Home Tukumbushane Isipoboreshwa kwa haraka UDART inaweza ikafa kama UDA

Isipoboreshwa kwa haraka UDART inaweza ikafa kama UDA

1730
0
SHARE

Wasafiri wagombania kuingia ndani ya basi la mwendokazi wakati wa “mgomo” wa madereva.

Na HILAL K SUED

Mapema mwezi huu baada ya lile sakata la ‘mgomo’ wa wafanyakazi wa kampuni ya mabasi ya mwendokasi (UDART), mgomo ambao ulisababisha adha kubwa kwa wasafiri wa jijini, kulikuwapo andiko moja lililokuwa likisambaa katika mitandao ya kijamii.

Lilikuwa ni onyo kwa wakazi wa Mbagala kwamba katu wasikubali kuletewa huduma kama hiyo ya mwendokasi katika maeneo yao kwani ni adha kubwa sana, na wakikubali watajuta, na ikiwezekana waandamane kuupinga mpango wa kupeleka huduma hiyo ambayo imo katika mpango wa serikali.

Nilistuka sana na andiko hilo, nilidhani ni dhihaka kama kawaida katika mitandao ya kijamii ambayo inapaswa kulaaniwa na kupuuzwa mara moja.

Lazima nikiri kwamba mimi si mtumiaji mkubwa wa huduma iliyopo ya usafiri wa mwendokasi lakini kwa mara chache ambazo nimeitumia huduma hiyo tangu ianzishwe kwake nimegundua kwamba kuna mapungufu makubwa – hasa katika utoaji huduma.

Jumatatu iliyopita kama saa 3 hivi asubuhi nilikuwa kwenye kituo cha Kisutu kungojea usafiri kuja Ubungo Shekilango. Baada ya kukata tiketi nilikaa pale kwa zaidi ya dakika 40 bila kupata usafiri. Mabasi mengi ya kwenda Ubungo/Kimara yalikuwa yanapita bila kusimama, mengi yakiwa na abiria wachache. Moja tu lililosimama lilikuwa limejaa watu kibao.

Nikauliza wenzangu tuliokuwapo kwa nini hali hiyo? Nikajibiwa kwamba yale yaliyokuwa yanapitiliza ni mabasi ya Express ambayo kituo cha kwanza kusimama ni Manzese. Nikauliza: mbona haya ya mabasi ya Express ndiyo mengi kuliko yale ya kawaida? Nikaambiwa kwamba mengine ya hayo yanayopitiliza siyo ya Express ila tu madereva wake hawataki kusimama-simama bila shaka wanaona ni adha tu kufanya hivyo.

Nikastuka sana kwa jibu hilo. Hatimaye likaja basi moja lililosimama na tukaingia na baada ya kuondoka tu tukatangaziwa kwamba ni la Express na kituo cha kwanza kusimama ni Manzese. Kuna mama mmojna akaanza kulalamika kwamba itakuwaje yeye anashuka kituo cha Magomeni Usalama? Ilibidi aende hadi Manzese na kutafuta usafiri mwingine kurudi alikotaka kuteremka.

Nashauri tu wahusika waingilie hili. Abiria ambao nauli zao ndiyo huendesha kampuni hiyo pamoja na kuwalipa mishahara madereva wake, hawapaswi kutendewa hivyo – wanalazimika kuingia kwenye mabasi ambayo hawajui kama ni ya express au la.

Mabasi ya express yanapaswa yawe na alama au rangi tofauti na yale ya kawaida au kuwepo matangazo ya sauti kabla abiria kuingia – kuepusha kuwachanganya bila sababu. Nakiri kwamba kuna maandishi yanayotembea mbele ya mabasi kwa juu lakini haya ni madogo, na basi likikupita pale uliposimama na kusimama mbele, huwezi kujua ni la huduma ipi – ya express au kawaida.

Kingine nilichokiona ni kwamba bado mabasi ni machache sana, watu wengi hungojea kituoni kuyasubiri, na ukichanganya na adha hii niliyoelezea, bila kuwepo marekebisho ya haraka, kuna uwezekano mkubwa huduma hii ikazorota kama ile ya UDA ya zamani, na watu wa Mbagala wakae chonjo kama walivyoelezwa. Watu wanasahau historia ya usafiri kwa wakazi wa jiji hili.

Huduma hii ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi ambayo ilianza rasmi karibu miaka miwili iliyopita ilileta matumaini makubwa kwa wakazi wa jijini hapa kutokana na adha waliokuwa wakipata kutokana na huduma za usafiri zilizokuwa zikitolewa na utitiri wa watu binafsi.

Ujio wa huduma ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi uliashiria kwamba wakazi wa jiji la Dar es Salaam walikuwa wanapata ukombozi, kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka 30, kutoka matatizo ya usafiri wao.

Mapema miaka ya 80 huduma iliyokuwa ikitolewa na shirika la umma – UDA ilizorota kiasi kwamba utawala wa rais Ali Hassan Mwinyi uliona hakuna njia nyingine isipokuwa kuruhusu watu binafsi kusaidia kutoa huduma hiyo muhimu jijini hapa.

