Home Latest News JAMMEH MHUNI, MKORA KWELI HASA!

JAMMEH MHUNI, MKORA KWELI HASA!

902
0
SHARE
Yahya Jammeh

ALIYEKUWA Rais Gambia, Yahya Jammeh (51), alikuwa mkora na mhuni, eti?

Baada ya Uchaguzi Mkuu hivi karibuni alikubali kuwa ameshindwa na kuahidi kumpa ushirikiano Rais  mpya.

Baada ya yapata wiki moja akakataa kutambua matokeo na kutangaza hali ya hatari nchini Gambia.

Alikataa kabisa wito wa viongozi wenzake wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ya kukubali kushindwa na kuheshimu demokrasia.

Baadaye alilitumia Bunge kuhalalisha kuendelea kuwa madarakani kinyume cha sheria hadi Aprili mwaka huu, wakati huo bila shaka akiangalia njia nyingine ya kujichimbia madarakani baada ya muda huo.

Baada ya kuona kuwa ujanja wake unagonga mwamba, hasa baada ya viongozi wa ECOWAS kuamua kumng’oa madarakani kwa kutumia jeshi, akajidai kukubali kuondoka madarakani eti bila “kumwaga damu ya mtu hata mmoja”!

Jumapili iliyopita akaondoka nchini Gambia kuelekea Guinea Ikweta baada ya kufilisi hazina ya Gambia na kubeba Dola za Marekani milioni 11 ambazo ni fedha za walipakodi wa nchi hiyo!

Hizi zote ni taarifa za mtu mkora, mhuni asiye na adabu wala heshima kwa nchi na watu wake!

Wagambia walifurahi sana waliposikia kuwa Jammeh atasakwa na majeshi ya ECOWAS yakiongozwa na Senegal, ambayo yalikuwa tayari yamepiga kambi katika mpaka na Gambia, yakijiandaa kumng’oa madarakani iwapo angeendelea kung’ang’ania madaraka.

ECOWAS ilikuwa imetishia kumwekea Jammeh vikwazo au kuingilia kijeshi nchini mwake iwapo asingeondoka madarakani hadi saa ya mwisho ya kumalizika kwa muda wake ambayo ilikuwa usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa iliyopita.

Wakati majeshi hayo yakipiga kambi eneo hilo tayari kwa lolote kwa baraka za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), Mkuu wa Majeshi wa Gambia, Jenerali Ousman Badjie alitangaza kutoliingiza jeshi lake vitani iwapo majeshi ya kigeni yangeingia katika ardhi ya Taifa hilo.

Jenerali Badjie alitoa kauli hiyo muda mfupi tangu Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz, kuondoka Gambia baada ya kushindikana kwa jitihada za mwisho za kumshawishi Jammeh aachie ngazi kwa hiari.

Jenerali Badjie, awali wakati Rais mteule wa Senegal, Adama Barrow, alipotangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Desemba mwaka jana, alimwahidi mgombea huyo wa Upinzani ushirikiano baada ya Jammeh pia kukubali kushindwa.

Lakini alibadili msimamo baada ya Jammeh aliyekuwa madarakani kwa miaka 22 kugeuka kwa kuyakataa matokeo yaliyompa ushindi Barrow.

Lakini tena baadaye Ofisa huyo wa ngazi ya juu katika Jeshi la Gambia, alisema kuwa hawezi kuwaingiza vijana wake katika mapigano ya kipuuzi. Mh, alikuwa naye anapiga ramli kwa upande wake!

Muda wa Rais Jammeh ulikuwa mefikia kikomo lakini bado alikuwa amekaidi kuachia ofisi baada ya kushindwa na mpinzani wake.

Ung’ang’anizi wake ulizusha mashinikizo ya kumtaka aachie ngazi kutoka kwa mataifa ya Afrika Magharibi, baada ya kushindwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia.

Nigeria na Ghana mbali ya kuandaa meli za kivita tayari kwa lolote, zilipeleka majeshi na ndege za kivita Senegal; na baadaye askari wakiwa na silaha walikusanyika katika mpaka wa Gambia.

ECOWAS iliipa Senegal jukumu la uongozi kwa sababu Taifa hilo limeizunguka Gambia pande zote, isipokuwa baharini.

Taarifa zinasema kuwa katika operesheni hiyo, Mkuu wa Majeshi wa Senegal, Jenerali Francis Njie, ndiye angeongoza mapambano hayo yaliyokuwa yahusishe wanajeshi 860 kutoka Nigeria na 500 kutoka Senegal.

Pia, wangekuwapo makomandoo maalumu 60 wenye jukumu la kumsaka na kumkamata  Jammeh akiwa hai au vinginevyo.

Uhuni wa viongozi kugan’gania madaraka baada ya muda wao kuisha hauwezi kuvumiliwa.

Jammeh alikaa madarakani kwa miaka 22 na akalewa madaraka hayo.

Amelazimika kuondoka, tena na fedha nyingi za walipa kodi wa Gambia, baada ya kuona ataaibika! Ni mhuni huyu aliyekubuhu, eti?

Hakuona kuwa ametawala miaka mingi Gambia na Wagambia walikuwa wamekwisha kuamua kuwa muda wake umekwisha!

Alilazimika, bila kuwa na njia nyingine ya kukwepa, kuondoka nchini Gambia Ijumaa iliyopita Januari 20, mwaka huu.

Ijumaa hiyo hiyo ndiyo tulimpata Rais mpya wa Marekani, Donald Trump, Rais mwenye vituko kibao.

Kwa kweli Ijumaa ya Januari 20 ilikuwa ya kipekee Tanzania, Afrika na duniani kubeba mambo makuu matatu.

Kwa hapa nchini, Ijumaa ya Januari 20, mwaka huu itakumbukwa ikiwa ni siku ambayo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk. Abdallah Possi, aliandika barua ya kujiuzulu ubunge kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Dk. Possi amefikia hatua hiyo baada ya Rais Dk. John Magufuli kumteua kuwa balozi na kukomesha mjadala uliokuwa umepamba moto ukidai Rais Dk. Magufuli alikuwa amevunja Katiba.

Dk. Possi alikuwa miongoni mwa wateule wa ubunge wa Rais Magufuli.

Lakini kwa upande wa Afrika, Jammeh alikubali kuondoka madarakani baada ya kukataa kukubali kushindwa Ijumaa Januari 20 hiyo.

Lakini kwa upande wa dunia Januari 20, mwaka huu itakumbukwa kwa kuwa Rais wa 45 wa Taifa kubwa na lenye nguvu, Marekani,  Trump, aliapa kuliongoza Taifa hilo kwa miaka minne.

Wakati Trump akiapa watu wanaopinga utawala wake waliendesha maandamano nchini Marekani na nje ya Marekani!

Mh, lakini maisha yanaendelea!