Home KIMATAIFA Jamaa aomba kuzichapa na mkewe mahakamani

Jamaa aomba kuzichapa na mkewe mahakamani

477
0
SHARE

Hassan Daudi na Mitandao

HIZI kesi za talaka zina mambo kweli kweli, hasa usiombe kukuta mmoja bado anampenda mwenzake. Hapo lazima atatafute sababu tu, hata kama ushahidi wa mahakamani utakuwa umethibitisha kuwa mwenzake ndiye mwenye haki.

Ndicho kilichotokea huko Marekani, ambapo jamaa aliyefahamika kwa jina la David Ostrom aliibua hoja unayoweza kuiita ya kipuuzi kabisa mara baada ya mahakama kuamuru ampe talaka mke wake.

Ostrom, mkazi wa Kansas mwenye umri wa miaka 40, aliona hakuna namna kwani ameshapigwa bao na mwanamke huyo, hivyo akaiomba mahakama ipewe nafasi ya kupigana na mkewe, Bridgette Ostrom (38).

Mwanaume huyo alikiri mbele ya mahakama kuwa amehujumiwa kisheria na bibiye Bridgette, lakini wapewe siku kadhaa za kila mtu kutafuta panga, kisha watandikane, kama wafanyavyo waigizaji wa filamu za Kichina, Japan na Korea.

Madai yake ni kwamba mkewe na mwanasheria Matthew Hudson walishirikiana kumchezea faulo, hivyo kushinda kesi yao mahakamani.

Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na vyanzo vya habari, Ostrom aliomba wiki 12 mbele ya mahakama, akiamini zitatosha kupata panga zuri lakini lisilokata kumkabili mke wake huyo wa zamani.

Hata hivyo, mwanasheria wa mkewe, Hudson, aliiomba mahakama kutupilia mbali ombi la jamaa huyo, akisema huenda tukio lao la kupigana kwa mapanga likaishia pabaya kwa mmoja kati yao kupoteza maisha.

Endapo hilo lingepitishwa na mahakama, basi ingekuwa mara ya kwanza kulishuhudia hilo likitokea katika ardhi ya Marekani, ingawa wataalamu wa historia wanasema ilikuwa kawaida nchini Uingereza katika karne nyingi zilizopita.

Ni kwa mujibu wa historia kwamba tukio la aina hiyo lilitokea Uingereza mwaka 1818.