Home Makala Jaguar ni mhaini?

Jaguar ni mhaini?

923
0
SHARE

Na NASHON KENNEDY   

MWAKA 1977 ulikuwa ni wakati wa mwisho kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuhitimisha safari kile kilichojulikana kama “Jumuiya ya Afrika Mashariki,” ya zamani hitima ya safari hiyo ilisimamiwa kwa ukakamavu na ujasiri mkubwa na aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kenya kwa wakati huo Charles Njonjo.

Njonjo waziri aliyejaa vituko na vibweka vya kila aina katika uongozi wake na aliyekuwa na nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Serikali ya Mzee Jomo Kenyata, pia aliamini kwamba ni waafrika wachache wanaoweza kufanya mambo kama wazungu.

Njonjo aliyejiweka karibu kabisa na utawala haramu wa makaburu wakati wa Voster, alianzisha chokochoko na uchonganishi kati ya Serikali za Afrika Mashariki zilizokuwa zinaunda jumuiya hiyo na hatimaye viongozi wa nchi hizo wakashindwa kuaminiana na matokeo yake jahazi likazama kwa kila mmoja kuondoka na mbao zake.

Wajanja waliondoka na mbao nyingi za jahazi kuliko hata walivyostahiki kwenye mgao wa mali za jumuiya hiyo, mfano nchi ya Kenya walichukua meli za Victoria na Nyangumi, ndege zote zilizokuwa za shirika la ndege la Afrika Mashariki na mali zote za Shirika la Posta na simu nazo zilichukuliwa na Kenya.

Tanzania na Uganda zilibaki na mali kiduchu, Uganda ikifaidika na Chuo cha Marubani cha Soroti kilichokuwa chini ya jumuiya hiyo huku Tanzania ikijitwalia chuo cha reli na injini na mabehewa ya treni na kiasi kidogo cha mabasi. Huo ndiyo ukawa mwisho wa matanga yaliyotengwa kuomboleza kifo cha EAC ya kale.

Matokeo ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo ukawa mwanzo mwa uhasama na chuki miongoni mwa ndugu waliopendana, kuthaminiana na kuheshimiana kwa kipindi kirefu. Baadhi ya Watanzania waliokuwa nchini Kenya walifukuzwa, Uganda wakajibu mapigo kwa kuwafukuza Wakenya waliokuwa nchini mwao na katika sarakasi zote hizi, Tanzania ilibaki kimya ikitafakari athari zilizokuwa zinasababishwa na kuvunjika kwa jumuiya hiyo.

Mwalimu Nyerere kwa wakati huo, alijaribu kuwarejesha viongozi wenzake katika fikira kuangalia upya madhara ya uamuzi waliokuwa wamechukua, uamuzi wa hasira kwamba mwenzio akimwaga ugali wewe mwaga mboga!

Mwalimu Nyerere kwa falsafa kubwa alijitahidi kuonesha athari za kuvunjika kwa EAC, Miongoni mwa maneno aliyotumia Mwalimu na hapa namnukuu, “Mataifa makubwa yenye nguvu za uchumi na kijeshi yanajitahidi kuungana na kutetea muungano wao kwa gharama kubwa, lakini wakati huo huo mataifa manyonge na dhaifu kiuchumi na kijeshi yanafanya jitihada kubwa kuvunja umoja wao,” mwisho wa kunukuu.

Jitihada za kuanzisha upya umoja huo zilianza mara tu baada ya athari za kuvunjika zilipoanza kujitokeza, Mzee Kenyata akapita katika utawala wake, Mzee Moi akapita, Mwai Kibaki akapita na hatimaye sasa Uhuru Kenyata, hali kadhalika hapa nchini Mwalimu Nyerere muda wake kama Rais, akaja Ally Hassan Mwinyi, Benjamini William Mkapa, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na sasa ni Dk. John Pombe Magufuli.

Nchini Uganda, Rais Milton Obote alipinduliwa, akaingia Idd Amin Dada, Paul Mwanga, Yusuph Kirondo Lule, Geofrey Binaisa, Tito Okello, baadaye Milton Obote akarejea hadi mwaka 1986, nchi hiyo ilipoangukia mikononi mwa Yoweri Kaguta Museveni.

Licha ya muda wote ulioshuhudia mambo mengi yanayofaa na yasiyofaa, wananchi wa EAC ya kale nah ii ya sasa wameendelea kuishi maisha ya kupendana. Hata mipaka ya kikoloni inayozigawa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda , Burundi na Sudan ya Kusini imeendelea kuwa wazi na kuwawezesha wananchi wa EAC kukaribiana.

