Home Makala Ijue ofisi ya CAG, madaraka na mipaka yake

Ijue ofisi ya CAG, madaraka na mipaka yake

365
0
SHARE

ANNA HENGA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni ofisa wa umma anahusika na ukaguzi wa fedha na rasiliamali zote za umma ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ofisi ya CAG ilianzishwa ili kuongeza ufanisi katika uwazi, ufanisi na uwajibikaji wa rasilimali za umma.

CAG anaeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa ibara ya 143(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisomwa pamoja na Kifungu cha 4(1) cha sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008. Ofisa huyu pamoja na sifa nyingine anatakiwa kuwa ni Mtanzania kwa kuzaliwa na mwenye uzoefu, uadilifu na mtaalamu katika maswala ya ukaguzi.

Pia ni kiungo muhimu wa ulinzi wa mali za umma anateuliwa na Rais kushika wadhifa wa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa kipindi cha miaka mitano lakini anaweza kuteuliwa kwa kipindi kingine sio zaidi ya mara moja. Hii ni kumaanisha kuwa, CAG anatakiwa kudumu madarakani kati ya miaka mitano na kumi kama hakuna sababu iliyofanya kuachia madaraka yake ama kuenguliwa katika nafasi yake.

Sababu kubwa ya kuwa na ofisi ya CAG ni kuhakikisha kuwa, fedha za umma zinatumika kwa njia halali na za wazi kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa mipango ya serikali iliyoidhinishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kuweka kumbukumbu sawia, ibara ya 63(2) ya Katiba ya Tanzania Bunge ndiyo chombo kikuu cha jamhuri ya muungano wa Tanzania. Ibara ya 63(3) (C) ya Katiba imelipa Bunge mamlaka ya kujadili na kuidhinisha mipango yeyote ya serikali. Ili kuupa nguvu mhimili wa Bunge katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na kwa kuzingatia upana wa shughuli zingine za bunge, ofisi ya ukaguzi wa umma ilianzishwa ili kufanya kazi za kudhibiti matumizi ya mali za umma kwa niaba ya Bunge ambalo kimsingi ndilo lenye mamlaka. 

Hii ni kusema kuwa CAG ni ofisa wa Bunge na hutenda shughuli zake kwa niaba ya Bunge kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma lakini ambaye hatalazimika kufuata mamlaka za ama serikali, Mahakama ama Bunge.

CAG ana majukumu mbalimbali lakini makuu na muhimu ni matatu kwa mujibu wa sheria za Tanzania ambazo ni kukagua hesabu za matumizi ya fedha za umma, kuidhinisha matumizi ya fedha za umma kutoka mfuko wa hazina kwa mujibu wa ibara ya 136(3) ya Katiba ya Tanzania na kudhibiti matumizi ya fedha za umma katika idara mbalimbali za serikali, Mahakama, Bunge na misaada ya wahisani

Pia sheria inampa CAG mamlaka ya kuhakikisha kuwa fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali ambayo hutungwa kila mwaka zinatumika siyo tofauti na ilivyoidhinishwa na Bunge. Sheria ya Ukaguzi wa Umma 2008 inamtaka mkaguzi mkuu kuripoti viwango hivi vya ukaguzi kwa Bunge angalau mara moja kila mwaka.

CAG anawajibika kwa mujibu sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 kukagua na kuandaa ripoti juu ya fedha zote kwa mamlaka ya serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wizara, idara, mashirika ya umma, serikali za mitaa, Bunge na Mahakama. Pia sheria inalazimisha mihimili yote kutoa ushirikiano kwa CAG.

CAG kama ofisa wa Bunge, ili kuleta uwajibikaji, uwazi na usalama wa fedha za umma kutoka kwa wale waliopewa dhamana ya kusimamia na kupangia shughuli mbalimbali, Bunge kama mhimili mkuu kwa mujibu wa katiba linatakiwa kudhibiti na kusimamia mipango yote ya serikali ikiwamo matumizi na kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika tu kwa shughuli zilizopangwa na kuidhinishwa na Bunge. 

Ili kuleta uwajibikaji huo, ofisi ya ukaguzi wa hesabu za serikali ilianzishwa kwa mujibu wa katiba ili kulisaidia Bunge kupata jicho huru lenye uwezo wa kufanya tathmini ya namna gani serikali inawajibika kutokana na mipango iliyopitishwa na Bunge

Pia mamlaka nyingine za umma zikiwamo idara za serikali, Mahakama na serikali za mitaa zote kwa umoja wao zinawajibika kwa umma kupitia kwa Bunge. Utendaji na matumizi ya rasilimali za umma zinahitaji kuhakikiwa na Bunge kama mwakilishi wa wananchi kuwa yanatumika kama yalivyopangwa na hii hufanyika kupitia ripoti za mwaka za ofisi ya CAG. 

