Home Makala Ijue Dar es Salaam ya miaka ya 60 na 70

Ijue Dar es Salaam ya miaka ya 60 na 70

1212
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Wakati naingia Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mapema 1969 idadi ya wakazi wake ilikuwa takriban watu 350,000 – yaani chini ya asilimia 10 ya wakazi waliopo sasa hivi. Sensa ya mwaka 1967 (sensa ya kwanza baada ya kupata uhuru wetu) ilionyesha Dar es Salaam kuwa na wakazi 272,821.
Miundombinu – kwa maana ya barabara ilikuwa bado haijakua ingawa baadhi ya maeneo kama vile Ilala mitaa yake ilikuwa ina lami (aina ya asphalt). Hadi leo hii barabara nyingi za eneo hilo hazijakarabatiwa – ile asphalt inayoonekana bado inakumbusha historia yake.

Magari pia yalikuwa machache sana kulinganisha na sasa. Kwa magari madogo madogo maarufu yalikuwa ni Ford, Volkswagen, na Peugeot 304, 203 na 404. Modeli ya 504 zilianza kuingia mwanzoni mwa miaka ya 70.

Hata taa za kuongozea magari zilikuwa katika  chache sana kuliko sasa kama vile makutano ya Lumumba na Uhuru, Jamhuri na Morogoro, Samora (zamani ikiitwa Independence) na Morogoro na pale Fire station.
Nakumbuka nilipoanza kazi idara ya Ushuru wa Forodha pale jengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki, mkabala na kituo cha mabasi ya DMT cha Stesheni (kabla ya ujio wa UDA) kulikuwapo askari mmoja wa trafiki akiongoza magari akisimama makutano ya City Drive (sasa Sokoine Drive) na Railway Street – pale karibu na Central Police Station.

Alikuwa akivaa kinadhifu na alikuwa akigeuka huko na kule akiongoza magari hasa pale misafara ya wakuu wa nchi ukiwa inapita. Mara nyingi nilikuwa nasimama na kumtazama askari huyu wa trafiki – hadi utampenda – maana alikuwa kama vile robot. Siyo siku hizi matrafiki wa barabarani wanaongoza magari huku wakiongea na simu zao za viganjani.
Majengo ya magorofa yalikuwapo zaidi maeneo ya Uhindini. Kariakoo kulikuwa magorofa kwenye barabara za Uhuru na Msimbazi na maeneo ya kuzungukia soko la Kariakoo, wakati huo kabla ya soko hili la sasa kujengwa. Sehemu moja ya eneo hilo – pale lililopo soko la sasa la mboga – ilikuwa ni kituo cha mabasi ya kwenda nje ya mji.

Lile eneo ambalo kumejengwa jengo la DDC Barabara ya Msimbazi ilikuwa ni kilabu ya pombe za kienyeji – kibuku.
Mabasi ya DMT yalikuwa yakienda kwa ratiba (timetable) na enzi hizo nyakati za kazi Idara ya Ushuru wa Forodha zilikuwa saa mbili asubuhi hadi saa 6 mchana huanza mapumziko na tunarudi tena saa nane mchana hadi saa 10. Nilikuwa nimepanga chumba pale Keko NHC mkabala na magorofa ya Wachina (Chinese flats).

 

Nauli ya basi ilikuwa ni senti 20 kwa safari za karibu na senti 50 zile za mbali. Basi langu lilikuwa ni la kwenda Uwanja wa Taifa (National Stadium) linaondoka pale Stesheni saa sita kasoro tano mchana, nafika nyumbani saa sita na dakika 20, napika ugali wangu na mboga nilizotayarisha jana jioni, nakula na kuwahi basi tena kurudi na kuingia ofisini saa nane kasoro 10. Kulikuwa hakuna misongamano wa magari kabisa.

 

