Home Habari kuu JANGA LA WALIMU

JANGA LA WALIMU

3084
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

TAIFA linakabiliwa na janga la uhaba mkubwa wa walimu wa shule za sekondari, msingi na wa elimu ya awali (Chekechea) wa masomo yote.

Uhaba huo hauwezi kuzibwa katika kipindi cha miaka 20 ijayo kwa sababu serikali haina uwezo wa kusomesha na kuajiri walimu wapya kulingana na mahitaji yaliyopo katika sekta ya elimu.

Taarifa za kuwapo kwa janga hili katika sekta ya elimu zimeibuliwa na baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari na baadaye kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti la RAI katika shule mbalimbali hapa nchini kuhusu tatizo la uhaba wa walimu nchini umeonyesha kuwa shule za msingi na sekondari zina uhaba wa walimu 180,000 huku serikali ikiwa na uwezo wa kuziba uhaba huo kwa theluthi moja pekee.

Walimu wakuu waliozungumza na RAI kwa nyakati tofauti na kuomba majina yao yahifadhiwe, walisema wakati serikali ikiwa imesitisha ajira mpya zikiwamo za walimu kwa wastani wa mwaka mmoja sasa, hali ya uhaba wa walimu imeanza kutishia mwenendo wa ufundishaji mashuleni kwa sababu ya uwepo wa idadi kubwa ya walimu wanaostafu au kuondoka katika ajira kwa sababu mbalimbali.

Wakati walimu hao wakieleza hayo, RAI katika uchunguzi wake limebaini kuwa serikali ina vyuo vya ualimu na vyuo vikuu vinavyofundisha ualimu vipatavyo 40 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha walimu 12,000 kwa mwaka.

Akizungumzia hali hiyo, Oluoch alilieleza RAI kuwa taifa lina shule za msingi 15,000 ambazo zina walimu 200,000 wakati mahitaji yake halisi ni walimu 300,000 hivyo kuwa na upungufu wa walimu 100,000.

Oluoch alisema kwa upande wa shule za sekondari zipo 4,650 na zina walimu 85,000 wakati mahitaji halisi ni walimu 135,000 hivyo zina upungufu wa walimu 50,000.

“Hili la uhaba wa walimu ni janga, serikali haijawa wazi kwa sababu hata walimu wa masomo ya sanaa wanaodaiwa kuwa wapo wa kutosha siyo taarifa sahihi kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa walimu wa lugha ya Kiingereza isipokuwa masomo ya Kiswahili, Historia na Jiografia. Haya masomo matatu pekee ndiyo yana walimu wa kutosha.

“Walimu waliopo vyuoni wanaopaswa kufundisha shule za msingi hawafiki 30,000 na hao waliopo CWT tulitaka waajiriwe mwaka jana kwa sababu kazi ya ualimu ni tofauti na nyingine, inakwenda na mitaala ambayo inatumia siku 194 kwa wanafunzi kupata elimu, ajabu walimu hao hawajaajiriwa hadi leo.

“Sasa Januari inakatika hakuna ajira zilizotangwa, ikifika Machi serikali ikatangaza ajira mwalimu lazima atumie muda wa mwezi mmoja kufanya maandalizi ndipo aingie darasani kufundisha. Kwa mantiki hiyo wanafunzi hawatafundishwa kwa miezi minne.

“Tunaona nusu ya mwaka inaweza kupita bila wanafunzi hawa kufundishwa lakini mitihani watatungiwa kufuatana na mitaala iliyopo. Hapo wanafunzi wasipofaulu walimu ndiyo wanatupiwa lawama,” alisema Oluoch na kuongeza kuwa;

“Hata Rais akiamua leo kuajiri walimu 50,000 wa sekondari hatawapata kwa sababu hawapo. Wachache waliopo walitakiwa kuajiriwa tangu mwaka jana lakini hadi leo wapo mtaani.”

Alipoulizwa kuhusu masomo ambayo yana uhaba mkubwa wa walimu kwa shule za sekondari Oluoch aliyataja masomo hayo kuwa ni uraia linalowajengea wanafunzi uzalendo kwa taifa lao, Fizikia, Hisabati, Kiingereza, na Biolojia.

Kuhusu shule za msingi alisema wanafunzi wanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili hivyo hawana msingi mzuri wa lugha ya kiingereza lakini wanajiunga na masomo ya sekondari wanakosa waalimu bora wa somo hilo.

