Home Latest News IEBC wang’atuke ili Kenya itulie

IEBC wang’atuke ili Kenya itulie

913
0
SHARE

Rais Uhuru KenyattaNa Franklin Victor,

WAKATI maaandamano ya wananchi wa Kenya kupinga uwepo wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka – IEBC (The Independent Electoral and Boundaries Commission), hayajafika tamati, tayari vifo, majeruhi na uharibifu wa mali vimeshatokea.

Ukiacha Wakenya na maandamano yao kuikataa IEBC, Waafrika wengine katika nchi mbalimbali, ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC na Guinea Bissau kama mfano, wanaandamana kushinikiza matakwa, mahitaji, maamuzi na matarajio yao kuheshimiwa, kukidhiwa na wanasiasa walioko madarakani.

Waandamanaji hawa wa Kiafrika ni ishara mbaya kwa baadhi ya viongozi wa Kiafrika waliokengeukia madarakani ambao kama wanazisoma vyema alama za nyakati hawana budi kubadilika, kujirekebisha mapema kabla hayajawakuta malipo stahiki ya udhalimu ambayo kwa bahati nzuri siku hizi yanalipwa hapa hapa Afrika, au Kimataifa endapo malipo halisi kupitia vyombo vya kitaifa yanashindikana.

Kiongozi wa CORD, Raila Amolo Odinga almaarufu Baba, anasisitiza ili uchaguzi mkuu ujao Kenya uwe wa huru, haki, wazi na wa kidemokrasia ni lazima IEBC hii na makamishna wake kwa pamoja watumbuliwe ama wajitumbue. Raila na viongozi wenzake wa upinzani wanasema IEBC haiaminiki na haiwezi kutenda haki kama itaachwa kusimamia uchaguzi mkuu ujao.

Inasemwa makamishna wa IEBC wanaegemea upande mmoja ambao si wa demokrasia hivyo kujikosesha sifa muhimu ya kuwa mlinzi, msimamizi na mtendaji wa demokrasia huru. IEBC haina utashi huru badala yake imebeba utashi wa kisiasa kwa kujipa hadhi sawa na wanasiasa ndani ya uwanja wa siasa.

Raila (Baba) licha ya kushambuliwa binafsi kwa kila namna, ameendelea kujikita katika hoja kuu ya msingi juu ya kwanini IEBC inalazimu kuundwa upya ili kukidhi matakwa ya demokrasia na kuwezesha uchaguzi mkuu 2017 kuwa wa huru, haki na wazi.

Kwa upande mwingine, viongozi wengi wa muungano wa Jubilee wanatetea uwepo wa IEBC na wanataka iachwe kama ilivyo na ikiwezekana ndiyo iusimamie uchaguzi mkuu ujao. Miongoni mwao, Seneta wa kuteuliwa wa Kanti ya Mombasa Ema Mbura anatetea kwa shinikizo uwepo wa IEBC ingawa kwa maoni ya baadhi ya watu wanaomsikiliza wanadai utetezi wake una maslahi, tashwishi ambayo naikubali.

Yawezekana seneta Mbura anajua yakifanyika mabadiliko na kupatikana IEBC mpya, uchaguzi ukaendeshwa kwa uwazi, uhuru na haki basi wanasiasa wengi wanaoyatumia madaraka ya kisiasa kwa maringo dhidi ya Wakenya hawatayapata tena baada ya 2017, hawatachaguliwa wala kuteuliwa.

Mbura na wanasiasa wenzake wa Jubilee wanasemwa kujivunia wingi wao katika maamuzi ya kimaslahi hivyo kutojali wengine wenye hoja thabiti huku wakiendekeza mbinu mbadala kuupaka matope upinzani ili uonekane kwamba hauna uzalendo, hauitakii mema Kenya!

Pia, kuna dalili ujinsia,,kama ilivyo kwa ukabila, kutumika kama kete muhimu lakini itakayotumiwa ndivyo sivyo katika siasa za Kenya kama itakavyokuwa katika nchi nyingi za Afrika siku za usoni.

Seneta maalumu Mbura ndiye mwaka jana alipendekeza wanawake wa jamii ya Mijikenda warudie enzi zao za kutembea uchi ili eti kuvutia utalii na watalii maeneo ya Pwani Mombasa!

Cord, licha ya kusisitiza msimamo wao juu ya IEBC wamesikika wakisema wako tayari kwa mazungumzo na Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta kwa sharti yahusishe wadau wote, si shinikizo la wanasiasa wa Jubilee pekee.

Maoni ya wanaharakati na wasomi hayatofautiani sana na msimamo wa Cord; na jambo muhimu ni kwamba wananchi, Cord, wanaharakati, viongozi wa kidini na kadhalika kwa wingi unaoshawishi wanaungana kuikataa IEBC iliyopo sasa.

Hili linathibitisha Wakenya wengi, pasi kujali kete hasi ya ukabila inayotumiwa na baadhi ya wanasiasa kupotezea watu lengo ili wasijadili mambo muhimu na kufanya maamuzi ya msingi, wanataka IEBC itwangwe, ing’oke, iondoke zake!

Kama hali ni hii, kwanini basi makamishna na mwenyekiti wa IEBC wasijiuzulu, wasijiondoe wenyewe na kuepusha shari kamili? Kwanini IEBC wasiione mantiki ya uzalendo kwa kujiuzulu sasa na kuiepusha nchi na mvua ya mawe ya migogoro itakayozalishwa na wingu zito la balaa linaloonekana kuielekea anga ya siasa ya Kenya!

Binafsi naamini, hapana nahisi, IEBC wataiona mantiki ya kutanguliza maslahi ya Kenya mbele, na kama wanajali mustakabali wa nchi yao hawatang’ang’ania kubaki ofisini wakati hawaaminiwi, hawatakiwi, hawakidhi mahitaji ya kidemokrasia ya Wakenya.

Raila Baba anajua wazi Kenya imara itajengwa, tuseme itakarabatiwa, na Wakenya imara kupitia maamuzi imara ya kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Raila anaelewa anapendwa na nguvu zilizo nyuma yake ndizo msukumo wake kuyaelekea mabadiliko wayatakayo Wakenya; na sauti za wafuasi wake, wananchi wake zinalazimu kuakisiwa kwa nguvu stahiki kupitia yeye na viongozi wengine wa kisiasa wanaopaswa kuyaweka maslahi ya taifa mbele akiwemo rais Uhuru Kenyatta aliye na dhamana kuu ya nchi, mamlaka na wajibu kwa Wakenya wote.

Kenya ndilo taifa tajiri kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na ni kati ya nchi za Afrika zinazotajwa kuwa tajiri. Athari yoyote kisiasa itakayohatarisha utulivu na amani vya nchi itaathiri vilivyo uchumiwa Kenya hivyo kuathiri pia uchumi wa nchi jirani zinazoizunguka hususan washirika katika jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC yenye nchi nyingine za Uganda, Tanzania, Rwanda, Sudani Kusini na Burundi.

                                                0772 066 667.