Home Habari Huyu ndiye Magufuli wa maamuzi magumu

Huyu ndiye Magufuli wa maamuzi magumu

1315
0
SHARE

BAKARI KIMWANGA

DHANA ya maamuzi magumu ni kitendo cha kuamua kufanya jambo fulani, ambayo msingi wake huleta matokeo chanya kutokana na kile unachokiamini.

Watu wengi hususani wapinzani wa Rais Dk. John Magufuli, wamekuwa wakitumia muda mwingi kuponda kila jambo linalofanywa na Serikali.

Na hata sasa wamekuwa wakishindwa kuelewa kuwa maamuzi magumu si tu hufanyika bali utekelezaji wake hufanyika kwa masilahi ya kulinda jamii au jambo fulani muhimu kwa masilahi ya watu wote katika Taifa.

Binafsi nimekuwa nikitafakari kwa kina hatua ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli hasa kwa staili yake ambayo imekuwa tofauti na yenye manufaa kwa umma.

Kwa muda wa miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli, sasa tunashuhudia nchi ikipita kwenye njia iliyonyooka huku tukisahau kwamba miongoni mwetu eti tulikuwa na msamiati wa ‘Tanzania inataka Rais mkali na si nyoronyoro’

Naam sasa hili limekuwa likitekelezwa sasa kwa kasi ya ajabu ikiwamo tukishuhudia kila kona miradi mikubwa ya maendeleo tena iliyopewa jina la miradi ya mkakati.

Leo sekta ya miundombinu imekuwa iking’ara kwa kila Mtanzania kufurahia thamani ya fedha yake, ambapo mtandao wa barabara umeimarika katika kila pembe ya nchi.

Ninakumbuka Magufuli huyo wa maamuzi magumu, akiwa Waziri wa Ujenzi moja kati ya mkakati wa wake ulikuwa ni kuhakikisha mikoa kwa mikoa inaunganishwa na mtandao wa barabara huku makao makuu ya mikoa ikipendezeshwa kwa kuwa na lami.

Kwa Jiji la Dar es Salaam, eneo la kwanza la mfano kwa kuwa na mtandao mzuri kwa wakati huo, mfano ulikuwa ni Manispaa ya Ilala tena wakati huo mbunge akiwa Mzee Idd Simba kabla ya kupokewa kijiti na Mussa Zungu ambaye anahudumu kwenye jimbo hilo hadi sasa.

Ninakuelewa Mzee wangu kama wanaokuita wewe dikteta wewe endelea na wakuite kila aina ya majina lakini kama kujenga barabara za kila eneo, Fly over ya Ubungo, mtandao wa maji, ruzuku ya Sh bilioni 23 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure.

Rais Magufuli ameonekana kuwa ni kiongozi anayetoa maamuzi ya haraka na magumu, ambayo wengine yaliwashinda ikiwamo hata tu kupambana na suala la watumishi hewa na hata kuwaachisha au kuwasimamisha kazi watendaji wanaokengeuka katika dhamana walizopewa.

Mwaka jana, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishwaji wa madini yasiyo chenjuliwa mpaka pale kodi za nyuma ziwe zimelipwa, kwangu huu ni uamuzi mgumu ambao wengine wangehofu kwa kile wanachoita diplomasia ya biashara bila kuangalia masilahi mapana ya nchi yetu.

Pia hatua hiyo ilikwenda sambamba na uamuzi mgumu wa Serikali ya Rais Magufuli wa kuweka mpango wa utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia yaani Smelter, hapa nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato na kutengeneza mapato kwa Watanzania.

Sasa nchi inashuhudia namna majengo ya masoko ya madini yetu kwa kila mkoa, ambapo kwa sasa wachimbaji wamekuwa wakiuza madini yao na kuona faida ya kazi wanayoifanya.

Watanzania tumeshuhudia historia kubwa ikiandikwa chini ya Rais Dk. John Magufuli baada ya kufanyika kwa tukio la utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji kati ya Tanzania na Misri ambao umesubiriwa kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Juni mwaka huu Serikali iliwasilisha bajeti ya nne ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015, ikitanguliwa na ya mwaka 2016/17 iliyokuwa ya Sh trilioni 29.5, 2017/18 Sh trilioni 31.7 na 2018/19 Sh trilioni 32.

Katika wizara zote ambazo ziliwasilisha mapendekezo yake, wizara ambayo imeonesha bajeti yake kuwa ni kubwa ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyoidhinishiwa Sh trilioni 4.9.

Mradi mwingine mkubwa wa Rais Magufuli ikiwa ni ya tatu miongoni mwa maeneo yaliyotengewa fedha nyingi ni Julius Nyerere Hydroelectric Dam ikifahamika zaidi kama mradi wa umeme wa maji unagharibu Sh trilioni 1.44 hadi kukamilika kwake.