“Upungufu umekuwa mkubwa sana kwa sababu kwa mwaka kuna walimu 5,000 hadi 6,000 wanaostaafu au kuondoka kwenye ajira kwa sababu mbalimbali na hawa nafasi hazijazwi kwa sababu ajira zimesitishwa.

“Takwimu hizi zipo wazi na serikali inazijua. Sisi katika CWT walimu wanapostaafu tunawapa mkono wa kwaheri na mabati 20. Hata hivyo kiwango hiki cha walimu kustaafu si kikubwa sana kwa sababu asilimia 92 ya walimu wa sekondari wana umri chini ya miaka 40 hiyo ina maana kuwa watu wenye umri kuanzia miaka 40 kwenda juu ni asilimia nane tu isipokuwa tatizo ni kwamba wanapoondoka nafasi zao hazizibwi.

“Asilimia 82 ya walimu wa shule za msingi wana umri wa miaka 40 kurudi chini, hiyo ina maana kwamba wenye miaka 40 kwenda juu ni asilimia 18 hivyo wanaostaafu ni wachache kuliko wanaobaki lakini miaka michache ijayo hawa watastaafu katika kipindi kinachokaribiana na hilo litasababisha tatizo.

“Sasa sisi katika CWT tunadhani kuwa mbali takwimu zilizo ofisini kwetu za wastaafu ambazo inazijua lakini haina takwimu sahihi za walimu waliopo nchini kwa sababu kusema nchi ina walimu wengi wakati kiuhalisia siyo sahihi ni wazi kuwa hapo kuna tatizo la takwimu sahihi za watumishi serikalini,” alisema Oluoch.

Akizungumzia taarifa za kuwepo kwa janga hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, alisema ni kweli kuna uhaba wa walimu kwa shule za sekondari, msingi na chekecheka lakini si kutisha kwa kiwango kilichozungumzwa na CWT na baadhi ya walimu wakuu.

“Sidhani kama kuna uhaba wa kiasi hicho katika shule zetu kwa sasa, ila nakiri kuna uhaba wa walimu wa Sayansi katika shule zetu, hata serikali hatulikatai hilo na mwanzo  tulikotokea kweli kulikuwa na kila kero hadi kuitwa yeboyebo ila sasa kumekuwa na walimu, hatujasitisha kudahili walimu.

“Lakini walimu waliohitimu tunatoa uwanda mpana kwa wahitimu hao kuweza kuanzisha hata shule zao, kwa sababu sekta ya elimu inazidi kukua, tena atakuwa mwendesha shule mzuri kwa sababu tayari anayo taaluma, tofauti na watu wenye fedha wanaofungua shule hovyo hovyo.

“Kwa mfano shule za binafsi bado tunaruhusu kuchukua walimu nje kwa sababu hakuna walimu wa kutosha. Kwa hiyo walimu wanaozalishwa kweli bado wapo, tena kuna changamoto ya ongezeko kubwa la walimu katika meneo ya mijini jambo ambalo limekuwa changamoto kwa serikali kwa sababu unakuta mtu ameolewa au ameoa anahitaji kuhamia kwa mwenziwe.

“Au wanahitaji kupata matibabu kwa karibu, hivyo haki za binadamu nazo zimewalazimu kuja mijini wengi kiasi cha kugawana masomo,” alisema Naibu Waziri Manyanya.

Aidha, akizungumzia msimamo wa serikali kutangaza ajira mpya siku za usoni au kutotangaza alisema hilo bado linafanyiwa kazi kuajiri kunahitaji vigezo vingi.

“Suala la kuajiri siwezi kulitolea tamko sasa kwa sababu halihusu taasisi moja, pia linaangalia vigezo vingi, huwezi kuajiri watu wengi kwa pamoja wakati maeneo ambayo yanahitaji nafasi ni chache.

“Kuna mambo mengi ambayo tunayaangalia katika kutoa ajira. Ndiyo maana hata hao wanaolalamika walipewa ajira miaka ya nyuma wakaenda kwenye vituo wakarudi au hawakwenda kabisa sasa wanataka kurudi wakati nafasi imeshabana, kwa hiyo kusema hakutakuwa na ajira siwezi kulitolea msimamo hilo kwa sababu suala la ajira linahitaji uchanganuzi wa vigezo vingi vya mahitaji,” alisema.