Sijui ni kutokana hali ya ugumu wa maisha au vipi – enzi hizo watu walikuwa waaminifu sana. Miezi miwili baada ya kuanza kazi nilihitaji kununua redio ingawa sikuwa na fedha taslimu ya kulipia. Enzi hizo modeli za redio ni Philips na National zilizokuwa zikitengenezwa (assembled) hapa hapa nchini.
Jamaa mmoja alinionyesha duka moja la Mhindi mtaa wa Msimbazi akaniambia niende tu na kitambulisho changu. Nikaenda pale na mwenye duka akaniuliza kitambulisho na wapi ninaishi. Baada ya kuandika maelezo yangu, akaniambia nichague redio ninayotaka. Nikachagua redio moja National bei yake sh 95.
Akasema ninazo ngapi za kutanguliza – nikamwambia ninazo sh 40. Nikampa akaandika katika kitabu chake na kuniambia nimalize deni (sh 45) katika kipindi cha miezi mitatu yaani sh 15 kila mwezi. Akanipa redio na kuondoka nayo. Kila mwisho wa mwezi nilikuwa nikipeleka sh 15 bila kukosa. Siku hizi hakuna kitu kama hicho. Baadaye niliweza kununua friji ndogo na radiogram (santuri) kwa njia hiyo hiyo.
Siku hizo magazeti ya kila siku yalikuwa ni Tanganyika Standard (kabla ya kutaifishwa na kuwa The Standard na baadaye Daily News) na Uhuru gazeti la chama. Pale ofisini, mimi na wenzangu tulikuwa tunanua gazeti la Standard kwa zamu. Bei yake ilikuwa senti 40. Anayenunua siku hiyo kwanza huwaachia wenzake walisome halafu mnunuaji ndiyo anaondoka nalo siku ile.
Mtaa wa Independence (sasa Samora) ndiyo ulikuwa ukisifika kwa maduka ya nguo na kulikuwa maduka maarufu kama Teekays na Afra ambayo huleta aina mpya ya mashati – yale ya Van Heusen, Arrow na Gossage.
Ukinunua shati jipya la Van Heusen wenzako lazima watakuuliza siku ya pili bei yake na baina ya sisi vijana kuliibuka club zikijulikana kama ‘Teekays Club’ au ‘Afra Club’ ambao wanachama hutambulishwa kwa mashati wanaovaa.
‘Club’ nyingine zilikuwa za kujisomea vitabu vya riwaya (novel) hasa zile za James Hadley Chase, Erle Stanley Gardner na Alistair Maclean. Kutokana na bei ya vitabu hivi kuwa kubwa (enzi hizo) mwenye kununua humuazima mwenzie kusoma na akimaliza humpa mwingine. Utamaduni huu wa kujisomea umepotea kabisa.
Mtaa wa Independence pia kulikuwapo maduka mawili maarufu ya kuuza zile sahani za santuri (gramophone records) – Dar es Salaam Music and Sports House na Mahmoud Radio House. Hilo la kwanza – mkabala na Benki ya NBC Clock Tower Branch hadi leo lipo lakini siku hizi linauza vifaa vya michezo tu. Lile la pili lilikuwepo pale makutano ya Mkwepu na Independence, baadaye mgahawa wa Salamander na ambapo sasa Yusuf Manji anainua jengo.
Kila Jumamosi lazima kuna ‘vibao’ (yaani santuri) mpya za akina Franco Luambo na Rochereau vilivyofika na pia santuri za zile za bendi zetu za nyumbani – Morogoro Jazz, Western, Dar Jazz, na Cuban Marimba. Yalikuwa ni maduka yangu makubwa hasa pale baada ya kununua radiogram iliyowezesha kupanga sahani kumi za santuri na kupiga moja baada ya moja.
Na maeneo ya burudani yalikuwa mengi hasa zile za usiku – yaani night club. Pale Mnazi Mmoja kulikuwapo Getways ambapo alikuwa anapiga Papa Miki na baadaye Safari Trippers. Jirani kulikuwapo ‘Princess Bar and Night Club’.
Night Club nyingine ilikuwa Margot, upande wa kushoto mwa jengo la TCCL la sasa ambako penyewe hapo ilikuwapo hoteli moja maarufu ikiitwa Splendid Hotel. Jirani ya hapo kwa nyuma ilikuwapo Cosy Café lakini hii ilikuwa ni mgahawa tu.
Sehemu nyingine maarufu ilikuwa ni Tanzania Legion – makutano ya barabara za Msimbazi na Morogoro, maeneo ya Fire. Dar es Salaam Jazz Band (Majini ya Bahari) chini ya gwiji Ahmed Kipande alikuwa akitumbuiza pale.
Kulikuwapo kumbi nyingine za burudani hususan zile zilizokuwa zikimilikiwa na DDC kama vile zile za Magomeni Kondoa na Keko ambako bendi mbalimbali zilikuwa zikitumbuiza – achilia mbali zile za pembezoni mwa jiji kama vile ile iliyokuwa ikijulikana kama ‘White House’ maeneo ya Kimara.
Siwezi kusahau yale ‘maboogie’ ya mchana ya kikundi cha Sunbursts na mengine lakini kuna kisa kimoja kilinipata huko nikaacha kuwa shabiki. Siwezi kwa sasa kuhadithia hicho kisa.
Kwa wapenda miziki ya Taarabu, Mtaa wa Jamhuri katika hoteli ya Holiday kila Jumatano na Jumamosi huwakosi ama Egyptian Musical Club chini ya Abasi Mzee au New Extra Musical Club. Marehemu Shakila na kundi lake la Black Stars wanapokuja kutoka Tanga walikuwa wakionekana ukumbi wa jengo la Adult Education Mnazi Mmoja. Enzi hizo ndiyo wakati kibao chake cha ‘Kifo cha Mahaba’ kilikuwa kikitamba.
Ujambazi au vitendo vya ukabaji vilikuwa hakuna kabisa. Nakumbuka siku nikiwa pale Princess Bar Mnazi Mmoja na nikichelewa mabasi ya DMT (mwisho huduma ya mabasi ilikuwa saa 5 usiku) na kama nimemaliza hela ya taxi (sh 2 tu kwa trip) huamua kwenda nyumbani Keko kwa miguu.

 

Ndiyo – kwa miguu saa 7 za usiku nikipita barabara ya Nkrumah, Pugu Road (sasa Nyerere Road) na kuingia Chang’ombe Road hadi nyumbani bila ya madhara yoyote. Nikikutana na watu nasalimiana nao kwa kukohoa tu nao hunijibu hivyo.
Jaribu kufanya hivyo sasa hivi – tena saa 4 ya usiku wala si saa 7. Wajukuu wa wale wale niliokuwa nikikutana nao ndiyo wakabaji wakubwa sasa hivi.