Home KIMATAIFA Huyu ndiye adui wa Rais Putin aliyenusurika kifo

Huyu ndiye adui wa Rais Putin aliyenusurika kifo

709
0
SHARE
Mwanaharakati na mkosoaji wa Serikali ya Putin, Alexei Navalny

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

SIASA za Urusi zimegubikwa na matukio ya unyanyasaji dhidi ya wale wanaojaribu kwa na namna moja au nyingine, kuinyooshea kidole serikali iliyoko madarakani chini ya Rais Vladimir Putin.

Hivi karibuni, habari iliyotikisa ulimwengu ni lile la kiongozi wa upinzani kunusurika kifo baada ya kuwekewa sumu katika chai.

Ni Alexei Navalny mwenye umri wa miaka 44, mwanaharakati ambaye kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji ‘mzuri’ wa Serikali ya Rais Putin.

Siku ya tukio Agosti 20 mwaka huu, Navalny anayesifika kwa kulaani vitendo vya rushwa anavyosema vimeshamiri chini ya utawala wa Rais Putin, aliugua ghafla akiwa kwenye ndege.

Hiyo ilisababisha ndege itue kwa dharura mjini Omsk na ndipo mwanaharakati mwenzake, Kira Yarmysh aliposema wamehisi sumu ilikuwa kwenye chai aliyokunywa.

Bila hofu yoyote, Navaly amekuwa akiongoza maandamano nchini humo kwa kile alichodai utawala wa Putin ni genge la wezi linalopaswa kuondoshwa haraka iwekezekanavyo.

Hata hivyo, siku zote ndoto yake iliyokwama ni kutumia boksi la kura kumng’oa madarakani Rais Putin.

Mwaka juzi, alichukua fomu ya urais lakini aliishia mlangoni baada ya kuwekewa kigingi. Kuelekea uchaguzi, alifunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, hivyo mahakama kumng’oa katika kinyang’anyiro cha kuifukuzia Ikulu.

Kutokana na ukosoaji wake, wengi walishangaa kuona bado anatembea uraiani bila kudhuriwa na mamlaka za Urusi.

Hiyo ilitokana na ukweli kwamba kumekuwapo na uadui mkubwa kati ya serikali ya nchi hiyo na wakosoaji.

Hata yeye, Navalny hii ni mara ya pili kunusurika kifo kwa staili hii kwani mwaka jana alikula kitu kilichotajwa kuwa na sumu akiwa ameshikiliwa na polisi.

SAFARI YAKE ILIANZIA WAPI?

Juni 4 mwaka 1976, ndiyo siku aliyozaliwa katika eneo liitwalo Obninsk, mji ulioko Kusini-Magharibi mwa Moscow.

Alipata shahada za sheria na fedha, zote akitunukiwa katika vyuo vikuu vya nchini Urusi. Navalny aliingia katika siasa mwaka 1999, kipindi ambacho Rais Putin alichaguliwa kwa mara ya kwanza, akijiunga na chama cha upinzani cha Yabloko.

Hata hivyo, chama hicho kilimtimua mwaka 2007 kutokana na misimamo yake, hasa kwa kitendo cha kushiriki maandamano ya kumpinga Rais Putin.

ALIPATAJE UMAARUFU?

Jina lake lilianza kuitikisa Urusi mwaka 2008, apoanzisha ‘blogu’ (aina ya mtandao wa kijamii) iliyojikita katika kufichua vitendo vya kiuhalifu na rushwa vilivyokuwa vikifanywa na taasisi za serikali.

Moja ya mbinu alizokuwa akitumia kupata taarifa ni kujifanya mwekezaji katika kampuni kubwa za mafuta, hivyo kutumia nafasi hiyo kuingia na kuchunguza ‘uhuni’ uliokuwa ukiendelea.

Baada ya kujipatia jina, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuachana na taasisi za serikali na kukita mizizi ndani ya Chama tawala, United Rusia, na hapo akawa ameingia rasmi kwenye ‘18’ za Rais Putin.

Katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 2011, alitibua mambo zaidi alipotumia blogu yake kuwaambia wananchi wapigie kura chama chochote lakini si United Rusia cha Rais Putin, akikitaja kuwa ni genge la wezi.

