Home Afrika Mashariki JAJI MARAGA AMEBADILI SURA YA SIASA ZA AFRIKA

JAJI MARAGA AMEBADILI SURA YA SIASA ZA AFRIKA

2755
0
SHARE

DEOGRATIAS MUTUNGI

Baada ya maamuzi ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kubatilisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, mwaka huu  uliompa ushindi wa asilimia 54.27,  Uhuru Kenyatta dhidi ya Raila Odinga aliyepata asilimia 44.74 na kuamuru ufanyike upya ndani ya siku 60 kabla ya Novemba mosi, umeonekana kubadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za Kiafrika.

Kwa mantiki ya kisiasa, maamuzi ya mahakama yanaiweka Kenya katika  ligi  yenye ushindani na ubora wa demokrasia iliyotukuka na pengine kuiweka taswira ya  Afrika  katika wigo mpana wa kuamsha soka ya siasa yenye uthubutu na umakini wa hali ya juu. Bila shaka mhimili huu umeonyesha mfano kwa mataifa mengine ya Kiafrika kufuata nyao za Wakenya.

Soka ya siasa za Kiafrika  inafahamika kwa ubovu wake wa kuendeshwa kwa mizengwe  bila kanuni, miiko, taratibu  na ukosefu wa vyombo vya usimamizi nikiwa na maana ya demokrasia, Katiba na tume huru, ukosefu wa dhana hizi kwa siasa za Kiafrika ndicho chanzo cha baadhi ya mataifa ya magharibi na Amerika  kuidharau Afrika kama bara lililoshindwa kujiendesha kisiasa na kiuchumi, dhana hii ya watu wa magharibi ina mashiko ndani yake kwa hoja ya udikteta, uhuni na uminywaji wa demokrasia unaofanywa na watawala wa Kiafrika.

Hivi karibuni Donald Trump, Rais wa Marekani akiwa Berlin Ujerumani kwenye mkutano wa G20, alitoka nje ya mkutano na kumwachia kiti mwanaye Ivanka pale walipoanza kujadili matatizo ya Waafrika, baadaye alipoulizwa na vyombo vya habari juu ya tukio hilo, Trump alijibu: “Hawezi kujadili bara lililoshindwa kujitawala,” ilikuwa ni kauli chafu kwa Waafrika lakini yenye kumaanisha ukweli ndani yake, kauli za namna hii ni matokeo ya watawala wa Kiafrika kuinajisi demokrasia bila aibu.

Siasa komavu na demokrasia kwa Afrika si kitu cha maana kwa baadhi ya viongozi uchwara wanaotawala kwa kusigina katiba na kucheza faulu nyingi kwa wapinzani wao, upinzani kwa Afrika  ni kama uadui na pengine uhaini, mataifa mengi  ya Afrika yamekuwa yakitumia dola na nguvu nyingi  kukabiliana na wapinzani wao kisiasa kuliko kuleta  maendeleo na hivyo kushindwa  kutimiza ilani zao za uchaguzi kwa wananchi waliowachagua, leo hii kwa Afrika kuwa mpinzani  ni kama dhambi na uzandiki na mahali pako ni jela tu hilo ndio soka letu la kisiasa, ni aibu kwa bara la Afrika lenye wasomi wenye weledi uliotukuka  kuendesha michezo michafu ya kisiasa.

Kimbilio la Wapinzani kwenye soka letu la siasa kwa Afrika  baada ya kuminywa kwenye sanduku la kura na tume za uchaguzi kuchakachua matokeo  limekuwa ni kwenda  mahakamani, hata hivyo si wote wanaoenda mahakamani kwa imani ya kupata haki stahiki, wengi wao wamekuwa na kasumba ya kwenda huko ili kutimiza wajibu na kujaribu nini kinaweza kutokea, hii inatokana na mhimili huu wa mahakama kutoaminiwa na baadhi ya vyama vya kisiasa  ambavyo huamini mahakama  mzania wake uegemea upande wa Serikali iliyoko madarakani na hiki ndicho kilio cha muda mrefu kwa wapinzani wa Kiafrika, rejea Angola, UNITA, PRS, DRC Kongo UDPS, Tanzania, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, Rwanda, DGP, Zimbabwe, MDC na kwingineko wote hawa wamekuwa wakishambulia mifumo ya kimahakama juu ya utoaji wa haki iliyo sawa.

