Home Makala ICC, Marekani vita ya mwili, kivuli

ICC, Marekani vita ya mwili, kivuli

164
0
SHARE
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo.

NA HASSAN DAUDI

KITENDO cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), kuinyooshea kidole Marekani na kutaka ichunguzwe kimesababisha mtikisiko wa aina yake katika siasa za kimataifa.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, alisema Marekani inatakiwa kuchunguzwa kwa kile alichodai wanajeshi wake walifanya vitendo vya kihalifu wakati wa vita nchini Afghanistan.

Kipindi kinachozungumziwa hapo ni kuanzia mwaka 2003 hadi 2004, ambapo maelfu ya watu (raia wa Afghanistan) si tu walipoteza maisha na wengine kuhama makazi, pia walikumbana na mateso makali, vikiwamo vitendo vya udhalilishaji, mathalan wanawake kubakwa.

Haikuishia hapo, bali pia ICC ‘imewapapasa’ washirika wakubwa wa Marekani, Israel, ikisema unahitajika uchunguzi kwani kuna shaka kuwa huenda kulikuwa na vitendo vya uhalifu wakati Wayahudi walipolazimisha kukaa West Bank na East Jerusalem.

Kufuatilia kauli hiyo ya ICC kutaka ufanyike uchunguzi utakaohitimishwa na adhabu endapo Marekani itakutwa na hatia, nchi hiyo kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo, iligeuka mbogo ikionya isitokee ikaguswa na mahakama hiyo kwa namna yotote ile.

Kama ujumbe huo hautoshi, wiki iliyopita Marekani ilipiga hatua moja zaidi kwa kumwekea vikwazo mwanamama Bensouda, raia wa Gambia mwenye umri wa miaka 59.

Hatua hiyo ilikwenda sambamba na hatua ya Marekani kutoa onyo kali kwa yeyote atakayeshirikiana na ICC katika kulichunguza taifa hilo lenye uchumi mkubwa.

Kwa mujibu wa vitisho vya Pompeo, upande utakaoungana na ICC katika uchunguzi dhidi ya nchi yao, basi utakumbana na makali ya kuwekewa vikwazo.

Alichokisema Pompeo wakati huo ni kwamba mshirika wa ICC katika uchunguzi atajikuta akizuiwa kuingia Marekani, sambamba na kutaifisha mali zake zote zilizoko nchini kwao.
Hata hivyo, mvutano wa ICC na Marekani umenifikirisha kiasi, hata kuukumbuka msemo wa mtaani, kwamba kinyago ulichokichonga hakiwezi kukutisha! Vilevile, hutakuwa umekosea kuufananisha mvutano huo na mtu anayepigana na kivuli chake.

Ndiyo, unapowazungumzia waasisi wa Mahakama hiyo, Marekani ni mmoja wao na nitakupa kisa hicho kilichoanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Marekani, sambamba na nchi zingine zilizokuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa, walikutana mjini Roma, Italia, ambako baada ya mabakubaliano ulisaini mkataba wa kuianzisha ICC.

Ilipofika mwaka 1998, Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton, Marekani ilithibitisha kutokuwa ndani ya ICC. Haikuwa Marekani pekee, bali na nchi zingine sita (China, Iraq, Israel, Libya, Qatar na Yemen).

Licha ya kuwa nje ya ICC kwa kipindi chote, bado Marekani haikuacha ‘kujipendekeza’ kwa kushiriki shughuli mbalimbali za taasisi hiyo.

Katika ukaribu wake huo na ICC, ilishuhudiwa namna Marekani, licha ya kutokuwa mwanachama, ilivyokuwa ikishiriki katika operesheni zake, ikiwamo kuwasulubu kwa kuwawekea vikwazo wale waliokuwa wakiitwa wahalifu na mahakama hiyo.

Kutolea mfano, wengi hawatakuwa wamesahau Marekani ikiwa nje ya nchi 123 zilizo chini ya ICC, ilivyowashughulikia watu wa karibu wa rais wa Syria, Bashar al-Assad.

Kama hiyo haitoshi, kama si kufuatilia kwa karibu, basi walau tulibahatika japo kuona namna Marekani ilivyokuwa mstrari wa mbele kuisaidia ICC katika uchunguzi wake dhidi vikundi vya kigaidi vya Taliban huko Afghanistan.

Pia, huku hiyo ikiwa ni kazi ya ICC, haijasahaulika kuwa Marekani ilijitosa kumsaka kila kona aliyekuwa mhalifu wa kivita wa Uganda, Joseph Kony, hata kufanikisha kukamatwa kwake mwaka 2005, akikabiliwa na makosa ya kuingiza watoto katika utumwa wa kingono.

