Home Latest News ‘HUDUMA ZIBORESHWE TRENI YA MWAKYEMBE’

‘HUDUMA ZIBORESHWE TRENI YA MWAKYEMBE’

802
0
SHARE
Abiria wakipanda treni

NA MANENO SELANYIKA,

KWA miaka mingi hapa nchini kumekuwapo na tatizo la usafiri wa nchi kavu, angani na majini hasa katika miji inayoendelea kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mingineyo. Hali hii inazorotesha ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa zima.

Miundombinu mingi hasa ya nchi kavu kama reli ilianzishwa enzi za ukoloni lakini mpaka sasa ni asilimia chache iliyoboreshwa huku nyingi ikiachwa na kutelekezwa kabisa.

Katika upande wa barabara angalau Serikali kwa kiasi fulani imejitahidi kuendeleza na kuziboresha hasa barabara kuu zinazounganisha mkoa hadi mkoa na zile za kuunganisha nchi jirani kwani idadi kubwa zimetengenezwa kwa kiwango cha lami.

Kwa mantiki hiyo RAI liliweza kuzunguka katika maeneo mbalimbali katika miundombinu ya reli iliyopo Jiji la Dar es Salaam kisha kuzungumza na watumiaji wa usafiri wa treni ya Mwakyembe iliyoanzishwa hivi karibuni kusafirisha abiria maeneo mbalimbali.

Treni za Jiji zipo mbili, ya kwanza ni treni ya Mbarawa inayoanzisha stesheni hadi Pugu wakati hii ya Mwakyembe ikianza Stesheni hadi Ubungo kwa kupitia Mabibo,Tabata, Mwananchi, Buguruni Kwa Mnyamani na Kamata.

Watumiaji wa usafiri huo hakika wamekuwa wakiufurahia usafiri huo kwa kuwa umerahisisha na kupunguza msongamano.

Mohamed Jumbe, ni miongoni mwa watumiaji wa usafiri huo ambaye anasema licha ya ubora wa usafiri huo bado changamoto ipo ya uchelewaji wa treni kufika kwenye kituo.

Anasema treni hiyo huanza safari yake asubuhi saa 12:30 hadi Saa 2:30 usiku ambapo kwa siku moja inaweza kwenda ruti kati ya tatu au nne.

“Wakati mwingine abiria tunaweza kusubiria stendi muda uliopangwa ikawa haijafika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa kama mvua kubwa ikinyesha na nyinginezo,” anasema Jumbe.

Naye mkazi wa Ubungo maziwa Rashid Mohamed, anasema treni hiyo awali ilipoanza safari zake ilikuwa inakuja hadi siku za wikendi siku ya Jumamosi lakini siku hizi haiji kabisa na kwamba hajui tatizo lipo wapi.

“Mimi nipo hapa karibu na treni ya Ubungo kwa muda mrefu sana nafanya biashara ya kuuza matofali kama unavyoona hapa, treni lazima ikija hapa niione kila wakati hivyo zamani ilikuwa inaweza kukaa siku mbili hadi tatu haiji kabisa na wala abiria hawapewi taarifa ila kwa sasa inafanya kazi vizuri,” anasema Mohamed.

Akizungumzia changamoto anazokutana nazo wakati wa kutumia usafiri huo Josephat Mwingira, anasema katika kituo kikubwa cha Ubungo Terminal hakuna huduma ya choo hivyo abiria wanaposubiria usafiri huo kwa muda mrefu hujikuta wakijisaidia sehemu ambayo hairuhusiwi.

Mfanyabiashara wa spea za pikipiki na magari Shaban Ally, anasema changamoto nyingine ni kwamba wahudumu hawana ushirikiano mzuri baina yao na abiria akitolea mfano wakiwa Posta au Kariakoo wakati wakisubiri usafiri huo endapo usipokuja kwa wakati hutangaziwa sababu ni nini lakini wanapokuwa vituo vingine hawaambiwi kitu chochote.

Naye David Chipite, anawatuhumu baadhi ya wahudumu wa treni wanaokataa kuchukua mizigo hivyo wakati mwingine inakuwa shida kwa abiria hivyo anaomba uwepo utaratibu wa kuchukua mizigo.

Akitolea mfano wa treni itokayo Ubungo hadi Posta Stesheni ambayo ina mabehewa kati ya 6 hadi 10 lingetengwa moja kwa ajili ya mizigo ya abiria.

Mkazi mwingine wa Jiji hili Ahmed Juma, anasema ajali zinazotokea husababishwa na ukosefu wa walinzi wanaotoa ishara kwa madereva wa magari wasipite kwa kuwa treni inakaribia kwenye baadhi ya makutano ya miundombinu ya reli na barabara.

Anatoa ushauri kwa Serikali iongeze reli ifike hadi Kibamba na njia nyingine iende hadi Bunju kwani huko kuna abiria wengi na kwamba itasaidia kupunguza msongamano wa magari.

Dereva wa daladala anayefanya safari zake kati ya Gongo La Mboto na Posta, Abdul Hussein, anasema tangu kuanzishwe kwa treni hiyo itokayo Pugu kupitia Kurasini hakuna tofauti.

“Abiria wanaochukua hupita katika njia yao na sisi tuna njia yetu hivyo nilitegemea labda wakati wa asubuhi au jioni nitakosa abiria lakini naona ni sawa na siku zote tu,” anasema Hussein.

Kuhusu kipato, kondakta wa daladala, Tamimu Ijumaa, anayefanya safari za Mabibo na Posta anasema kwa kiasi fulani kipato kimepungua kwa kuwa abiria wengi wanatumia usafiri wa treni.

Anasema abiria wengi ambao walikuwa ni tegemeo lao walikuwa wanaanzia safari zao kutoka Mabibo mwisho lakini kwa kuwa ufasiri wa treni hupita njia hiyo wengi hukimbilia huko.