Home Latest News JAJI KAIJAGE HATAKUWA NA TOFAUTI NA WALIOMTANGULIA

JAJI KAIJAGE HATAKUWA NA TOFAUTI NA WALIOMTANGULIA

1085
0
SHARE
Jaji Semistocles Kaijage akiapishwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi (NEC).

NA HILAL K SUED,

Muda mfupi tu baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi (NEC) nchini, Jaji Semistocles Kaijage, pamoja na mengine alisema atahakikisha anafanya kazi yake kwa uhuru, uadilifu na haki na maamuzi yake hayatakuwa na upendeleo wowote.

Kwanza kabisa namtakia kila la kheri katika nafasi yake ngumu na yenye changamoto nyingi mno. Nasema hivi kwa sababu kuna wakati – tena kwa muda mfupi sana – atajikuta ameishika amani ya nchi katika vidole vyake na maamuzi yake ndiyo yanaweza kuwa hatima ya taifa zima.

Hata hivyo matamshi yake ya kutenda kazi yake kwa haki yamekuwa yakitolewa na watangulizi wake kila wanapoapishwa kushika nyadhifa hizo na mara nyingi hubakia jinsi yalivyokuwa yakitolewa – matamshi. Sababu kubwa ya “matamshi” haya kutokwenda zaidi ya hapo bila shaka wanazifahamu wateule wenyewe wakiwa kama Majaji wa Mhakama Kuu – sifa moja muhimu inayowawezesha kuchaguliwa katika nyadhifa hizo.

Jaji Kaijage bila shaka anaufahamu msingi mkuu wa kutoa haki usemao ‘haki si tu kwamba inatakiwa itendeke, bali pia inatakiwa ionekane inatendeka’. Sasa basi namna alivyoteuliwa kushika wadhifa huo mkuu wenye kuhitaji utoaji wa haki kamwe haionyeshi iwapo haki ikitendeka.

Kwa maneno mengine katika sehemu ya pili ya msingi huo wa haki nilioutaja hapo juu ya – haki haitaonekana kutendeka kwa sababu ‘mtoa haki’ – yaani Jaji Kaijage (na NEC nzima) iliteuliwa kwa namna ambayo kimuonekano wake haiwezi kutarajiwa kutenda haki.

Bila shaka aliyeubuni ulazima kwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa na sifa za jaji wa Mahakama Kuu aliyafikiria masuala mbali mbali likiwemo hili la msingi mkuu wa kutoa haki.

Jaji Kaijage aliteuliwa na mtu ambaye mbali kuwa ni Rais wa Jamhuri, bali pia ni mwenyekiti wa chama kinachotawala (CCM) na ambaye piga ua atakuwa ni mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Nasema ‘piga ua’ kwa sababu kufuatana na utamaduni ambao chama hicho kilivyojiwekea Rais John Magufuli atagombea tena nafasi hiyo mwaka 2020 kumaliza kipindi chake cha pili cha urais wake na hivyo chama chake kitaingia katika ushindani mkuu wa kisiasa dhidi ya vyama vingine.

Sasa hapa haki kweli inaonekana kutendeka, pamoja na kauli yake ya kusema atatenda haki tu na hatampendelea upande wowote? Haiwezekani – uteuzi wa Jaji Kaijage (na wengine waliomtangulia) haukuwa na kiashirio cha kuweza kutenda haki.

Vivyo hivyo mwenyekiti wa chama kilichopo madarakani ndiyo mteuzikwa watendaji wengine wakuu wa NEC kama vile mkurugenzi mkuu wa uchaguzi na wasaidizi wake wakuu. Hali kadhalika wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo mbali mbali ambao ni Wakurugenzi wa halmashauri za miji na wilaya.

Lakini ndivyo Katiba ya sasa inavyosema. Katiba hii ilipitishwa na Bunge la chama hicho mwaka 1997 na kufanyiwa marekebisho na Bunge lenye wabunge wengi wa chama hicho kukidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi.

Haitarajiwi kamwe kuwepo kwa Katiba mpya kurekebisha kasoro hizo zinazokinzana katika kanuni za utoaji haki kwa sababu viongozi wengi katika chama hicho wanaona mambo kwao ni shwari kabisa – na hakuna haja ya kuangalia zaidi ya urefu wa pua zao.

Lakini lazima watambue kwamba haya ni mapungufu makubwa ya Kikatiba na yanaweza kuathiri amani yetu na utulivu huko tuendako. Kwa ujumla Tume yetu ya uchaguzi kamwe siyo huru na kuna vigogo wawili wa utawala wamewahi kuwa wakweli na kutamka hivyo hadharani.

Swali ni kwamba iwapo Jaji Kaijage atasimamia alichokisema je kabla ya uchaguzi wa 2020 ataweza kusukuma kuwepo marekebisho ya katiba au sheria ya uchaguzi yatakayoashiria uwepo wa haki kwa Tume yake katika usimamizi wa uchaguzi?

Jibu ni hawezi, hawezi, hawezi. Atalazimika kwenda na mfumo wa Tume yake jinsi ilivyo ambapo mwenyekiti wa chama tawala anaweza kumbadilisha yeye mwenyewe na/au watendaji wake wakuu wakati wowote, hata katika muda mfupi tu kabla ya uchaguzi. Limetokea hili – tena wakati uchaguzi wa mwaka jana ulipokuwa ukikaribia. Na hali ya namna hii iko katika nchi nyingi Barani Afrika na kwingineko duniani ambako demokrasia ya vyama vingi basdo dhaifu.

Kada mkongwe maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Pius Msekwa aliwahi kutoa undani wake kuhusu hali ya ‘uhuru’ unaodaiwa kuwepo katika tume za uchaguzi za barani Afrika.