Swali kuntu hapa ni je, mahakama zetu ziko huru kiasi gani kutoa maamuzi yaliyo sahii kwa wachezaji wa upande wa pili ndani ya soka ya siasa, licha ya mahakama kuwa mhimili mwingine unaojitegemea lakini kwa Afrika ni nadra sana chombo hiki kutoa maamuzi yaliyo na haki ndani yake si kwamba majaji na mahakimu hawajui sheria la hasha, bali watawala huamua kuwaondoa ufahamu wa taaluma zao na kutenda watakavyo,  vitendo ambavyo kwa baadhi ya mataifa ya Kiafrika vimezua migogoro, machafuko na umwagaji damu.

Ndio maana mantiki inaonyesha kuibua mjadala mzito juu ya maamuzi ya mahakama ya juu nchini Kenya  kuamua uchaguzi urudiwe  upya, mbali na historia kuwekwa na Taifa la Kenya, lakini  huu ni kama utamaduni mpya  kwa Afrika, ni maamuzi ambayo  hayakutegemewa kabisa na pengine ni kama sehemu ya ushindi kwa baadhi ya wapinzani ndani ya Kenya na nje ya Taifa hilo, ni jambo la pekee kutokea Afrika wengi hawaamini maamuzi ya mahakama lakini ukweli ndio huo na pengine ndio mwanzo wa Afrika mpya kisiasa.

Ndio maana shangwe, vigelegele na nderemo zilitawala kwa wafuasi wa Odinga na NASA (National Super Alliance) kwa ujumla, hii ni sawa na Taifa Stars kuifunga Brazil tatu bila tena ugenini, hata Rais Kenyatta hakuamini kile alichokisikia ndio maana ameamua kuwaita majaji walioamua kesi hiyo ‘Wakora’ akiwa na maana ya watu wenye roho mbaya wasiomtakia mema, kwa Kenyatta kutamka wakora ina maana alichotegemea sicho kilichokuwa.

Kisaikolojia ndani ya mifumo yetu ya kidemokrasia na miundo ya kiutawala Afrika hatuaminiani, hata kidogo tunazo katiba za ovyo kabisa ambazo zinabana baadhi ya vyama kupata haki zao za msingi  kwenye mihimili mingine, lakini zinatoa ahueni kwa upande wa pili kufanya watakavyo, huu ni ujangili wa kisiasa na demokrasia.

Kunajisi mifumo ya kisheria ni jambo ambalo halikubaliki kabisa kwa wanademokrasia wa  Afrika ya sasa, inahitaji kuwa  na mihili kama mahakama isiyobanwa na Katiba katika kutoa haki sawa bila kujali itikadi za vyama vya kisiasa, lakini bado tunazo Katiba zilizopitwa na wakati na zenye viraka vingi kwa mantiki ya kuibeba mifumo ya utawala wa kidhalimu na kifisadi.

Uzalendo ni jambo la muhimu katika ukombozi wa Taifa lolote duniani, kwa mantiki ya uzalendo nairejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema: “Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza  jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.” Hizi ni baadhi ya katiba tulizonazo Afrika ambazo bado zinaendelea kuingilia mihimili mingine katika upatikanaji wa haki katika soka letu la siasa na kufanya tusipande katika ligi iliyo juu zaidi.

Kwa mantiki ya maamuzi ya mahakama nchini Kenya, nadharia na taswira kwa siasa za Kiafrika zinaweza kuzalisha mambo mawili makuu katika soka letu la siasa. Mosi kuhamasisha hamasa kwa vyama vya upizani na wanaharakati kudai Katiba huru zitakazokuwa mkombozi wa demokrasia barani Afrika ili kukuza  wigo mpana wa haki na usawa wa kisiasa miongoni mwa mataifa ya Kiafrika na kuondoa udhalimu na dhuluma ya kisiasa.

Pili kuibuka mbinyo mkali kutoka kwa viongozi wa Kiafrika wanaoendesha nchi kwa udhalimu na uhuni kunyanyasa na kufunga midomo kwa kila atakayejaribu kudhubutu kuongelea neno Katiba mpya maana wanajua athari zake kutokana na kilichojili Kenya sambamba na hofu ya uovu wao walioutenda wakiwa madarakani.

Hata hivyo iwavyo na iwe, lakini  kilichotokea nchini Kenya ni historia ambayo haitasahaulika kwenye bara lenye utawala uliojaa maovu na mabavu na iwe angalizo kwa watawala wanaoamini kutumia mabavu kupora haki ya wengi ndio suluhisho la kila kitu, Afrika ya leo ni tofauti kabisa na ya miaka ile ya akina Mobutu Seseseko Kuku Ngbendu, tukiri kuwa maamuzi ya mahakama ya juu nchini Kenya yamelipandisha daraja soka letu la siasa kutoka ligi ndogo na kuingia kwenye ligi ya kimataifa na yenye ushindani.

0717-718619

dmutungid@yahoo.com