Home Makala IPCS: Magufuli ndiye mwenye kufuli la migogoro ya kisiasa

IPCS: Magufuli ndiye mwenye kufuli la migogoro ya kisiasa

1148
0
SHARE

NA MOSES JOHN

HALI ya kisiasa nchini si shwari licha ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusitisha kwa muda maandamano na mikutano waliyokuwa wamepanga kuifanya kuanzia Septemba mosi mwaka huu.

Maandamano hayo waliyoyapa jina la operesheni Ukuta, yalileta mtafaruku tangu kutangazwa kwake Julai mwaka huu hali iliyolazimu taasisi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini kuingilia kati.

Licha ya jitihada zote hizo, bado wamedai kuwa wataanza maandamano hayo Oktoba mosi mwaka huu. Hali hii bado imeendelea kuzua hofu katika tasnia ya siasa hasa ikizingatiwa katika upande wa jirani Visiwani Zanzibar hali nako si shwar.

Ili kudadavua hayo yote na namna ya kuyakabili, Taasisi ya Amani na Utatuzi wa Migogoro Barani Afrika (IPCS), imeona sasa isikae mbali katika kutoa ushauri ambao utachochea kupatikana kwa suluhu ya kudumu kwa kila pande kukubali kulinda amani na utulivu wa nchi yetu.

Katika mazungumzo yake na RAI hivi karibuni Mkurugenzi wa taasisi hiyo Cosmas Bahali, anasema umefika wakati sasa kwa Rais John Magufuli kukutana na Baraza la Vyama vya Siasa nchini ili kufikia suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaohatarisha amani na utulivu uliopo nchini.

Anasema licha ya Rais Magufuli kufanikiwa kuziba mianya ya rushwa na kukuza uchumi, pia anatakiwa kutoa kipaumbele katika kulinda demokrasia na utawala wa kisheria.

“Wakati Rais akiweka nguvu kubwa kwenye sekta ya uchumi, suala la siasa hasa demokrasia na utawala wa kisheria hajaweza kuupa kipaumbele zaidi. Hii inaweza kusababisha migogoro ya mara kwa mara na maandamano kama yanayopangwa na vyama vya siasa.

“Kwa kuwa Rais Magufuli ni mwenyekiti wa CCM, angeweza kutumia baraza la vyama vya siasa kuweka msimamo wake na kushirikisha wenyeviti wa vyama vingine vya siasa na kupata nafasi ya kujitambulisha kwao na malengo ya serikali yake.

“Mbali na misimamo hiyo ya kisiasa anatakiwa kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kama vile vyama vya siasa, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, Bunge, vyombo vya habari, vyama vya wafanyakazi,  vyama vya vijana na wanawake”  anasema Bahali.

Anasisitiza kuwa ushirikishwaji huo wa wadau mbalimbali ni muhimu kwa sababu kuna mambo ya kikatiba ambayo Rais hawezi kuyatolea maamuzi mwenyewe.

Aidha, anasema Rais Magufuli anapaswa kuunda baraza la taifa la kuzuia na kutatua migogoro kwa kushirikisha wadau wa demokrasia ambao ni vyama vya siasa, viongozi wa dini na wadau wengine.

Hata hivyo, anasema maandamano yaliyopangwa kufanyika Oktoba mosi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  si suluhisho la kudumu la kutafuta demokrasia na utawala wa kisheria.

“Kinachotakiwa ni kukaa pamoja mezani na kujadili mustakabali wa demokrasia na utawala wa sheria, kwa kutumia utaratibu huu shirikishi wa kitaalamu wa kushughulikia mgogoro, hali ya kisiasa itaboreshwa na kuisaidia serikali kutekeleza yake kwa ufanisi zaidi,” anasema.