Katika kongamano moja la masuala ya kisiasa hapa nchini baada tu ya uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2007 uliofuatiwa na machafuko makubwa na umwagikaji wa damu Msekwa alisema machafuko yale yalisababishwa na Tume ya uchaguzi kumtangaza Mwai Kibaki wa PNU kuwa mshindi dhidi ya Raila Odinga wa ODM.

Msekwa alisema: “Isitoshe jina rasmi la tume hiyo iliyotangaza matokeo hayo ya utata lilikuwa ‘Tume Huru ya Uchaguzi’ (Independent Electoral Commission), lakini angalia madudu iliyofanya!”

Alichogusia Msekwa, ingawa hakukisema moja kwa moja, ni kwamba tume za uchaguzi barani Afrika ndizo husababisha machafuko baada ya chaguzi kutokana na maamuzi yake yasiyo ‘huru.’

Ambayo hakuyasema Msekwa ni kwamba hapa kwetu bahati bado inatupenda na tunakwenda nayo (hiyo bahati) vizuri pamoja na kwamba Tume yetu ya Uchaguzi (NEC) siyo huru.

Kigogo mwingine aliyewahi kuikosoa Tume ya Uchaguzi ni Jaji Augustine Ramadhani – ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Nne wa Tanzania. Miaka kadha iliyopita aliwahi kuwaambia waandishi wa habari katika kongamano moja la masuala ya siasa kwamba hakuwahi kuamini kwamba NEC ilikuwa ni chombo huru. Hata hivyo alisema kauli hiyo ni yake binafsi.

Ajabu moja ni kwamba pamoja na maonyo yote yote haya kuhusu NEC bado tunaenda na mtindo huu huu ulipo, hakuna hata katika utawala mwenye kuweza kutoa tahadhari kwamba tunaweza kuwa tunalikaribia korongo.

Na tunaenda na upofu huu pamoja na kutambua kilichowakumba majirani wetu wa Kenya miaka tisa iliyopita na kuwaletea maafa makubwa. Kwa majirani zetu hao maafa hayo yaliwapatia akili, wakakaa mezani pamoja na kuamua kutunga Katiba mpya ambayo pamoja na mengine ilirekebisha kasoro hiyo kuhusu Tume ya Uchaguzi – ingawa bado ziko figisu figisu katika utekelezaji kwani kama msemo mmoja usemavyo ‘utamaduni hauwishi kirahisi’ (traditions die hard).

Wakati Magufuli anamuapisha Mweyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi, huko Kenya sintofahamu kubwa iliibuka Bungeni kuhusu sheria yao ya uchaguzi ambapo serikali ya chama tawala cha Jubilee kilipeleka muswada wa marekebisho ya sheria hiyo kuiwezesha Tume yao ya Uchaguzi (IEBC) kutuma (au kusafirisha) matokeo ya uchaguzi kutoka vituoni kwa njia ya kawaida iwapo njia ya kielektroniki itashindikana.

Muungano wa vyama vya upinzani chini ya CORD ulikuwa unaupinga muswada huo wa marekebisho ukidai kwamba Jubilee walikuwa wanajiwekea mazingira muafaka ya kuiba kura katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka ujao.

Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi wetu hapa wa mwaka jana kuna watu wa upinzani walikamatwa wakikusanya matokeo ya uchaguzi kielektroniki (kupitia computer) kutoka maeneo mbali mbali nchini, wakidaiwa ni kosa la jinai kufanya hivyo na baadaye kufunguliwa mashitaka chini ya Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ambayo ilikuwa imepitishwa kwa haraka haraka na Bunge siku chache tu kabla ya uchaguzi.

Hata hivyo ingawa serikali baadaye ilifuta mashitaka dhidi yao, suala hili ni nyeti sana kwani serikali inatambua kutokuwapo kwa usiri wa njia za mitandao katika kusafirisha data za matokeo ya uchaguzi.

Kwa ujumla serikali haitaki vyama vingine vya siasa (na wananchi pia) vikajua (na siyo kutangaza tu) namna kila chama kinavyojilimbikizia kura kutoka maeneo mbali mbali pindi yanapotangazwa vituoni. Serikali hupenda NEC tu ndiyo ina haki pekee ya kujua hesabu zinavyoendelea na baadaye yenyewe kutangaza mshindi/washindi ni nani.

Huko Kenya upinzani chini ya muungano wa CORD unadai kuwa kuruhusu kutuma matokeo ya uchaguzi kwa njia za kawaida kutokana na kufeli kwa njia za kielektroniki kunaweka mazingira ya wizi wa kura. Wanataja ilivyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2013.

Lakini huko Kenya tume yao ya uchaguzi – yaani Mwenyekiti na Wajumbe wake – hupatikana kwa njia ya uwazi na hivyo haki inaonekana kutendeka zaidi kufuatana na katiba yao mpya. Baada ya kampeni kubwa yakiwemo maandamano, muungano wa CORD umefanikiwa kuing’oa Tume ya zamani ya uchaguzi iliyokuwa ikiongozwa na Isaack Hassan na ambayo ilisimamia uchaguzi wa mwaka 2013.

Jopo maalumu limeshafanya kazi yake ya kupendekeza majina mawili ya kumrithi Hassan na ambayo yatapelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atachagua jina moja. Hali kadhalika jopo hilo hilo limependekeza majina 11 kuwa Makamishna wa Tume ambapo rais atachagua sita miongoni mwao.

Hata hivyo majina ya Mwenyekiti wa Tume na Makamishna sita ambayo Rais uhuru atayachagua kati yao lazima yapelekwe Bungeni kwa ajili ya kithibishwa kabla ya kutangazwa.