Elimu, maji na afya inachukua nafasi ya nne, tano na sita baada ya Bunge kupitisha Sh bilioni 863 (elimu), Sh bilioni 611 (maji) na Sh bilioni 547 (afya). 

Kiasi cha Sh bilioni 500 imepitishwa kwa ajili ya Air Tanzania Company Limited (ATCL) ikiwa ni nia ya Rais Magufuli kufufua shirika hilo, ambapo sasa nchi inashuhudia anga likitabasamu kwa kumuona Twiga wetu ‘akipaa mawinguni’ kwakuwa kieleleni zaidi.

Kwangu ninaita uamuzi mgumu pale nionapo namna umeme vijijini unaposambaa kwa kasi ya ajabu huku REA kwa kushirikiana na Tanesco wakiwa na nguvu ya pamoja kuchochea umuhimu wa nishati na uanzishwaji wa viwanda vidogo.

Hayo hayafanyiki tu bali yanafanywa kwa mkakati maamulu wa kumfikia Mtanzania wa kawaida kule kijijini na kutokana na umuhimu huo na utekelezaji wa Rea III zaidi ya Sh bilioni 363.11 zimetengwa katika kutekeleza mradi huo.

Leo Jiji la Dar es Salaam ni kati ya majiji sita yaliyoko hapa nchini ambapo ni la kwanza lenye idadi kubwa ya watu, ambapo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ilikuwa na watu 4,364,541 kati ya watu 44,928,923 nchi nzima.

Kutokana na wingi huo wa watu, jiji hilo limekuwa na changamoto nyingi kama vile foleni za magari, miundo- mbinu hafifu pamoja na baadhi ya maeneo kuathirika na mafuriko katika kipindi cha mvua.

Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ipo katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu katika jiji hilo.

Ujenzi unaofanyika kwa mafungu kumi ambao ujenzi huo, ulianza rasmi mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Ujenzi unaofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya jiji ambazo zinajengwa sambasamba na mifereji ya maji, taa za barabarani za sola, madaraja, masoko ya kisasa ambayo pia yatakuwa na huduma za kibenki pamoja na vyoo vya umma.

Leo kupitia DMDP Dar es Salaam inang’ara hebu pita barabara ya Tandale kwenda Magomeni hasa nyakati za usiku utafikiri upo nchi za ulaya kumbe ‘nyumbani kwetu Tandale’ na hata unapofika pale maaarufu kwa ‘mahakama ya simu’ kwa Mtogole huwezi amini.

Ndio huwezi amini kwa sababu mazingira yamefanya makundi ya vijana hasa waliokuwa wamezoa kupiga debe na kupewa chochote kubadili mwelekeo na sasa wengi wao kujikuta wakigeukia shughuli za kiuchumi.

Namuona Rais Magufuli ni mwenye uamuzi mgumu kwa sababu amebadili mwekelezo na taswira ya nchi ya kufikia sasa watu kuheshimiana na kuulizana namna bora ya kuyaendea maisha badala ya kukaa kusubiri kesho itakuja nyingine.

Septemba 22, mwaka huu Taifa likashuhudia tena uamuzi mgumu wa Rais Magufuli kwa kuamua kumshauri Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwamba mahabusu wa makosa mbalimbali hasa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha walizotakatisha, wasikilizwe ndani ya siku saba.

Kila mara mkuu huyo wa nchi amekuwa akirejea kauli yake kwamba hapendi kuongoza taifa la watu wenye machungu hususan waliopo magerezani huku akitamani siku moja kusiwe na mahabusu wala wafungwa.

Ninajua mzee huyo wa maamuzi magumu kwa vitendo ni mwenye kuumia na akisema anamaanisha kwamba amesimamia ule usemi kwamba  wanaokwenda jela si wote wenye hatia.

Hakika kwa kukiri kwao kwa namna moja ama nyingine, leo Serikali imekusanya zaidi ya Sh bilioni 40 pamoja na ahadi kutoka kwa watuhumiwa hao na ninaamini fedha hizo zinakwenda kutekekeza miradi ya maendeleo.

Tunapokuwa na uchovu na kukata tamaa katika uamuzi wetu, tunaweza kujua kwa ujasiri kwamba tunamtumikia Mungu ambaye anajua kile tunachopitia sisi kama Taifa.

Hakika Rais Magufuli, nafsi yangu inajiambia kwamba wewe ni kiongozi mwenye maamuzi magumu ili mradi tu yana masilahi kwa umma, hakika tupe neema ya leta neema ya maendeleo Watanzania si wajinga naona na kushuhudia na hakika jasho lako halitovuja bure kwa nchi yetu.