Mara zote katika mahojiano yake, Navalny alisistiza kuwa anataka kuing’oa serikali inayoruhusu asilimia zaidi ya 80 ya utajiri wa Urusi kumilikiwa na kikundi kidogo cha watu.

Haikuzuia United Russia kushinda, ingawa ulikuwa ni ushindi kiduchu, tena ukitajwa kuchagizwa na wizi wa kura, hata kusababisha maandamano makubwa jijini Moscow na maeneo mengine.

Misukosuko gani amekutana nayo?

Maandamano hayo ya Desemba 24 mwaka 2011 hayakumwacha salama Navalny kwani alikamatwa na kuswekwa gerezani kwa siku 15.

Huku Rais Putin akishinda, Navalny alifunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi, hata wakati fulani kesi hiyo ikiongezewa walakini wa elimu yake ya sheria.

Julai mwaka 2013, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani, adhabu ambayo hata hivyo ilihisiwa na wengi kuwa ilisukwa kisiasa.

Kabla ya kumaliza adhabu, ilishangaza kuona akiruhusiwa kutoka na kwenda kwenye kampeni za kugombea nafasi ya meya wa Moscow, ambapo alishika nafasi ya pili nyuma ya mshirika wa Rais Putin, Sergei Sobyanin.

Kwa wengi, huo ulikuwa ni ushindi mkubwa kwani hakuwa akiruhusiwa kutumia televisheni katika kampeni, bali simu na maneno ya mdomo tu.

Alipoachiwa, alidakwa tena mwaka 2017 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano, safari hii ikionekana wazi ni mpango uliosukwa kumtoa katika mbio za urais wa mwaka mmoja baadaye.

NI SUMU GANI ILIYOKARIBIA KUMUUA?

Kwa mujibu wa taarifa, ni kemikali inayopatikana kwenye dawa za wadudu na ndiyo iliyowahi kutumika katika jaribio la kumuua aliyekuwa kachero wa Urusi, Sergei Skripal, sambamba na binti yake,Yulia, tukio lililotokea mwaka juzi.

Dhidi ya kachero huyo, ilikuwa mara ya kwanza kwa sumu hiyo kutumika tangu Vita ya Pili ya Dunia ilipomalizika mwaka 1945.

WENZAKE WALIKUTANA NA MATESO GANI?

Kama ilivyoelezwa awali, utawala wa Rais Putin umejijengea taswira mbaya kwa matukio ya ukandamizaji dhidi ya wakosoaji wake.

Miongoni mwa wakosoaji waliowahi kukutana na makali ya utawala wa Rais Putin ni Vladimir Kara-Murza, ambaye alinusurika kifo baada ya majaribio mawili ya kulishwa sumu.

Boris Nemtsov, kiongozi mwingine wa upinzani kabla ya Navalny, ambaye alipigwa risasi mwaka 2015.

Mwingine ni Alexander Litvinenko, kachero aliyelishwa sumu jijini London mwaka 2006 na mmoja kati ya washukiwa wa kifo chake alipata ubunge mwaka mmoja badaye, kabla ya kupewa tuzo ya nishani na Rais Putin.

NANI ALAUMIWE?

Mataifa ya Ulaya, sambamba na Marekani, yamekuwa yakilaaniwa kwa kushindwa kupazia sauti kile kinachoendelea Urusi dhidi ya wanaharakati wanaokinzana na utawala wa Rais Putin.

Mathalan, katika miezi ya mwanzo wa utawala wake madarakani, Rais Donald Trump aliulizwa juu ya msimamo wa mataifa makubwa kwa kile wanachofanyiwa wakosoaji nchini Urusi. “Wauaji wako wengi. Unafikiri nchi yetu nayo iko safi?” alihoji Rais Trump.

Akitoa maoni yake kupitia mahojiano aliyofanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Navalny alisema: “Nataka wanaojihusisha na rushwa na ukandamizaji wa wanaharakati wazuiwe kuingia kwenye nchihizo (za Ulaya), wanyimwe viza.”