua.

Anasema wametenga eneo maalumu kwa ajili ya huduma hiyo, ambalo litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 10 kwa wakati mmoja.

VYUMBA VYA UPANDIKIZAJI ULOTO
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Mloganzila, Redemptha Matindi anasema kumetengwa vyumba maalumu vya kulaza wagonjwa, watakaofanyiwa
upasuaji wa kupandikiza uloto .

Anasema vyumba hivyo vimejengwa ndani ya wodi maalumu kwa kuzingatia usalama zaidi wa kila mgonjwa, kwani huhitaji uangalizi wa karibu kuhakikisha hali zao zinaimarika mara baada ya upasuaji.

“Si kila mtu anaruhusiwa kuingia ndani ya vyumba hivi, kuingia wodi hiyo upo mlango maalumu unaofunguliwa na
kufungwa kwa utaratibu maalumu.

“Ukishaingia hapa ndani, kila chumba kipo peke yake kwa ajili ya mgonjwa mmoja, ataruhusiwa kukaa na ndugu mmoja, kabla ya kuingia kwenye chumba cha mgonjwa kuna nafasi maalumu inazuia hewa ya nje isiingie kule kwa mgonjwa.

“Si kila mtu ataruhusiwa kuingia moja kwa moja chumbani kwa sababu kinga yake ya mwili itakuwa chini, ndiyo maana anaruhusiwa ndugu mmoja tu kukaa naye.

“Mgonjwa huhitaji msaada wa kisaikolojia, wataalamu wao watakuwa wakiingia mara kwa mara kumhudumia,”anasema.


Anasema mgonjwa hukaa wodini kwa muda wa wiki tatu, akifuatiliwa hali yake kwa ukaribu sana, ndani ya wodi hii pia kuna chumba maalumu kwa ajili ya wauguzi na kingine cha madaktari.


“Kila kitu kimewekwa na kinafanyika humu humu, kila mgonjwa atakuwa na daktari wake, ndugu atalala naye ndani,”anasema.

VIFAA TIBA
Anasema hospitali hiyo imejengwa kwa mfumo bora zaidi, hadi ndani ya wodi za kawaida mgonjwa hupatiwa msaada endapo dharura itatokea.
“Kumefungwa vifaa tiba ukutani kwa ustadi, kwa mfano (akimuonesha mwandishi wa makala haya), kuna mashine ya hewa ya oksijeni na kila kifaa kinachohitajika kumpa huduma ya dharura mgonjwa.

“Ikiwa mgonjwa atahitaji msaada anaweza (yeye au ndugu) yake kupiga simu iliyounganishwa hapa ukutani moja kwa moja pale mapokezi ya wodi na kuhudumiwa.

“Hali yake ikiimarika, ameanza kutembelea kwa kusaidiwa na ndugu, ikiwa ndugu hayupo na anataka kutembea kuna vifaa maalumu vya kumwezesha kutembea bila kuanguka,”anasema.

TAKWIMU ZA WAGONJWA
Dk. Magandi akizungumzia idadi ya wagonjwa wanaopokelewa katika hospitali hiyo, anasema imekuwa ikiongezeka kila mwaka tangu uzinduzi ulipofanyika.

Anasema hatua hiyo inaonesha ni kwa namna gani jamii imepokea huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.

“Kipindi cha robo mwaka ya kwanza (Julai – Septemba mwaka 2018) tuliona wagonjwa wa nje 17,116, kufikia robo mwaka (Oktoba – Desemba mwaka 2019) idadi imeongezeka hadi 24,945,hili ni ongezeko la kiwango cha asilimia 46 tukilinganisha na robo ya kwanza ya mwaka 2018 ilipoanzishwa,” anasema.

Dk. Magandi anasema idadi ya wagonjwa wa ndani imeongezeka katika robo ya mwaka 2019 ikilinganishwa na robo ya mwaka 2018 kwa asilimia 66.

“Idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji nayo inaongezeka kila siku, kwa sababu tumeendelea kuimarisha huduma za upasuaji ikiwamo kuongeza idadi ya watumishi,”anasema.

Dk. Magandi anasema wameongeza idadi ya wataalamu wa kutoa dawa za usingizi na kuboresha vifaa tiba vya kufanyia upasuaji.

Anasema tangu Julai – Septemba mwaka 2018 hadi Oktoba –Desemba mwaka 2019 kumekuwa na ongezeko la asilimia 90 ya
wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji katika hospitali hiyo.

“Sasa tunazidi kujikita katika kutoa huduma bobezi za upasuaji, tayari wataalamu wamefanikiwa kufanya upasuaji kupandikiza vifaa vya usikivu wagonjwa watoto waliozaliwa na matatizo ya usikivu.
“Awali, Serikali iliwapeleka nje ya nchi ambako mgonjwa mmoja hugharamiwa kati ya Sh milioni 80 hadi 100. Huduma hii ilianzishwa Muhimbili – Upanga na sasa Muhimbili – Mloganzila ipo ,” anasema.

Dk. Magandi anaeleza kuwa katika utoaji wa huduma bobezi za upasuaji wataalamu wa Mloganzila wamefanya upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo.

“Upasuaji wa aina hii unafanyika pia, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), hii ni huduma ya bobezi kwa ajili ya kutibu wagonjwa wenye uvimbe kwenye ubongo.

“Kuianzisha mloganzila maana yake tumesogeza huduma karibu zaidi na jamii, wagonjwa watano wameshanufaika,”anasema.

Reuben Razack Mkazi wa Tegeta Dar es Salaam, anasema moja ya sababu zinazowafanya wananchi kwa sasa kukimbilia huduma za afya ni mafanikio yanayoonyesha na Rais Dk. John Magufuli katika utendaji wake na uwekezaji mkubwa ulifanyika katika sekta hiyo.

“Miaka ya nyuma huwezi kwenda kwa sababu wataalamu hawakuwa na moyo wa utayari wa kumhudumia
mgonjwa, wanadai rushwa, lakini hali ilivyo sasa ni tofauti unapokelewa vizuri na
unapatiwa matibabu na bado daktari atakupigia simu kama upo nyumbani kuuliza unaendeleaje,”anaeleza.

Anasema si kwamba miaka ya nyuma watu walikuwa hawaumwi bali walikuwa wakijiuguza kwa njia za asili
kuepukana na kauli chafu za kukatisha tamaa kutoka kwa watumishi wa afya.

“Kwa hiyo unaposikia tunakimbilia Mloganzila huduma ni bora na kila mwananchi anaridhika na anachoelezwa na
watalamu,”anabainisha.

MIUNDOMBINU

Dk. Magandi anasema wanatarajia kuwa na jengo la ghorofa nne litakalokuwa malumu kutoa huduma za upandikizaji viungo mwilini ikiwamo figo, inni, mimba na viungo vingine.

“Serikali imetenga Sh bilioni nane kwa ajili ya kuanza ujenzi lakini gharama halisi zitajulikana baada ya maandalizi kukamilika, Tupo katika hatua za awali za kutengeneza mpango mkakati wa miaka mitano 2020-2025, utakaotupa mwongozo wapi tulipo, wapi tuelekee na wapi hospitali ifike katika utoaji huduma.