Home Michezo Huyu hapa kinda aliyemliza Samatta Uefa

Huyu hapa kinda aliyemliza Samatta Uefa

1887
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WIKI iliyopita ilikuwa nzuri kwa mashabiki wa soka la Ulaya kutokana na uhondo wa Ligi ya Mabingwa barani humo, mechi za kwanza za hatua ya makundi zikichezwa katika viwanja mbalimbali.

Yalikuwapo mengi ya kufurahisha lakini kwa mashabiki wa kandanda nchini, jicho lilikuwa kwa Genk ya Ligi Kuu huko Ugelgiji, ambayo anachezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Genk wakiwa ugenini nchini Austria, walitandikwa mabao 6-2 na Red Bull Salzburg, siku ambayo Samatta alifunga mara moja, akiweka rekodi za kuwa Mtanzania ya kwanza kucheza na kupasia nyavu katika michuano hiyo.

Hata hivyo, kwa barani Ulaya, hakuwa Samatta, bali kinda mwenye umri wa miaka 19 katika kikosi cha RB Salzburg, Erling Braut Haland, ndiye aliyekuwa gumzo baada ya dakika 90 za mtanange huo, baada ya kufunga mabao matatu (hat trick).

Nyota huyo raia wa Norway alilitangaza jina lake, akiingia na kushika nafasi ya tatu katika orodha ya wanasoka watatu waliowahi kupachika ‘hat trick’ wakiwa na umri mdogo, akiungana na Yakubu na Wayne Rooney.

Juu ya hilo, lilikuwa bao la 17 kwa kinda huyo katika mechi tisa tu alizoichezea Red Bull Salzburg tangu kuanza kwa msimu huu.

Hii si mara ya kwanza kwake kuonesha kuwa ni adui mpya kwa walinda mlango katika ulimwengu wa soka. Mwanzoni mwa mwaka huu, akiwa na kikosi cha U-20 ya Uholanzi, alipachika mabao tisa peke yake dhidi ya Honduras.

Haland alifanya hivyo katika mtanange wa fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri huo, chini ya miaka 20, ambapo siku hiyo waliishindilia Honduras mabao 12-0.

Huenda si wengi wanaomfahamu Haland, hivyo makala haya yanakuibulia haya yanayomhusu kinda huyo aliyekuwa chachu ya kipigo cha ‘mbwa koko’ walichokipata Genk ya Samatta.

Haland anatokea katika familia ya soka. Ni mtoto wa aliyekuwa beki wa Manchester City, Alfe-Inge. Mkongwe huyo, ambaye pia alikuwa akicheza eneo la kiungo alitua Man City mwaka 2000 akitokea Leeds United.

Moja kati ya matukio ya kukumbukwa akiwa Man City ni rafu mbaya aliyowahi kuchezewa na aliyekuwa kiungo wa Man United, Roy Keane.

Solskjaer ndiye aliyemsajili Haland, wakati huo kocha huyo wa Man United kwa sasa akiinoa Molde ya Ligi Kuu ya kwao, Norway. Kipindi hicho, Haland alikuwa na umri wa miaka 16.

Kabla ya hapo, chipukizi huyo alikuwa akiichezea Bryne iliyokuwa Ligi Daraja la Pili na msimu wake wa kwanza akiwa na Molde alipasia nyavu mara 14.

Hivyo basi, ambacho mashabiki wa Man United wanatakiwa kukifahamu ni kwamba Haaland alianza kuchomoza akiwa chini ya kocha wao wa sasa, Ole Gunnar Solskjaer. Ni wakati Solskjaer akiinoa Molde ya Ligi Kuu huko kwao, Norway.

Licha ya kwamba klabu mbalimbali zinamtaka, zikiwamo Barcelona na Borussia Dortmund, baba yake anataka kuona mwanawe huyo akijiunga na Man United.

Hata hivyo, ukiachana na klabu zote kubwa barani Ulaya, Haaland ni shabiki wa Leeds iliyoko maeneo alikozaliwa. Alifichua siri hiyo mwaka juzi, aliposema anatamani siku moja aipe Leeds taji la Ligi Kuu ya England.

“Nataka sana hilo litokee. Ndoto ni kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nikiwa na Leeds. Pia, nataka kuwa mchezaji wa kiwango cha juu kama alivyokuwa mzee wangu…” alisema.

Mwisho, kati ya klabu zinazoifukuzia saini yake, itakayoweza kumnasa italazimika kuipa RB Salzburg si chini ya Pauni milioni 10 (zaidi ya Sh bil. 20 za Tanzania).