Home Latest News INDIA NI CHUNGU KWA WAANDISHI, WATOTO WA KIKE

INDIA NI CHUNGU KWA WAANDISHI, WATOTO WA KIKE

5080
0
SHARE
NA HASSAN DAUDI     |

RIPOTI ya mwaka huu ya Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka la Ufaransa (RSF) imeendelea kufichua ukandamizwaji wa uhuru wa vyombo vya habari unaopiga hatua kubwa duniani kwa sasa.

Nikukumbushe tu, makala haya ni sehemu ya kuiaga Siku ya Uhuru ya Uandishi wa Habari ambayo iliadhimishwa ulimwenguni kote Alhamisi ya wiki iliyopita, Mei 3.

Ripoti hiyo ya RSF, ambayo ilitoka siku chache kabla ya maadhimisho hayo, ilihusisha mataifa 180, Norway ikiwa kileleni, nafasi ambayo ilikuwa mwaka jana, likitajwa kuwa ndilo taifa linaloheshimu zaidi uhuru wa kujieleza, ikifuatiwa na Sweden iliyobaki nafasi ya pili.

Kwa upande mwingine, unapoyataja mataifa yaliyoendelea kusota katika nafasi za chini kwa na ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa habari ni India ambayo inaunda ‘top 42’ zilizo mkiani, ikishika nafasi ya 138 kati ya 180. Huko ni kuporomoka kwa nafasi mbili kwani ripoti ya Aprili, mwaka jana, ilionesha kuwa walikuwa wa 136.

Kama ilivyo kwa mataifa menginge yaliyoanishwa na ripoti ya mwaka huu kuwa yanauminya uhuru wa kujieleza, matukio ya kuuawa, kutekwa, kunyimwa taarifa muhimu yamekuwa sehemu ya maisha wanataaluma wa tasnia ya uandishi wa habari nchini India.

Tukio la kushitua zaidi na lililoteka mijadala ya mitandao ya kijamii ni la Septemba, mwaka jana, ambapo mhariri wa gazeti la wiki la Lankesh Patrike, mwanamama Gauri Lankesh, aliuawa kwa kupigwa risasi.

Hilo ni mbali ya lile la mwaka 2012, ambapo mhariri wa gazeti la Arunachal Times, Tongam Rina, kupigwa risasi ya tumbo, ikiwa ni miaka minne baada ya mwingine aitwaye Konsam Rishikanta kufanyiwa unyama huo na watu wasiojulikana.

Wakati hayo yakiwa ni mateso ya kila uchwao kwa waandishi, inaelezwa kuwa wamiliki wa vyombo vyao vya habari wamekuwa wakishindwa kuwasaidia, hasa pale wanapoingia katika matatizo dhidi ya Serikali. Waandishi wengi wamejikuta wakikosa mikataba mipya au kutakiwa na mabosi wao kuachana na ‘habari zenye utata’, yaani zinazoweza kuigusa Serikali.

Kwa mazingira hayo ya kuhofia kupoteza kazi, waandishi wamejikuta wakiachana na stori zenye afya kwa ustawi wa jamii, hasa zile zinazolenga kufichua ubadhirifu unaofanywa na ‘wachache’.

Kuna tatizo pia katika masilahi, ikielezwa kuwa waandishi wanalipwa kiduchu na wengi hawana mikataba, licha ya kutumia muda mwingi kazini, tena wakifanya hivyo katika mazingira magumu.

Kampuni zinazoonekana kuwa bora zaidi, yaani zinazofanya vizuri sokoni, asilimia kubwa ya waandishi wake hufanya kazi wakiwa na mikataba isiyozidi mwaka mmoja.

Katika hilo, mwandishi ambaye si mwajiriwa wa gazeti la Assamese daily, Chayamoni Bhuyan, anasema: “Achana na wachangiaji (freelancers) kama mimi, ambao hatujaliwi kabisa, hatuna ulinzi, tunafanya kwa mapenzi yetu kwa uandishi.

“Hata waandishi katika kampuni, hawana ulinzi wa kimasilahi. Kampuni zinavunja sheria za kazi. Wahariri wengi wanatimuliwa wanapotofautiana kimtazamo na wamiliki,” anasimulia Bhuyan.

Huku hali ikiwa hivyo kwa waandishi, pia katika siku za hivi karibuni, taswira ya India imekuwa ikichafuliwa na matukio ya unyanyasaji wa kingono.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, maeneo mbalimbali yamewashuhudia wananchi wenye hasira kali wakiingia barabarani kulaani uhalifu huo. Tukio baya zaidi kwao likiwa ni lile la Januari, ambapo watu wasiojulikana walimbaka na kumuua binti mwenye umri wa miaka nane.

Iliripotiwa kuwa watu kadhaa walimteka na kisha kumpa dawa za kulevya, kabla ya kumfanyia unyama binti huyo mkazi wa Kashmir.

Kutokana na kujirudia kwa vitendo vya ubakaji dhidi ya watoto wa kike, Serikali iliweka wazi mwezi uliopita kuwa atakayebainika kutenda unyama huo kwa msichana mwenye umri wa chini ya miaka 12, atahukumiwa kifo.

Wakati huo huo, kauli hiyo ya Serikali haikwagusa wengi kwani ilionekana kuchelewa, ikilinganishwa na kasi kubwa ya kuenea kwa utamaduni huo wa wasichana kutokuwa huru hata wanapokwenda shule, sokoni, au maeneo ya ibada.

Wiki iliyopita, msichana mwenye umri wa miaka 16, ambaye alibakwa na wanaume nane waliomteka akiwa nyumbani kwao, tukio lililotokea katika Wilaya ya Nuh, aliripotiwa kujiua. Baada ya kumfanyia hivyo, walimrejesha na kumwacha nje ya mlango wao.

Chanzo cha tukio hilo kilielezwa kuwa ni uhasama kati ya baba yake na familia moja ya kitajiri, ambayo ilikuwa ikimlazimisha mzee huyo kuachana na kesi aliyokuwa amewafungulia mahakamani.

Tukio hilo lilifuatiwa na lile la Kusini Magharibi mwa New Delhi, ambako binti mwenye umri wa miaka 19 alibakwa na na vijana watano, akiwamo mmoja aliyetajwa kuwa ni fundi bajaji.

Takwimu zilizopo juu ya udhalilishaji huo wanaofanyiwa wasichana zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, matukio ya ukabaji yameongezeka kwa asilimia 60.

Kama hiyo haitoshi, utafiti wa Shirika la Haki za Binadamu, Human Rights Watch, unagundua kuwa mabinti 7,200 kati ya 100,000, hufanyiwa hivyo kila mwaka.