Bunge kama nguzo kuu inayotegemewa na umma, inahitaji hakikisho kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi, uadilifu na kwa kufuata sheria na mipango ya serikali ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa kupitia ripoti za ukaguzi za kila mwaka.

Hii ni kumaanisha kuwa, kila ripoti ya ukaguzi ya CAG ni lazima iwasilishwe kwa mwenye mamlaka ya uwakilishi wa wananchi yaani Bunge na hii itafanyika kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama akishindwa kuwasilisha basi, CAG yeye mwenyewe atawasilisha ripoti ya ukaguzi kwa spika wa Bunge.

Spika wa Bunge, baada ya kuipokea atalazimika kuiwasilisha ripoti hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.

Kamati hizo za Bunge zitajadili na kuwasilisha bungeni maoni na mapendekezo yao kuhusu ripoti hiyo na Serikali pia itawajibika kutoa majibu ya ripoti hiyo na kuyawazilisha kwa Bunge na CAG.

Mtu anayeshikilia mamlaka ya CAG anaelekezwa kufanya kazi kwa usawa, bila uwoga ama upendeleo na halazimika kufuata maelekezo yoyote ya mtu ama taasisis zaidi ya Katiba na Sheria za nchi. 

Ili kuhakikisha kuwa CAG na maofisa wake wanakuwa huru kufanya kazi zao kwa weledi, sheria imempa yeye na maofisa wanaotenda kazi kwa niaba yake kinga dhidi ya mashtaka yeyote yanayohusiana na kazi za ukaguzi na udhibiti wa hesabu za serikali.

Pia sheria imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa, ajira ya CAG haitahatarishwa kwa namna yoyote na mihimili anayoikagua na kuiwajibisha kupitia ripoti zake. 

Pia sheria imeipa ofisi ya ukaguzi mamlaka ya kupitia, kukagua nyaraka zote katika idara mbalimbali za serikali kuu, serikali za mitaa, mahakama na Bunge na mihimili yote inalazimika kisheria kutokuweka kikwazo chochote katika ofisi ya mkaguzi wa hesabu za serikali katika kutimiza mipango yake.

CAG amepewa mamlaka ya kuajiri wataalamu watakaomsaidia kutekeleza majukumu yake na yeye mwenyewe atakuwa ndiyo mamlaka ya kinidhamu dhidi ya waajiriwa wote wa ofisi yake. Pia sheria ya umma ya ukaguzi imempa mamlaka ya kupanga viwango vya stahiki za ujira kwa wafanyakazi wote walioajiriwa katika ofisi yake. 

CAG atatambulika kuwa amestaafu atakapofikisha miaka 65 akiwa ofisini ama awamu yake ya miaka mitano itakapokwisha na bila kuteuliwa tena na Rais muda wowote wa awali kati ya hizo itamsaafisha. Pia anaweza kutoa notice ya nia ya kutoendelea na majukumu yake kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1) (2)(a) and (2)(b)(i-ii) ya Sheria ya Ukaguzi 2008

Tofauti na wateule wengi wa Rais na sawasawa na Majaji wa Mahakama kuu na Mahakama ya Rufani, ujira wake umelindwa kwa mujibu wa Katiba na hawezi kufukuzwa kazi kwa mapenzi ya mamlaka ya uteuzi ila kwa kufuata sheria.

Anaweza tu kutenguliwa kwenye nafasi yake ikithibitika kuwa anashindwa kutekeleza majukumu yake ama kwa ugonjwa ama kwa tabia mbaya, ama kwa kukiuka sheria za ukaguzi ama maadili ya viongozi wa umma na hii ni baada ya tume ya uchunguzi itakayoundwa na Rais kushauri kuwa, CAG afukuzwe kazi. 

Kama Tume ya uchunguzi itamshauri Rais vinginevyo, atalazimika kufuata ushauri wa tume aliyoiunda na CAG hatafukuzwa kazini. kwa mujibu wa Ibara 144(3) ya Katiba.

Mara baada ya kumaliza madaraka yake hataruhusiwa kushika ama kuteuliwa katika ofisi yeyote ya umma. Hii inakusudia kuleta ufanisi katika shughuli za zake ili kutoyumbishwa na uwezekano wa ahadi ya madaraka flani mara atakapomaliza kipindi chake cha ukaguzi.