Mwendesha Mashitaka wa ICC aliyewekewa vikwazo na Marekani, Fatou Bensouda.

Ni kama ambavyo Marekani haikubaki nyuma kuhakikisha aliyekuwa kiongozi wa waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Bosco Ntaganda.

Aidha, bado Marekani haijasahaulika kwa ushiriki wake katika kumkamatana na kumfikisha mikononi mwa ICC kiongozi mwingine wa waaasi DRC, Dominic Ongwen.

Yote kwa yote, yatosha kusema hii ya safari hii, kwamba sasa ICC inataka Marekani ichunguzwe, haina tofauti na mtoto anayemfunga baba yake aliyemkuza na kumsomesha kwa tabu kabla ya kupata kazi ya uanasheria.

Kabla ya ICC kuingia safari hii, Marekani ilikuwa na nafasi nzuri ya kumaliza hili lakini kwa jicho la tatu, haikuonekana kulipa nguvu ya kutosha.

Unaweza kusema hivyo kwa sababu mara kadhaa Marekani iliutangazia ulimwengu kuwa inafanya uchunguzi dhidi ya wanajeshi wake waliokuwa Afghanistan, ili kuwabaini na kuwaadhibu wale waliokengeuka na kufanya uhalifu wakiwa kwenye nchi hiyo ya Kiarabu.

Itakumbukwa ilikuwa hivyo mwaka 2009, ambapo ulimwengu uliendelea kusubiri majibu ya uchunguzi lakini hakuna kilichotokea hadi leo hii.

Wakati huo huo, mengi yanaweza kusemwa juu ya ICC na Marekani lakini ni ngumu kutoutaja utawala wa Rais Donald Trump unapozungumzia kuyumba kwa uhusiano wa pande mbili hizo.

Mengi yalishuhudiwa mwaka juzi, ambapo baada ya aliyekuwa Mshahuri wa Usalama wa Taifa, John Bolton, alisema hawatashirikiana na ICC, kauli iliyoungwa mkono na Rais Trump wiki mbili baadaye.

Ilipofika Machi 15 mwaka jana, akasikika Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo, akiutangazia ulimwengu kuwa nchi yao itazuia maofisa wa ICC kuingia nchini kwao.
Siku mbili baadaye, Pompeo aliwatishia hadharani maofisa wawili wa ICC kwa kile alichosema atawafanyia kile anachoona kina masilahi mapana kwa taifa lake.

Rais Trump aligongelea msumari Juni 11 mwaka huu, alipoagiza mali za maofisa wa ICC zilizokoko Marekani ziwekwe chini ya ulinzi, sambamba na kuzuia familia zao kuingia nchini kwake.

Ilipofika Septemba 2 mwaka huu, ndipo sasa ilipotangazwa rasmi kuwa Marekani imemuwekea vikwazo Mwendesha Mashitaka Mkuu, Bensouda, sambamba na ofisa mwingine wa ICC, Phakiso Mochochoko.

Akilizungumzia hilo, Oumar Ba ambaye ni mwandishi wa vitabu na mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Morehouse nchini Marekani, anasema utawala wa Rais Trump umevuka mpaka kwa ICC.

“Ingawa marais wengine wa Marekani wamekuwa wakijitoa kwenye Mahakama, hakuna aliyeenda mbali kama hivi (kuwekea vikwazo maofisa wake),” anasema Oumar Ba.
Licha ya kuyumba kwa uhusiano wake na Marekani, je, ICC nayo ni safi kiasi gani? Kwanini imekuwa ikioneka kuwa na ukakasi machoni mwa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa?

Ukweli usiopingika, taasisi hiyo nayo imeingia kwenye kashfa mara kadhaa, hata kuifanya ionekane ya kutilia shaka machoni mwa baadhi ya wakosoaji.

Ukianzia kwa aliyekuwa rais wake, Silvia Fernandez de Guemendi, mwendesha mashitaka wa zamani, Luis Moero Ocampo, na hata huyu wa sasa, Fatou Bensouda, hakuna aliyeweza kuepuka kashfa na kuitwa msafi.

Mathalan, kile kilichowahi kuripotiwa na moja ya vyombo vya habari ni kwamba Fernandez aliipata kwa hila nafasi ya kuingia ICC.

Hapo, ikaelezwa kuwa mwanamke huyo alishikwa mkono na aliyekuwa rais wa Argentina, Cristina Kirchner, sambamba na wanasaisa wenye ushawishi mkubwa Venezuela, Hugo Chavez (sasa marehemu) na Maduro.