Aidha hatua hiyo ilikuwa inaendana na sera za utawala wake wa kuanzisha soko huria – utawala kuacha kabisa kudhibiti njia kuu za uchumi na kufanya biashara. Wakazi wengi wa Dar walipumua kwa kupata huduma za mabasi yaliyopachikwa jina la ‘daladala.’ Lakini baadaye, polepole, huduma hii ikaanza kuwa mateso kwao.

Kwanza kabisa, kwa kuwa kulikuwa hakuna magari binafsi ya abiria ya kutosheleza – kutokana na udhibiti wa uingizaji magari uliokuwapo wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza, serikali iliruhusu magari ya aina ya pick-up kufanya kazi kubeba watu – baada ya kujengewa bodi za mbao na kuwekewa viti.

Kwa wanaokumbuka, haya yalifanana na yale mabasi ya “mninga” yanayotumiwa na ndugu zetu ng’ambo ya pili ya bahari. Hivyo kuna pick-up nyingi tu ziliopolewa kutoka majalala ya magari (vehicles scrap yards), yakakarabatiwa na kuingizwa barabarani.

Baadaye yakaja mabasi ya KIA kutoka Korea yaliyopachikwa jina la ‘chai maharage” – kutokana na namna ya ukaaji wa abiria, mkao wa kutazamana mithili ya watu wanavyokaa kupata huduma ya chakula ya chain a maharage kwenye vibanda vya ‘mama lishe’. Mabasi haya ambayo abiria huingia kwa kupitia mlango wa nyuma, usukani ulikuwa mkono wa kushoto, na yalipewa jina lingine – ‘wauaji wenye magurudumu’.

Hata hivyo serikali ilifumbia macho sheria zake za magari barabarani kwa kuruhusu haya magari ya abiria yenye usukani upande wa kushoto – na lilikuwa kosa kubwa sana kwani watu wengi walipoteza maisha kutokana na magari hayo kugongana na mengine uso kwa uso wakati wa kupishana (overtaking).

Jinsi miaka ilivyokuwa ikienda, idadi ya mabasi ikaongezeka pamoja na ubora wake – enzi za ‘vipanya” (Hiaces) zikarithiwa na magari makubwa aina ya Toyota Coaster, Isuzu Journey na Nissan Civilian, na baadaye yakaja makubwa kabisa yenye milango miwili ya kuingilia abiria. Mabasi haya yakaanza kusababisha ongezeko la msongamano wa magari katika barabara za jiji la Dar es Salaam.

Isitoshe wafanyakazi wa mabasi hayo – madereva na makondakta – wakaanza kuwa adha kubwa kwa wasafiri kutokana na yale walikouwa wakifanya na lugha zao za mdomoni. Kuna mambo mengine ni vigumu kutia akilini.

Kwa mfano, wenye mabasi hupiga kelele kupandisha nauli, na wanaporuhusiwa na serikali kupandisha nauli, wakiwa vituoni makondakta wanarudia kutangaza nauli za zamani hasa pale wanapokosa abiria.

Madereva wao hawapendi kutii sheria za barabarani – wanasimama popote wanapotaka, hasa kubeba abiria, lakini si kwa wale wanaoshuka – ambapo wanakuambia kuna ‘askari” mbele.

Aidha huwa hawapendi kukaa kwenye foleni – mara nyingi huamua kuendesha upande wa yale magari yanayokuja, au hata kuendesha juu ya pavement.

Lakini kuna wengi hufaidika na huduma za hizi daladala kama vile askari wa jeshi na polisi ambao kwa sababu ambazo hazijaeleweka wanasafiri bure, kwani enzi za huduma za mabasi ya UDA watu hawa hawakuwa wanasafiri bure.

Wengine wanaofaidika ni jamii moja ya watu ambayo ilianzishwa na wafanyakazi wa ndani ya mabasi haya – wapigadebe wa vituoni. Watu hawa baadaye wakaanza kuwa kero kwao kwani hulazimisha malipo kwa huduma ya kuita abiria vituoni, kazi ambayo hata hivyo huwa hawatumwi kuifanya.

Sasa tunaona dalili kwamba huyu “mkombozi” wa mara ya pili – huduma ya mwendokasi – naye anaanza kutetereka? Sababu ni nini? Baada ya ule “mgomo” wa mapema mwezi huu mengi yameandikwa na kikubwa kilichokuwa kinajionyesha kunaonyeshea kidole watoa huduma – kampuni ya UDART – ambayo serikali ina hisa kubwa tu. Kwa hiyo huenda kuna kale kagonjwa ka zamani kanarudi, kale ka fikra potofu kwamba ni “mali ya umma.”

Fikra hizi ndizo zilizo zorotesha na kuua huduma nyingi sana za kijamii zilizokuwa zikitolewa na yaliyokuwa mashirika ya umma, pamoja na mashirika mengine makubwa ya kibiashara. Tusirudi huko.