Kuvunjika kwa jumuiya ya kale ya EAC hakukuhusisha kwa namna yoyote ile wananchi, ila ilivunjwa na tama za baadhi ya viongozi wake.
Tukiwa tumesahau yale yaliyosababishwa na Njonjo aliyechangia kuvunjika EAC mwaka 1977, sasa anaibuka Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua (Jaguar) akiwa na maneno yaleyale na njama ile ile aliyoisambaratiwa EAC wakati ule. Mara hii Jaguar anaibuka na kioja cha kuipa Serikali ya Kenya saa 24 kuhakikisha wageni wote walioko nchini humo wanaondoka mara moja, na kuonya kuwa endapo wageni hao hawataondoka, wataondoshwa nchini humo kwa kupigwa.

Anatoa maneno haya mbele ya wapiga kura wake, maneno yanayohamasisha na kushawishi wananchi wa Kenya na viongozi wao kuwafukuza wageni na haswa Waganda na Watanzania wanaofanya biashara nchini Kenya ni maneno yanayosikitisha kwa kuzingatia uchanga wa jumuiya yenyewe.

Maneno hayo ya uchochezi yanayojenga chuki miongoni na baina ya wananchi wa Tanzania, Kenya na Uganda bila shaka ni uhalifu (Exephorbia) kama ilivyofanyika mara mbili huko Afrika Kusini na Serbia wakati wa Slobodan Milosovik, ambapo mamia ya wageni waliuawa na kunyang’anywa mali zao na wenyeji wa mataifa hayo.

Uhusiano wa Tanzania na Kenya kama waasisi wa Jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki na sasa una mifano na faida nyingi , kila taifa miongoni mwa mataifa haya mawili, linanufaika na uwapo wa taifa jingine, inajulikana na sio siri kuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Kenya duniani ni Tanzania.

Tatizo wanaoanzisha chokochoko za aina hii ni watu wasiojitambua, wana fikra zilizogubikwa na dhana ya ukoloni mkongwe, wana imani ile ile ya Charles Njonjo kwamba kila jambo kubwa na zuri haliwezi kufanywa na mwafrika.

Jaguar anasahau au hajui kutokana na upeo wake mdogo wa kujua mambo na kuyachambua  kuwa Wakenya wengi wakati wa vita ya Mau Mau (Ukombozi-Kenya) walikimbilia Tanzania na kuhifadhiwa kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dodoma (Kikuyu), Iringa(Mufindi) na Shinyanga kwa kutaja maeneo machache katika nchi yetu. Kwa kuwahifadhi wapigania uhuru hao ndio maana hata kesho wakenya na vizazi vyao wamechukulia kwamba ‘Tanzania is their next home’.

Wakenya wengi wamo Tanzania na wamefanikiwa kushika nafasi mbalimbali katika Serikali, Mfano marehemu, Joseph Mungai, aliyekuwa wazira katika wizara mbalimbali, Baby Twist aliyewahi kuongoza Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania wakati huo (FAT) na wachezaji wengi wa Tanzania wameichezea timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars, kama Abbas Magongo mlinda mlango maarufu wa Harambee stars na Ambrose Anyonyi.

Katika EAC mpya kuna itifaki mbalimbali kama ushirikano wa pamoja katika masuala ya ushuru, masoko na mipaka, ushirikiano huu utafanikiwaje ikiwa vitimbakwiri kama huyu Njagua wataendelea kujitokeza? Naishukuru Serikali ya Kenya imeanza kumchukulia hatua za kisheria.

Lakini pia ni jukumu la Serikali ya Kenya mbali ya kuanza kumchukulia hatua mbunge huyo, itumie fursa hii pia kuanza kutoa mafunzo kwa viongozi na wabunge wake namna bora ya kulinda diplomasia ya uhusiano, uchumi na ulinzi baina yake na nchi majirani ili upuuzi wa aina hiyo usijitokeze tena.

Mwananchi wa Marekani akithibitika kuanzisha chokochoko za kuvunja muungano wa majimbo ya Amerika( United States of America) adhabu yake ni ile ile kama mtu anayetaka kupindua utawala. Jaguar ama ni mhaini au anakaribia kuwa mhaini, tusipokuwa makini kama nchi, hii itakuwa ni dalili za kuivunja upya Jumuiya ya Afrika Mashariki! Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Jumuiya ya Afrika Mashariki.