Ukija kwa Ocampo, zikiwamo kashfa za kupokea rushwa na kuwa na akaunti za siri ili kukwepa kodi. Pia, mwanasheria huyo raia wa Argentina alinyooshewa kidole cha lawama, akitajwa kumpendelea rafiki yake, bilionea wa Libya, Hassan Tatanaki na kuyaweka nyuma masilahi mapana ya ICC.

Kwa upande wa Bensouda, unaanza na kashifa zote za Ocampo, kwamba huwezi kumtenganisha nazo kwa kuwa ndiye aliyekuwa mshahuri wake wa karibu. Hayo ni yeye na bosi wake.

Aidha, zimekuwapo kelele nyingi za ukosoaji dhidi ya Bensouda, zikiwamo hizi za hivi karibuni alipotangaza kufutilia mbali uchunguzi dhidi ya Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Katika hilo, Bensouda aliyekuwa msaidizi wa Mwenedesha Mashitaka wa ICC kuanzia 2004 hadi mwaka 2012 alipokwaa kiti cha bosi wake huyo, anaingia kwenye lawama za ‘kumlinda’ kiongozi huyo, jambo linalotajwa kuwa ni kukiuka maadili ya majukumu yake ndani ya ICC.

Wakosoaji wake wanasema hakuna sababu ya ICC kutomfikisha kizimbani Maduro ikiwa tayari kuna malalamiko zaidi ya 110 dhidi ya utawala wake nchini Venezuela.

Wakati huo huo, Bensouda ni mlengwa wa madai mazito, kwamba hata yeye alishiriki kwa kiasi kikubwa katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu akiwa kwao, Gambia.

Wanaosema hivyo wanadai kuwa alishiriki katika matukio mengi ya uvunjifu wa haki wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Gambia na hata pia alipokuwa Waziri wa Sheria kuanzia mwaka 1998 hadi 2000.

Zaidi ya hizo zinazowagusa watu, pia kama taasisi, ICC nayo imekuwa ikinyooshewa kidole cha lawama, ikitajwa kutupa jicho zaidi kwa viongozi wa Afrika, kana kwamba nchi za Ulaya na Marekani hazina matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kutokana na dhana hiyo ya ICC kujifanya haioni uhalifu unaofanywa na viongozi wa nchi za kizungu, imebaki kwenye kumbuku namna Umoja wa Afrika (AU) ilivyowahi kutishia kulitenga Bara hili na taasisi hiyo.

Huku Rais wa Afrika Kusini wakati huo, Jacob Zuma, akiita ICC kuwa ni minyororo ya wakoloni dhidi ya Afrika, itakumbukwa alivyoitisha mkutano maalumu wa AU uliofanyika Oktoba 13 mwaka 2015.

Kinyume cha matarajio ya Zuma, kwamba AU ingepitisha hilo na kisha nchi wanachama kujitoa ICC, hoja yake ilikosa sapoti ya kutosha.

AU ilifeli katika hilo lakini kwa kiasi kikubwa iliamsha vuguvugu dhidi ya ICC. Ni mwaka mmoja tu baadaye, Burundi ilitangaza kuwa ingejitoa baada ya Mahakama hiyo kuanza upelelezi dhidi ya vurugu za kisiasa zilizotokea nchini humo.

Hazikupita wiki mbili, zikaibuka Afrika Kusini na Gambia, kila moja ikianika dhamira yake ya kujiweka kando na Makama hiyo, tishio ambalo pia lilisikika Kenya na Namibia.

Hoja kubwa ya nchi hizo ilikuwa ni kwamba wahanga wakubwa wa hukumu za ICC ni viongozi wa Afrika. Hilo moja. Pili, Mahakama hiyo imefumbia macho upelelezi dhidi ya uhalifu mkubwa wa Iraq kuvamiwa na Marekani mwaka 2003.

Mwisho, ni kwa maana hiyo basi, hatua ya ICC kuigeukia Marekani inaweza kuanza kurejesha imani yake kwa mataifda ya Afrika na mengine machanga duniani kote.

Licha ya wengi kuiona kwa jicho hilo, Gambia, ambako ndiko anakotokea Mwendesha Mashitaka aliyewekewa vikwazo, Bensouda, wameibuka na kuiomba Marekani kujifikiria mara mbili, kama si kuacha vikwazo vyake dhidi ya ICC. Ombi hilo pia limetumwa na Ujerumani.

Sambamba na kuitaka Marekani ifutilie mbali hatua hiyo, pia Ujerumani ilisisitiza kuwa itaendelea kuwa sehemu ya kufanya kazi kwa karibu na ICC. Alichokisema Waziri wa Mambo ya Nje ni kwamba, Ujerumani ina imani na kazi inayofanywa na ICC na inaichukulia Marekani kuwa imefanya kosa kubwa.